Dar/Mikoani. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua kilio cha wanachama na viongozi wao kukamatwa kwa nyakati tofauti maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Chadema, ndani ya wiki mbili makada na viongozi wa chama hicho, wamekamatwa na polisi huku wengine wakitoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo, baadhi ya maeneo Jeshi la Polisi limekuwa likitoa taarifa kuwa linafuatilia suala hilo, wakati Chadema wakiendelea kukitilia shaka kuhusu ufuatiliaji wa matukio hayo.
Kwa mujibu wa Chadema, matukio hayo yanaongezeka lakini Jeshi la Polisi halijatoa taarifa au ufafanuzi wa kina kuhusu kadhia iliyowakumba viongozi na wanachama hao.
Taarifa ya kukamatwa na kupotea kwa makada na viongozi wa Chadema ilitolewa jana Jumamosi Oktoba 4, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia akidai kuwa, kuna vijana wanne wamepotea katika mazingira ya kutatanisha Kata ya Bulyanhulu wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.
Rupia amedai kuwa, Ibrahim Mfangavo alichukuliwa kwa nguvu nyumbani kwao mbele ya wazazi wake na walipojaribu kuzuia asichukuliwe walitishiwa.
Mbali na hilo, Rupia amedai vijana wengine wanne wanaoendesha pikipiki waliokuwa wakifuatilia tukio hilo nao wametoweka katika mazingira ya kutatanisha, hata hivyo jambo hilo limeripotiwa katika kituo cha Polisi Bugarama.
Kwa mujibu wa taarifa ya Rupia, tukio jingine ni la Lobezi Masanyiwa aliyepotea Oktoba mosi wilayani Busega, lakini polisi hawakutoa taarifa wala kuchukua hatua zozote.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo akisema ufuatiliaji wa kina unaendelea ili kubaini ukweli.
“Ni kweli tumepokea taarifa kutoka Chadema na tumeanza kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hili,” amesema Kamanda Swebe wakati akizungumza na Mwananchi Oktoba 2, 2025.
Katika hatua nyingine, Rupia amedai Oktoba mosi, Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya ya kichama ya Kibamba, Ernest Mgawe pia alikamatwa polisi baada ya kuitikia wito wa jeshi hilo, kituo cha polisi Gogoni.
“Jeshi la polisi linamtuhumu Mgawe kuhamasisha maandamano na kuhamasisha fujo kwenye vituo vya mwendokasi, hadi sasa bado hajapata dhamana wala kufikishwa mahakamani,” amedai Rupia.
Mbali na Brenda, Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amedai kuwa ndani ya siku tano, makada wao wamepotea katika mazingira ya kutatanisha, pasipo polisi kutoa taarifa ya kina.
“Kumekuwa na matukio ya makada wa Chadema kuchukuliwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha, sio Shinyanga na Simiyu pekee, bali nimeambiwa hata Ikungi (Singida) kuna makada wetu hawaonekani,” amedai Mnyawami.
Wakati Mnyawami akieleza hayo, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amedai kuna wanachama wao wawili wamepotea katika mazingira ya kutatanisha huku sita wakiwamo viongozi chama hicho, wakishikiliwa na polisi bila kupewa dhamana.
Obadi amesema miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Khalid Hussein ambaye bado hajapata dhamana.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Belle Ponera amesema katika kanda yenye mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi, hakuna makada waliopotea, isipokuwa kuna watu wawili wanaodaiwa kuwa wafuasi wa chama hicho wanashikiliwa na polisi.
“Nimezungumza na mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Mtwara kulifuatilia tukio hili, lilitokea Masasi. Inadaiwa watu hawa walikuwa wanasambaza vipeperushi vya maandamano,” amesema Ponera.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Jimbo la Lupembe mkoani Njombe, Abedinego Sanga anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwenye eneo analofanyia biashara zake Matembwe jimboni humo.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Njombe, Seth Vegula ameeleza hayo leo Oktoba 5, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu.
Vegula amesema taarifa walizozipokea zinadia kuwa, Sanga alipotea saa moja na nusu usiku jana baada ya gari kufika katika eneo lake la biashara la duka la dawa.
“Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda alishuka mtu mmoja kutoka kwenye hiyo gari na kuingia dukani kisha kumwambia Sanga anahitajika kwenye gari lakini alikataa na kumuuliza kuna kitu gani.
“Baada ya Sanga kukataa alishuka mtu mwingine kutoka kwenye gari hiyo, ili kumshika kwa lazima ndipo mwenyekiti huyo alianza kupiga kelele za…ndipo majirani wakaanza kusogea eneo la tukio,” amedai Vegula.
Hata hivyo, Vegula amesema watu hao walijitambulisha kuwa wao ni askari polisi, ingawa hakuwaeleza kwa kina tuhuma za Sanga, badala yake waliondoka naye.
Baada ya kuondoka na Sanga, jitihada za kumtafuta mwenyekiti huyo zinaendelea ikiwemo kutoa taarifa kituo cha polisi Lupembe, sambamba kuwasiliana na wakuu wa polisi wa wilaya ya Njombe ili kujua kiongozi wao alikopelekwa.
Katibu wa Chadema Jimbo la Lupembe, Emmanuel Uhagile ameliomba Jeshi la Polisi mkoani Njombe, kufuatilia kwa kina tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema jeshi hilo limepokea taarifa za tukio hilo, baada ya kupigiwa simu usiku kuhusu sakata hilo.
“Kwa sasa askari wapo hapo Lupembe, kuna wananchi wanatoa maelezo na baada ya hapo tutaanza uchunguzi wa jambo hilo kubaini hilo.
“Siwezi kusema kama ni mtu wa Bavicha ametekwa ila kuna mtu amekamatwa na watu ambao bado hawajafahamika,” ameeleza Kamanda Banga.
Oktoba mosi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na wanahabari alisema polisi inawashikilia makada watano wa Chadema kwa tuhuma za kuchana mabango ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, makada hao walikamatwa Septemba 30,2025 katika maeneo tofauti jijini Mwanza, wakiendelea kuratibu mipango ya kuharibu mabango ya wagombea wa CCM.
Hata hivyo, Obadi aliiambia Mwananchi leo Jumapili kuwa, kati ya hao watano baadhi waliachiwa isipokuwa, makamu mwenyekiti wa Chadema wa kanda hiyo, aliyekamatiwa Muleba bado.