::::::::
Na Mwandishi Wetu,
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga na Mwanasiasa Mkongwe, Khamis Mgeja amejitosa kumpigia kampeni mgombea urais wa chama hicho, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mgeja ambaye alikuwa nchini India kwa matibabu, amerejea na kuingia moja kwa moja kwenye mapambano ya kuomba kura za Dk. Samia.
Mkongwe huyo wa siasa, jana aliungana na wanachama wa chama hicho wa kata ya Kilago, kuhamasisha wananchi wamuunge mkono Dk. Samia katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Mgeja, akiwa mwenye afya na ari kubwa kisiasa, alimwaga Sera na Ilani ya CCM katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Wame Kilago, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Mbali ya kumnadi Dk. Samia, Mgeja alimnadi mgombea Udiwani wa Kata hiyo, Bertha Daudi Lwamala, akisisitiza kuwa chama hicho hakina desturi ya kuwatupa wanachama waliopoteza katika kura za maoni, bali ni suala la “kupokezana kijiti kwa amani na upendo”.
“Chama chetu hakijawahi kumtupa mwanachama. Wale waliopoteza kura za maoni ni sehemu ya familia ya CCM. Hii ni zamu ya Dada yetu Bertha, na jukumu letu ni kumpa ushirikiano na kuhakikisha CCM inaendelea kushinda kwa kishindo,” alisema Mgeja huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Aidha aliendelea kusisitiza kuwa CCM haina utamaduni wa kuwatupa wanachama wake wanaoshindwa kwenye mchakato ndani ya chama, hivyo aliwataka kuungana kuhakikisha Rais Samia anashinda tena, pamoja na wabunge na madiwani wake.
“CCM hatutupani ila tunapangana tu wale wote walioshindwa ndani ya chama, hawajatupwa kwa sababu uongozi ni kupokezana kijiti, leo atatoka Mheshimiwa Kishimba, atakuja Benjamin Ngaywa vile vile na udiwani, hawa wengine wanabaki kuwa hazina ya chama ndiyo utamaduni wa CCM,” alisema Mgeja.
Pia Mgeja alimpongeza Dk. Samia kwa uongozi wake thabiti na jitihada kubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi, kuleta maendeleo ya kijamii na kuendeleza siasa za upendo, umoja na maridhiano.
“Wananchi wenzangu, tunapomchagua Dk. Samia maana yake tunachagua maendeleo, tunachagua amani, tunachagua Muungano wetu, kwa maana hiyo tukimchagua Mama, nchi yetu, itakuwa katika mikono salama. Kwa hiyo nawaomba sana tarehe 29 tumpe kura zote, ninyi wenyewe ni mashahidi tukisema tuzungumzie mafanikio ya Rais wetu tutachukua siku tatu, alisema Mgeja.
Aliwataka wananchi Kata ya Kilago, kutopoteza muda ifikapo tarehe 29, Octoba wakaipigie kura CCM ili Tanzania iendelee kuwa na utulivu na amani.
“Dk. Samia amekuwa kielelezo cha amani na maendeleo. Hivyo ninawaomba wananchi wa Kilago na Shinyanga kwa ujumla, tumpe tena kura zetu zote ili aendelee kutuletea maendeleo na kudumisha amani nchini,” alisisitiza.
Mgeja pia alitumia fursa hiyo kuhimiza amani na utulivu katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi, akiwataka wananchi kuepuka maneno ya uchochezi na migogoro inayoweza kuvuruga mchakato wa kidemokrasia.
“Uchaguzi ni sehemu ya maisha ya kidemokrasia. Tofauti za kisiasa zisigeuke chuki. Tuendelee kuwa wamoja kama Watanzania,” aliongeza.
Hata hivyo Mgeja alisema Kata ya Kilago, wameandika historia kwa kumchagua mgombea Udiwani mwanamke Bertha Lwamala na kuwataka tarehe 29, wathibitishe kwa kumpigia kura nyingi ili akashirikiane na Mbunge mtarajiwa, Benjamin Ngayiwa kuleta maendeleo.
“Niwaambie wananchi wa kata ya Kilago mmeandika historia kubwa sana kwamba tangu nchi ipate uhuru, ndio wanapata diwani mwanamke kwa mara ya kwanza. nawaombeni msimwangushe Mama huyu ili akatuletee maendeleo, lazima tumuunge mkono, kazi yetu ni moja tu siku ya tarehe 29,” alisema.
Kwa upande wake mgombea udiwani Kata ya Kilago, Bertha Lwamala aliwaeleza wananchi hao kuwa kuanzia sasa ana deni kubwa la kuwatumikia wananchi wake na kazi yao ni moja kwenye sanduku la kura ifikapo tarehe 29 oktoba.
Wananchi wa Kilago walionekana kufurahia ujio wa Mgeja, wakimpongeza kwa moyo wake wa uzalendo na kujitolea kuendelea kukitumikia chama licha ya changamoto za kiafya alizopitia.