Sheikh Njalambaha: Waislamu tuitumie sharia mahakamani

Mbeya. Waumini wa dini ya Kiislamu wameshauriwa kutumia sharia za dini yao mahakamani kudai au kuomba haki, badala ya kuiingizia Serikali gharama kubwa za kuwaandaa wataalamu wasiotumika.

Ushauri huo umetolewa leo Jumapili Oktoba 5, 2025 na Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Msafiri Njalambaha wakati wa mahafali ya kwanza ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu Mar-wa tawi la Mbeya.

Sheikh Njalambaha amesema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya waumini kutozingatia matumizi ya sharia mahakamani licha ya Serikali kuweka mfumo huo rasmi.

“Tutumie fursa hii na tushawishi wengine kutumia mifumo iliyowekwa na Serikali. Itakuwa ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya waumini wakikataa kutumia sharia za dini mahakamani. Serikali ikiona hakuna watumiaji itaziondoa, tutaandamana au kulalamika? amehoji.

Aidha, amepongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuwaleta Waislamu pamoja kupata elimu, akisema hatua hiyo itasaidia kuibadilisha jamii na Taifa.

Kwa upande wake, Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Dk Hassan Mbarazi amesema kumekuwapo mgongano wa kisheria kati ya sharia za dini ya Kiislam na sheria za Serikali, hasa katika masuala ya mirathi na ndoa.

“Kwa upande wa Uislamu, msichana anapovunja ungo anaweza kuolewa, lakini kwa sheria za nchi lazima awe na umri wa kuanzia miaka 18. Vivyo hivyo, Kiislamu mwanaume akimwambia mwanamke nimemuacha talaka inakuwa imetimia, lakini kisheria mahakama inahitaji maandishi,” amesema.

Hata hivyo, ameshauri kuwa tofauti hizo haziwezi kuwa kikwazo endapo mamlaka husika zitatoa maelekezo kwa wanaohitaji huduma ili kila upande uendelee kuheshimiwa.

Miongoni mwa wahitimu, Abdulhamid Said aliyemaliza shahada ya kwanza ya sharia, amesema watashirikiana na Serikali kuelimisha jamii, hususan wale wanaokwenda kinyume na maadili.

“Sharia za Kiislamu zinahitaji kufanyiwa kazi na waumini badala ya kuhadithiwa tu. Zipo pia sheria za nchi ambazo lazima tuziheshimu, maana tumeelekezwa kutii mamlaka iliyo juu yetu. Kwa kupitia elimu hii, tunaisaidia Serikali kupunguza migogoro,” amesema.