Butiku: Suala la amani, mshikamano nchini si la kuchezewa

Musoma. Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere (MNF), Joseph Butiku amewaomba Watanzania kupuuza taarifa zilizotolewa jana Oktoba 4, 2025 na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Kapteni wa Jeshi la Wananchi Tanzania, JWTZ (Kapteni Tesha), akilitaka jeshi hilo kuchukua hatua.

Butiku ametoa ombi hilo mjini Musoma leo Jumapili Oktoba 5, 2025 alipokutana na waandishi wa habari ambapo amesema suala la amani umoja na mshikamano wa kitaifa linapaswa kuwa kipaumbele kwa Watanzania wote bila kujali umri, jinsia, dini wala kabila.

Amesema Watanzania wote wanapaswa kuunga mkono kauli iliyotolewa na jeshi hilo jana kupitia Kaimu Msemaji wake, Kanali Bernard Mlunga. Ambapo pamoja na mambo mengine Kanali Mlunga alisema jeshi hilo linaendelea na utekelezaji wa majukumu yake kikatiba kwa uhodari na kuzingatia kiapo chao.

Amewataka vijana nchini kujiepusha na kutoshabikia matamko ambayo kwa namna moja ama nyingine hayana nia nzuri na amani iliyopo nchini, ambayo inatakiwa kulindwa kwa nguvu zote na kwa wivu mkubwa.

Amesema yeye binafsi anaamini kuwa mtu huyo si mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania kutokana mambo mbalimbali ikiwemo mwonekano na mavazi yake ambayo hayaakisi hali halisi ya jeshi hilo.

“Labda naomba mfahamu kuwa mimi ni askari mstaafu wa cheo cha Meja, hivyo mtu yule kwa mwonekano wake tu si askari, kwanza ana ndevu pia amevaa fulana inayoonyesha kuwa na rangi ya jeshi lakini imefika hadi kwenye koo vitu ambavyo havipo jeshini,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Kama Kapteni Tesha ni mwanajeshi basi atakuwa na jeshi lake na sitaki kuamini kuwa ndani ya nchi yetu kuna jeshi lingine tofauti na hili la wananchi.”

Butiku amesema Watanzania wanapaswa kuwa na imani na jeshi hilo na kamwe wasiyumbishwe na watu ambao amesema hawaitakii mema nchi kwa sababu wanazozijua wenyewe.

“Wakati mwingine mnaweza kuwaona wanajeshi huko kwenye siasa sio kwamba wakionekana ndio wanajihusisha na siasa hapana, unaweza kukuta wapo huko kwa kazi zao za kijeshi na hiyo isiwape shida kwani jeshi letu halishikamani na chama chochote cha siasa,” amesema.

Amesema yeye kama mzee wa Tanzania hajafurahishwa na hali hiyo iliyojitokeza na kuwataka wazee wengine kujitokeza na kukemea vitendo vya aina hiyo, huku akiwaomba Watanzania kwa ujumla kuliunga mkono jeshi hilo chini ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan.

“Askari anaruhusiwa kupiga kura siku ya uchaguzi na sio vinginevyo, Watanzania tusiwaruhusu watu kama hawa kutupeleka pabaya kwa kisingizio cha siasa, sisi askari hatuna tabia kama ya Tesha,” amesema Butiku.

Butiku ambaye pia ametumikia Serikali kwa nyadhifa mbalimbali zikiwamo za ukuu wa Mkoa wa Mara pamoja na kuwa msaidizi wa Rais wa awamu ya kwanza hayati Julius Nyerere, amewataka Watanzania kutokuruhusu watu kulihusisha jeshi hilo na siasa jambo ambalo amesema sio zuri kwa ustawi wa nchi na jeshi pia.

Amesema Watanzania wanapaswa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu, ili kuwapata viongozi wanaowataka kwa mujibu wa Katiba ya nchi na si vinginevyo.

Wakati huohuo Jukwaa la Wahariri Tanzania, TEF limelaani kauli ya watu hao wawili waliojitambulisha kuwa ni wanajeshi wakihamasisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiingiza kwenye siasa kwa njia ya mapinduzi.

Katika tamko hilo, lililosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile leo Jumapili Oktoba 5, 2025 pia limeonya watu wanaojiita wanaharakati wanaosambaza matusi dhidi ya viongozi wa nchi mitandaoni, badala ya ajenda au sera.

Pamoja na hayo TEF imepongeza hatua ya haraka ya JWTZ kutoa taarifa kwa umma kukemea matendo hayo ndani ya muda mfupi.

“Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni wa saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Ni kawaida kuona joto la kisiasa na mijadala mikali ya sera nyakati za uchaguzi, lakini si hoja za kupinduana. Tunashuhudia nchi zilizofanya mapinduzi jinsi watu wao wanavyoishi kwa mateso, umwagaji damu, uharibifu wa mali na kudhoofisha taasisi za nchi,” imeeleza taarifa hiyo.

Imeeleza kuwa wanajeshi wa Tanzania hawaruhusiwi kuwa wanachama wa vyama vya siasa na msingi huu ndiyo ngao ya amani na utulivu wetu.

“Kauli za kujaribu kuchochea jeshi uasi ni hatari, zinavunja misingi ya Taifa na kuharibu mwelekeo wa Taifa lolote duniani. TEF inaasa vyama vya siasa visijihusishe kwa namna yoyote na fikra za mapinduzi kama njia ya mkato kuingia madarakani, bali vijijenge kiushindani kisera, vikiamini katika nguvu ya sanduku la kura.

“TEF tunatoa angalizo maalumu kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii. Tumeshuhudia mitandao ikitumika kusambaza taarifa zisizo sahihi, picha na video zenye upotoshaji na matusi zinazoweza kuhatarisha amani ya Taifa letu…

“Tunasihi Watanzania kuwa makini na kuchunguza ukweli kabla ya kusambaza taarifa kwenye simu. Wenye mitandao watangulize maadili, uzalendo na uwajibikaji, badala ya kugeuza majukwaa hayo kuwa vyanzo vya hofu na chuki,” imeeleza taarifa hiyo.

Pamoja na hayo TEF imevitaka vyama vya siasa navyo visikalie kimya kauli zenye mwelekeo wa uchochezi.

Imeeleza kila chama kinapaswa kujitenga na matamko hayo kwa kuyalaani bila woga, kwa nia ya kulinda umoja, maisha na mali za watu. Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja na mshikamano. Njia pekee ya kuendeleza uongozi ni kupitia demokrasia na ridhaa ya wananchi.

“TEF tunakemea kauli za kuhamasisha mapinduzi, tunaipongeza JWTZ kwa uaminifu wake kwa Katiba, na tunasihi Watanzania wote kulinda amani na umoja wa Taifa letu, muda wote,” imeeleza taarifa hiyo.