Meatu. Wananchi wa Kata ya Sakasaka, Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wameeleza hofu na masikitiko yao kufuatia uvamizi wa tembo kutoka Pori la Akiba la Maswa ambao wamekuwa wakihatarisha maisha ya watu, kuharibu mali na kusababisha vifo.
Wakizungumza leo Oktoba 5, 2025 na Mwananchi Digital baadhi ya wakazi wa Kata hiyo wamesema tatizo hilo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu na sasa limesababisha familia kadhaa kuamua kuhama makazi yao kutokana na hofu ya kushambuliwa.
Samson Mathias mkazi wa kijiji cha Sakasaka amesema kuwa tembo hao wamekuwa wakivuka mipaka ya pori hilo na kuvamia makazi ya watu, kuharibu mali, kusababisha vifo na majeruhi.
“Changamoto ya tembo ni kubwa, wanavunja nyumba, wanaharibu mashamba na hata kuua watu. Baadhi ya wananchi wamehama kutokana na hofu hii.
Tunaiomba Serikali ichukue hatua za haraka,” amesema.
Ramadhani Said ameeleza kuwa uvamizi wa tembo hao umekuwa ukiwasumbua zaidi nyakati za usiku.
“Hatupati usingizi. Tembo wanapovamia wanabomoa nyumba, wanakula mazao na tunalazimika kujaribu kuwakimbiza wenyewe ili kupunguza madhara, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yetu,” amesema.
Naye Mathias Nghumbu amependekeza kuwekwa uzio maalumu ili kuzuia tembo kuingia kwenye makazi ya watu. Pia ameshauri kufugwa nyuki pembezoni mwa pori la akiba, mbinu ambayo imetumika maeneo mbalimbali duniani kuwazuia tembo kutokana na hofu yao kwa nyuki.
Mgombea udiwani wa Kata ya Sakasaka kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Emanuel Maliganya, akizungumza katika uzinduzi wa kampeni zake katika kijiji cha Sakasaka amesema kuwa changamoto ya tembo ni moja ya mambo yanayomnyima usingizi kutokana na madhara makubwa yaliyosababisha vifo vya wananchi wanne ndani ya kipindi cha miaka mitano.
“Ni kweli tembo wametusumbua sana. Katika kipindi cha miaka mitano tumepoteza maisha ya watu wanne. Nikipewa ridhaa ya kuwa diwani wa kata hii kwa kipindi cha pili cha miaka mitano tutaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha tatizo hili linapatiwa suluhisho la kudumu.
“Tayari vituo vya askari wanyamapori vimeanza kujengwa na vijana wamepewa mafunzo maalum ya kudhibiti tembo,” amesema.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) wamesema tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kudhibiti tatizo hilo, ikiwemo kuongeza askari na vifaa vya kufuatilia mienendo ya tembo wanaotoka porini.
Akizungumza na Mwananchi digital kwa njia ya Simiyu, Omary Khalid kwa niaba ya Mkuu wa pori la akiba la Maswa amesema kuwa kwa sasa wamepanga kuongeza doria na kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori, pamoja na wananchi wa vijiji jirani vilivyopo karibu na pori hilo.
“Tunatambua changamoto inayowakabili wananchi wa Sakasaka na maeneo jirani. Tayari tumepanga kuongeza doria na kuimarisha ushirikiano kati ya askari wanyamapori na vijiji vilivyo jirani na Pori la Maswa. Pia tunahamasisha matumizi ya mbinu rafiki za kuzuia tembo kama vile ufugaji wa nyuki na mashamba ya pilipili,” amesema.