SIKU chache baada ya kutambulishwa na kutua rasmi kuanza kazi ndani ya Simba, Meneja Mkuu wa timu hiyo, Dimitar Pantev, jambo jipya limeibuka.
Jumatatu ya Oktoba 6, 2025, anatarajiwa kuanza rasmi kazi ya kuinoa timu hiyo inayorejea kutoka mapumziko baada ya kucheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, ukiweka kando lile la kukosa vigezo vya kuwa kocha mkuu, imefichuka Yanga ilikaribia kumnasa kocha huyo Mbulgaria.
Pantev ametua nchini Oktoba 4, 2025 akitokea Gaborone United ya Botswana iliyotolewa wiki iliyopita na Wekundu hao katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Jumatatu anaanza kazi na kujitambulisha rasmi kwa wachezaji baada ya kufanya hivyo kwa benchi la ufundi lililosalia baada ya Fadlu Davids na wenzake kutimkia Raja Casablanca ya Morocco.

Mapema mara baada ya kutua nchini, kocha huyo alijinasibu kwamba amekuja kufanya kazi na kufafanua soka lake ni la kushambulia na anaamini kuna makubwa atayafanya na wenzake kwa vile timu hiyo ina wachezaji bora wanaoweza kuendana na falsafa yake ya 4-3-3.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 na anayetambulika kirahisi kwa kuwa na michoro mwilini mwake (tattoo) na kuvaa kwake hereni, ametua Msimbazi akiwa na kazi kubwa ya kuirejeshea heshima timu hiyo inayosotea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la FA kwa msimu wa tano sasa.
Simba msimu uliopita ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji mbele ya RS Berkane ya Morocco iliyoshinda kwa jumla ya mabao 3-1, kazi ambayo Dimitar atakuwa na kazi kuivusha katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ina rekodi ya kucheza robo fainali mara kadhaa.

ISHU YA YANGA
Lakini wakati kocha huyo akianza rasmi kazi leo, inaelezwa Yanga ilikuwa ikimpigia hesabu Dimitar, licha ya kuwa na Romain Folz ikiwa na lengo la kutaka kumfanya mbadala kutokana na shinikizo lililopo baada Mfaransa huyo kuifanya timu icheze soka lisilovutia kama zamani.
Taarifa kutoka Yanga zimelidokeza Mwanaspoti, mabosi wa klabu hiyo waliwasiliana na Dimitar mara ilipomwona na Gaborone Utd ilipokuja kucheza na Simba na kumuulizia uwezekano wa kumpata.
Inadaiwa Yanga ilimvamia kocha huyo baada ya kuona soka la kocha huyo wakati akiiongoza Gaborone United ikipata sare ya bao 1-1 katika mechi hiyo ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, wakati Yanga inatua kwa Dimitar, kumbe kocha huyo alikuwa anasubiria tiketi ya ndege tu ili akamilishe dili lake la Simba.

Yanga pia ilikuwa inataka kupata uhakika wa vyeti vya kocha huyo na kabla ya kutumiwa ikajulishwa tayari Simba, imeshamalizana na Gaborone katika kununua mkataba aliokuwa nao.
“Tulikuwa kwenye mazungumzo kweli nadhani ni siku moja baada ya kumalizika kwa mechi ile timu ya Gaborone United na Simba. Wakati tunaongea naye kulikuwa na mambo tulitaka kujiridhisha kwanza, unajua kocha huyo hakukaa benchi katika mechi ya kwanza kule Francistown, Botswana.”
“Hata huu mchezo wa hapa, hakuorodheshwa kama kocha tukaambiwa kuna mambo yake hayako sawa, hivyo tukamuomba vyeti vyake,” chanzo hicho kilisema na kuongeza;

“Wakati tunasubiri vyeti akatujibu tayari ameshamalizana na Simba na anaheshimu mazungumzo aliyoyafanya na wenzangu, hivyo tukaachana naye.”
Yanga iko katika msako wa siri kutafuta kocha wa kuchukua nafasi ya Folz wanayempigia hesabu kutokana na shinikizo la mashabiki na kama itafanya hivyo itakuwa inarudia kile ilichofanya msimu uliopita ilipomtema Miguel Gamondi ikiwa katikati ya michuano huku akiweka rekodi kadhaa.