Azaki za kiraia zimependekeza ili kupatikana kwa katiba mpya ndani ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi, viongozi wote wa kisiasa, kijamii na kidini wanapaswa kuonyesha dhamira ya kweli ya kuhuisha mchakato wa katiba mpya kwa masilahi ya Taifa, badala ya masilahi binafsi au ya kisiasa.
Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa nchini vikionyesha utayari kuharakisha upatikanaji wa katiba mpya kupitia Ilani zao za uchaguzi, azaki za kiraia nchini zimependekeza Bunge la kwanza la Novemba mwaka huu lianze marekebisho ya sheria ya kupata katiba hiyo.
Azaki hizo zimependekeza kuwa upatikanaji wa katiba mpya ufanyike ndani ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi, huku wakisema kunapaswa kuanzishwa kisheria kamati ya wataalamu wasiozidi 25 watakaochakata na kuunganisha maoni ya wananchi.
Maoni yatakayochakatwa na kuunganishwa na wataalamu hao, ni yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, Katiba inayopendekezwa na Katiba iliyopo sasa.
Mapendekezo hayo yanakuja wakati huu wa uchaguzi ambapo asasi za kiraia zimerejea ahadi za wagombea kwenye vyama vya siasa ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), CUF, NCCR Mageuzi na ACT Wazalendo vimeahidi upatikanaji wa katiba mpya zikiunda serikali ndani ya siku 100.
Akizungumza leo Oktoba 5,2025 jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya azaki, Mratibu Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Wakili Onesmo Olengumwa amesema pendekezo la kupatikana kwa katiba ndani ya mwaka mmoja linalenga kuepusha kurudiwa kwa hali ya kusuasua na kupoteza mwelekeo kama ilivyotokea katika mchakato uliopita.
“Kuanzishwa kwa mchakato mapema kutatoa fursa ya kujenga ari ya kitaifa, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kisiasa, na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani kwamba katiba mpya ni kipaumbele cha Taifa,” amesema.
Amesisitiza kutoendesha mchakato wa katiba wakati wa uchaguzi kwa kuwa tayari madhara yameshaonekana ya kuendesha mchakato huo karibu na uchaguzi kama ilivyokuwa mwaka 2024/2015.
“Pia mchakato wa katiba mpya ukamilishwe kwa kura ya maoni, kwa kuwa hatua hii ndiyo itakayotoa uhalali wa mwisho wa katiba mpya mbele ya wananchi.
“Hatua hii itahakikisha katiba mpya inaakisi matarajio ya wananchi, na kuwa msingi imara wa uongozi na ustawi wa Taifa,” amesema
Ole Ngurumwa amesema kabla ya kuanza mchakato huo ni vyema kukawa na mwafaka wa kitaifa, kufanyia kazi mpasuko wa kitaifa uliotakana na changamoto za uchaguzi wa 2019/ na uchaguzi wa 2024
“Tuainishe hoja kuu zenye mgongano katika jamii kuhusu katiba mpya na kutafuta ya maridhiano ya kitaifa kabla ya kuanza mchakato wa kumalizia upatikanaji wa katiba mpya, hoja hizi ni pamoja na muundo wa muungano, mifumo ya uchaguzi, haki za binadamu, mgawanyo wa madaraka na mamlaka ya rais,” amesema.
Pia ameshauri kutibu majeraha ya kitaifa yaliyotokana na migawanyiko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi iliyoibuka wakati wa mchakato wa awali wa katiba mpya.
Ole Ngurumwa amesema ni muhimu Rais kusikiliza zaidi maoni ya wananchi na sio wale aliowaajiri kwa ajili ya kumshauri kwa kuwa wananchi ndio waliomuajiri.
Ahadi za vyama kwenye ilani
Mwenyekiti na mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya chama chake akiomba wananchi kumpa ridhaa ya kuunda Serikali ameahidi ndani ya siku 100 kuhuisha mchakato wa katiba.
Ahadi hiyo si tofauti na iliyotolewa na Chama cha Wananchi CUF, kilichoahidi mchakato wa uandaaji wa katiba mpya ya wananchi utafufuliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya chama hicho kushika hatamu.
Nako Chaumma kupitia Ilani yake kimeahidi ndani ya siku 100 baada ya kuunda serikali, kitawasilisha bungeni muswada wa sheria kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa katiba mpya.
Vilevile ACT Wazalendo imeahidi endapo kitachaguliwa kuongoza Serikali itafufua na kukamilisha mchakato wa katiba mpya ndani ya mwaka mmoja.