OMO: Tutarudisha miji mikononi mwa wananchi

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman ameahidi kurejesha uendeshaji wa miji visiwani humo, ukiwemo wa Chakechake mikononi mwa wananchi.

Hatua hiyo kwa mujibu wa Othman, inalenga kuwafanya wananchi wawe na uamuzi zaidi kuhusu usimamizi wa shughuli za maendeleo ya miji, tofauti na sasa.

Othman ameyasema hayo leo Jumapili, Oktoba 5, 2025, alipokuwa anahutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Chanjaani Chakechake, Pemba. Mgombea huyo amehitimisha ziara ya kampeni zake za kusaka kura kwa awamu pili kisiwani humo, kabla ya kurejea Unguja.

“Tutairejesha miji ukiwamo wa Chakechake mikononi mwa Wana Chakechake wenyewe. Waamue wapange wanataka kufanya nini katika mji wao huu,” amesema Othmani.

Amesema endapo wananchi wataridhia kuwapa kura waongoze dola, baada ya hatua hiyo Serikali yake itajikita katika kutoa vigezo vya nini kinahitajika ili eneo liwe na hadhi ya kuitwa mji, huduma na taratibu za uendeshaji biashara.

Amesema suala la uendeshaji wa miji litakuwa mikononi mwa wananchi kwa lengo la kuwapunguzia viongozi watakaoteuliwa kiburi katika mali za umma.

“Ukipewa nafasi ofisi ya umma, lazima uwe na heshima, adabu zako na lazima utimize na kufuata misingi ya kusimamia nafasi ya umma,” amesema Othmani.

Amesema hatua hiyo ndiyo itakayoikuza Chakechake na kuufanya kuwa mji wa wastaarabu kwa kuwa una rasilimali nyingi zinazoweza kuwatajirisha wananchi wake.

“Ahadi yetu ya mwanzo, kama tunataka tutoke hapa tulipo ni kuirejesha nchi hii mikononi mwenu wananchi. Tukishairejesha, atakayekaa kwenye Serikali atakuwa na adabu kwa sababu yupo mwananchi wa kumshikisha adabu,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, amesema Serikali yake itauunganisha Mji wa Chakechake na Uwanja wa Ndege, huku akiahidi kuwalipa fidia wananchi wote waliodhulumiwa baada ya kupisha utekelezaji wa mradi huo.

“Watu wanapiga mabilioni, wewe mwananchi nyumba yako unalipwa milioni saba au milioni 12 ukajenge wapi. Haiwezekani hii ndio dhuluma tunayokwenda kuikomesha,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesisitiza kuwa Serikali itakayoundwa na Othman haitakuwa na ubaguzi bali itawahudumia Wazanzibari wote pasipo kujali itikadi zao za kisiasa.


“Tukijaaliwa na Mungu Oktoba 29, tunakwenda kuinyoosha Zanzibar chini ya Othman Masoud, tuna nia ya dhati ya kuwatumikia Wazanzibari,” amesema Jussa ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi ya ACT – Wazanzibar, Zanzibar.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT – Wazalendo, Mansour Yusuph Himid amesema maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar haikuwa ghafla kama watu wanavyodhani, bali kulikuwa na historia ndefu ya kufikia mchakato huo.

“Miaka ya nyuma watu walidhulumiwa haki zao, siasa zetu zilikuwa za chuki na kuumizana, hizi ndizo sababu za msingi za Maalim Seif Sharif Hamad na Aman Abeid Karume kufikia mwafaka wa kuleta umoja na maridhiano Zanzibar, kwa maslahi ya Wazanzibari,” amesema Mansour.

Mansour ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya mariadhiano Zanzibar, amejenga hoja hiyo akirejea namna malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara kwa akidai vijana wanyimwa vitambulisho vya kupigia kura Oktoba 29.

“Zanzibar ni taifa la watu wastaharabu, watu wema, tunahitaji mabadiliko. Hatupaswi kuwa katika mazingira kama haya ya sintofahamu zisizokwisha kwa sababu hii si ahadi ya waasisi wa Zanzibar.”

“Walioasisi Zanzibar walitaka kila kitu kiwe haki kwa sawa kwa watu wote,” amesema Mansour.

Amesema kwa sasa Zanzibar inahitaji kiongozi anayejiamini, mwadilifu, mkweli na aliyeonesha kuwa nani kwa Wazanzibari kwa sababu nafasi ya urais haijaribiwi, mwenye sifa hizo si mwingine bali ni Othman wa ACT – Wazalendo.

“Mchagueni Othman Masoud Othman ili tuishi kwa heshima na umoja wetu, mshikamano wa kuijenga Zanzibar yetu. Hatuwezi kufika mahali au kupiga hatua za maendeleo ikiwa tunabaguana au kuchukiana,” amesema Mansour.