Na Said Mwishehe,Michuzi-Dodoma.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya kampeni za kistaarabu, zinazozingatia utu wa mtu huku kikitoa mwito kwa kila Mtanzania kuwa mlinzi wa amani ya nchi, kwani amani na utulivu ndiyo tunu yetu Watanzania.
Akizungumza leo Oktoba 5,2025 Mjini Dodoma alipokuwa akitoa tathimini ya mikutano ya kampeni ya mgombea urais kupitia Chama hicho Dk.Samia Suluhu Hassan, Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo Kenan Kihongosi amesema kampeni zinazofanywa na mgombea wao zimekuwa za kuhimiza umoja,amani ,upendo na mshikamano pamoja na utu wa Mtanzania.
“Nitoe mwito kwa kila Mtanzania kuwa mlinzi ww amani ya nchi ,kwa kuwa amani na utulivu ndio tunu yetu Watanzania.Na CCM tunaamini chini ya uongozi wa Dk.Samia Suluhu Hassan nchi yetu iko salama na itaendelea kuwa salama.
“Tumeshuhudia tangu alipozindua kampeni pale Kawe jijini Dar es Salaam na kote ambako amepita mgombea wetu Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya kampeni za kistaarabu, zinazozingatia utu wa mtu.”
Hata hivyo amesema katika kipindi hiki cha lala salama, CCM imejipanga
kikamilifu kuhakikisha inamfikia kila Mtanzania na kumhamasisha akapige kura.
“Tumejipanga kupata ushindi wa kishindo kwa mgombea wetu wa urais wabunge na madiwani.” Amesema Kihongosi alipokuwa akitoa tathimini ya mikutano ya kampeni ya mgombea urais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Kihongosi ni kwamba tangu kuanza kwa kuanza kwa mikutano ya kampeni ya kampeni mgombea wao wa urais, Dkt Samia Suluhu Hassan, ameshafanya mikutano 77, katika mikoa 21, kwenye kanda za Kati, Magharibi, Pwani, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pemba na Unguja (Zanzibar), vilevile Kanda ya Kaskazini.
“Zaidi ya watu milioni 14.62 wamejitokeza kwenye mikutano moja kwa moja. Watu milioni 31.6, wamefuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mikutano yote hiyo, kanda kwa kanda, mkoa hadi mkoa, mahudhurio yamekuwa makubwa.”