Mahakama ilivyowaachia wawili walioua bila kukusudia

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora, imewaachia huru kwa masharti, watu wawili waliokiri kuua bila kukusudia akiwemo Manase Kulwa, aliyekiri kumuua bila kukusudia mke wake Sophia Jidai, baada ya kumkuta akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.

Manase alimuua mkewe Oktoba 21,2024 katika Kijiji cha Mwambondo Wilaya ya Uyui, mkoani  Tabora baada ya kumkuta akifanya mapenzi na mwanamume mwingine ambaye alikimbia eneo hilo, na mshtakiwa kumpiga mkewe kwa fimbo hadi kupelekea kifo chake.

Hukumu hizo zimetolewa Oktoba 3, 2025 na Jaji Adam Mambi aliyekuwa akisikiliza na nakala zake kupakiwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji huyo alimtia hatiani Manase baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia.

Awali mshtakiwa huyo alisomewa shtaka la mauaji ila katika ombi lake alikiri kuua bila kukusudia.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa baada ya mshtakiwa kumkuta mkewe akifanya mapenzi na mwanamume mwingine ambaye alikimbia eneo hilo na kumuacha Sophia akiwa mtupu, mshtakiwa aliingia ndani na mkewe na kuanza kugombana ambapo alimpiga kwa fimbo na kusababisha kifo chake  .

Jaji amesema kwa kuwa mshtakiwa alikiri shtaka la kuua bila kukusudia, Mahakama inamtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha  195 ya Kanuni ya Adhabu.

Jaji amesema amezingatia ukweli na mazingira ya kifo cha marehemu ili kumuwezesha kuamua hukumu inayofaa ambapo kosa la kuua bila kukusudia ambalo alishtakiwa nalo Manase, linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha jela, chini ya kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu.

“Kutokana na ukweli kwamba kifo hicho kilitokana na ugomvi huo na lilikuwa ni kosa la kwanza kwa mshtakiwa kama ilivyokubaliwa na upande wa mashtaka chini ya kumbukumbu za kesi, mahakama imeona ni vyema kuzingatia adhabu ndogo,”

“Kwenye kumbukumbu kwamba mshtakiwa alikuwa na mgogoro, na marehemu lakini kwa bahati mbaya ugomvi huo ulisababisha kifo chake. Hii inaonyesha mtuhumiwa hakuwa na chuki ,”amesema Jaji.

Jaji amesema maamuzi mbalimbali ya mahakama yanaonyesha kuwa pale inapothibitika kuwa kifo kilitokana na ugomvi, mahakama inapaswa kuzingatia kuchagua kosa la kuua bila kukusudia ambapo pia ilizingatia muda aliotumia mshtakiwa akiwa rumande (zaidi ya mwaka mmoja).

Amehitimisha kuwa kwa kuzingatia mambo hayo na mazingira ya kifo cha marehemu, mshtakiwa anaachiwa kwa masharti kwa mujibu wa kifungu cha 38 cha Kanuni ya Adhabu.

Kwa mujibu wa kifungu hicho mtu anapoachiwa kwa masharti, anatakiwa kutotenda kosa lingine kwa muda usiozidi miezi 12.

Katika kesi ya pili, ambayo hukumu yake ilitolewa siku hiyohiyo, Mahakama hiyo ilimuachia huru kwa masharti, Mabhondo Kisinza ambaye pia alikiri kuua bila kukusudia.

Mahhondo alikiri kumuua Suzana Sangisangi, Desemba 24,2023 katika Kitongoji cha Mwamashimba, kilichopo Kijiji cha Imalaupina, wilayani Kaliua Mkoa wa Tabora.

Mshtakiwa alipofikishwa mahakamani alikiri kuua bila kukusudia na mahakama kumtia hatiani chini ya kidungu cha 195 cha Kanuni ya Adhabu.

Jaji Mambi amesema kutokana na ukweli kwamba kifo kilitokana na ugomvi baina ya hao wawili na lilikuwa ni kosa la kwanza kwa mshtakiwa, mahakama imeona ni vyema kuzingatia adhabu ndogo.

“Ni kwenye kumbukumbu kwamba mshtakiwa alikuwa na mgogoro na marehemu lakini kwa bahati mbaya ugomvi huo ulisababisha kifo chake. Hii inaonyesha mtuhumiwa hakuwa na chuki,” amesema Jaji

Jaji amesema pia amezingatia muda mshtakiwa aliotumia akiwa rumande ambao ni zaidi ya mwaka mmoja, pamoja na mazingira ya kifo anaona ni sahihi mshtakiwa kuachiwa kwa masharti kwa mujibu wa kifungu cha 38 cha Kanuni ya Adhabu.