CCM kujenga kiwanda cha tumbaku Tabora

Tabora. Mgombea mwenza wa urais wa Tanzania wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ametoa ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha Tumbaku katika Jimbo la Tabora, Mkoa wa Tabora ili kupunguza gharama za usafirishaji lakini kuchagiza ajira kwa vijana.

Kiwanda hicho ni mwendelezo wa ahadi za CCM mkoani kuwainua wakulima kwani imewaahidi pia ujenzi wa kiwanda cha utafiti wa mbegu za kilimo.

Leo Jumapili, Oktoba 5, 2025, Dk Nchimbi ameendelea kunadi ilani ya uchaguzi mkuu ya mwaka 2025/2025 katika Jimbo la Sikonge na kutoa ahadi mbalimbali ikiwemo za sekta ya kilimo, afya, elimu, mifugo na miundombinu ya barabara.

Katikati ya ahadi hizo, Dk Nchimbi amewaomba Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa chama hicho.


Dk Nchimbi amesema Mkoa wa Tabora unazalisha Tumbaku kwa asilimia 60 ya Tumbaku yote inayozalishwa nchini ambapo Sikonge ni miongoni mwa maeneo yanayolima Tumbaku kwa wingi.

“Katika ilani ya CCM, tumeahidi kuendeleza ushirikiano na taasisi mbalimbali kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata haki yao. Tunataka tumbaku ya Sikonge iwe kichocheo kikuu cha maendeleo kwa watu wake,” amesema Dk Nchimbi.

Dk Nchimbi ameaema chama hicho kitaboresha majengo ya hospitali ya wilaya ya Sikonge, kuongeza vifaa tiba na kuongeza wataalamu wa kutosha ili kuimarisha huduma za afya jimbo la Sikonge.

“Wataalamu wataletwa hapa wakutosha kuhudumia watu wetu wa Sikonge na vifaa vitaongezwa hapa tena vya kisasa kabisa na chama cha mapinduzi kimedhamiria kwa dhati kuboresha afya za wanaSikonge,” amesema Dk Nchimbi.

Mgombea mwenza huyo ameahidi CCM itajenga shule mpya  mbili za sekondari na kuongeza vyumba vya madarasa 80, itajenga shule mpya mbili za msingi na kuongeza vyumba vya madarasa 120 katika jimbo la Sikonge na wakati huo itajenga pia stendi mpya ya mabasi Sikonge.

“Miundombinu ya elimu hapa itaimarishwa pamoja na kujenga shule mpya watoto wetu wapate elimu katika mazingira mazuri ukizingatia elimu ni haki yao ya msingi na ndio maana tunaitoa bure,” amesema.

Upande wa maji na barabara, Dk Nchimbi amesema zitajengwa barabara kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Ipole mpaka Rungwe na zitajengwa barabara za changarawe katika jimbo hilo na maji ya ziwa Victoria yatazambazwa  maeneo yote ya jimbo la Sikonge.

“Hapa hatutazungumzia changamoto ya maji safi na salama kwa sababu tutaleta maji safi na ya kutosha kutoka ziwa Victoria lakini pia tutajenga barabara mpya za lami na za changarawe nyie tupeni tu ridhaa,” amesema Dk Nchimbi.

Mratibu wa kampeni kwa kanda ya kati na aliyekua katibu mkuu mstaafu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally  amesema kanda ya kati itashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na kura nyingi zilizomchagua mgombea urais wa chama hicho Samia huku akiwapa pole wale wote wanaotikisa msingi wa mahusiano mema yaliyopo.

Kwa upande wake, mgombea  ubunge wa Sikonge, Amos Maganga amesema kilimo cha Tumbaku kilikuwa na changamoto ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika lakini kwa sasa hakuna changamoto katika kilimo cha zao hilo.


“Kwa sasa tunashukuru sana soko la Tumbaku linaleta matumaini kwa wakulima wa hapa Sikonge na tunaendelea kuzalisha kwa kasi kwa kuwa tuna uhakika wa masoko,” amesema Maganga.

Amemuomba mgombea mwenza kuwa endapo CCM itapata ridhaa basi itafute masoko ya uhakika ya asali kwani kwa sasa Sikonge inalima zaidi ya tani 6000 lakini masoko ya uhakika hakuna.

“Tunakabiliwa na changamoto ya masoko ya uhakika ya asali yetu kwa hiyo tunaomba sana tusaidiwe endapo CCM itapata ridhaa,” ameomba.