Kisa kocha, vigogo Dodoma wajifungia

MABOSI wa Dodoma Jiji wanatarajia kukutana muda wowote kuanzia sasa ili kujadiliana masuala mbalimbali ya timu hiyo, huku ajenda kubwa ikiwa ni ishu nzima ya mustakabali wa kocha wa kikosi hicho raia wa Rwanda, Vincent Mashami.

Hatua hiyo imejiri baada ya Dodoma Jiji kutozwa faini ya Sh15 milioni na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kutokana na kucheza mechi tatu msimu huu bila kocha mkuu, baada ya Mashami kutokidhi vigezo vya kikanuni vya kuongoza benchi hilo la ufundi.

Mashami aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akichukua nafasi ya Mecky Maxime, anatakiwa kuboresha leseni yake ‘Refresher Course’, kwa sababu ya sasa aliyonayo ya CAF A haimruhusu kusimama akiwa kocha mkuu, kwani anatakiwa awe na UEFA Pro.

Taarifa kutoka timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti mabosi wa kikosi hicho unakutana kujadiliana juu ya suala hilo ili lisiendelee kuwatia hasara kutoka kwa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB), ingawa kumuondoa sio kipaumbele kwa sasa.

“Lengo la kukutana ni kuangalia kama hizi wiki mbili anaweza kupata kozi fupi ya maboresho ‘Refresher’, kwa sababu faini tulizopata ni kubwa na zinaturudisha nyuma, tuna imani naye sana na suala la kumuondoa halipo,” kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson, alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia suala hilo, amesema kama kutakuwa na habari zozote zinazoihusu timu hiyo wataweka wazi, hivyo mashabiki waendelee tu kusapoti kikosi hicho.

Timu hiyo imecheza mechi tatu za Ligi Kuu bila ya kocha mkuu, ikichapwa bao 1-0, dhidi ya KMC, Septemba 17, ikatoka sare ya mabao 2-2 na TRA United zamani Tabora United, Septemba 20, kisha ikaifunga pia Coastal Union 2-0, Septemba 27, 2025.

Mashami aliyewahi kuifundisha timu ya Taifa ya Rwanda, ‘Amavubi’, amejiunga na kikosi hicho cha Dodoma Jiji kwa mkataba wa mwaka mmoja, akitokea Police ya Rwanda, aliyodumu nayo kwa miaka mitatu na kutwaa mataji mbalimbali ikiwamo Peace Cup 2024, Super Cup 2025, na kuiwezesha timu hiyo kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupita takribani miaka 10, huku akitwaa pia ubingwa wa ligi akiwa na kikosi cha APR ya Rwanda.