Ile siku Othman Masoud Othman, alipoteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ilikuwa heshima ya hali ya juu, maana alikuwa anaziba nafasi iliyoachwa wazi na mwanasiasa mahiri na mkongwe, Seif Sharif Hamad.
Heshima hiyohiyo, kwa upande wa pili ni mateso makubwa.
Othman au OMO, ndiye mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).
OMO anakuwa mwanasiasa wa pili wa upinzani kuwa na nguvu kwenye uchaguzi Zanzibar, tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa, uliporejeshwa Julai mosi, 1992.
Uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, na kila uchaguzi mkuu baada yake Zanzibar, mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa na nguvu kubwa alikuwa na Seif.
Februari 17, 2021, Seif alipokea wito wa mauti akiwa Makamu wa Kwanza wa Raia wa Zanzibar.
OMO akapendekezwa na ACT-Wazalendo kumrithi. Na sasa, kuelekea uchaguzi mkuu 2025, ACT-Wazalendo wameweka matumaini yao kwa OMO.
Wasifu wa OMO unaanza na imani kuwa, chama chake kiliona anaweza kuvaa viatu vya Seif, japo ni vikubwa kiasi gani, lakini pengine chama chake kilifikiria kuwa akiweza kujaladia soksi kadhaa, basi ataweza kuvaa na kutembea.
Inawezekana pia imani yao ni kwamba, OMO ni bora sana, lakini hakuwahi kupata nafasi kama ya Seif.
Hapa niweke mkazo, kitendo cha kufikiriwa kuwa unaweza kushika nafasi iliyoachwa wazi na Seif ni kuaminika kwa hali ya juu. Seif, gwiji kabisa wa siasa za Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alijenga jina lake kwa miaka mingi na Wazanzibari wengi walimtazama kama mtetezi wao katika njia za kistaarabu.
Upande wa pili, kila uchaguzi mkuu, Seif alikaribia kugawa kura nusu kwa nusu. Mara nyingi, yeye na watu wake walitangaza kushinda uchaguzi, lakini walidhulumiwa matokeo.
OMO anaposimama kama turufu kuu ya upinzania Zanzibar, licha ya kwamba anawania urais kwa sifa zake, bado anatazamwa kama nguvu yake ya ushawishi, itaweza kuitikisa CCM.
Ndani ya miaka minne, OMO akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, amekuwa akijitahidi kwa kila namna kujiondoa kwenye kivuli cha Seif. Amejitahidi kufanya kama yeye badala ya kumuiga Seif. Wakati huohuo, hajawahi kukerwa wala kuogopa pale watu wanapomlinganisha na Seif.
Februari 7, 1963, kwenye Kijiji cha Pandani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar, ndiko OMO alizaliwa.
Elimu ya msingi alisoma Shule ya Pandani, Wete, kisha alifaulu kuendelea na elimu ya sekondari, Shule ya Fidel Castro, iliyopo Chakechake, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Pemba.
OMO ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kisha alisoma shahada ya uzamili ya sheria, Chuo Kikuu cha London, Uingereza.
Shahada hiyo ya uzamili, OMO alijikita zaidi kwenye sheria ya biashara na kampuni. OMO ana shahada nyingine ya sheria aliyofuzu Chuo Kikuu cha Turin, Italia.
Shahada ya sheria ambayo OMO aliisomea Chuo Kikuu cha Turin, ilihusu Sheria ya Ubunifu (intellectual property).
OMO pia, amepitia mafunzo mbalimbali ya uongozi na mambo mengine hasa eneo la sheria.
Hivyo, kwa utambuzi, ni sahihi kumwita OMO mwanasheria mbobezi.
Mwaka 1989, mara tu alipomaliza shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, OMO aliajiriwa kama mwanasheria wa Serikali, Zanzibar.
Mwaka 1993, OMO aliporejea Tanzania baada ya kuhitimu shahada ya uzamili London, aliteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, aliyekuwa akishughulikia sheria.
Mwaka 1996, OMO aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Kiongozi.
Wakati huohuo aliendelea kubaki na cheo chake cha Naibu Mwanasheria Mkuu, kisha aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Utawala Bora.
Kipindi hicho, aliendelea pia kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar.
OMO alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Utawala Bora mpaka mwaka 2000, alipoteuliwa kuanzisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar.
Mchakato huo wa kuanzisha ofisini ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Zanzibar ulichukua miaka miwili.
Mwaka 2002, baada ya ofisi ya DPP kukamilika Zanzibar, OMO aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka wa kwanza Zanzibar. Nafasi hiyo aliishikilia kwa miaka tisa. 2002 – 2011.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Zanzibar ilipata Rais mpya, Dk Ali Mohamed Shein.
Mwaka 2011, Dk Shein alimteua OMO kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar. Mwaka 2014, OMO aliondolewa nafasi ya Mwanasheria Mkuu baada ya kukinzana na msimamo wa Serikali kuhusu suala la Muungano.
OMO ni mume wa Zainab Shaib Kombo na ana watoto wanane.
Ahadi ya OMO kwa Wazanzibari ni kuwa akishinda urais, jambo la kwanza ni kuimarisha demokrasia, atahakikisha anakomesha mtindo wa viongozi kuchaguliwa katika njia zisizo halali.
OMO anasema kuwa, Wazanzibari wanapaswa kumwamini na kumchagua awe Rais wa visiwa hivyo na atautumia urais wake kuirejesha Zanzibar kwenye mikono ya Wazanzibari.
Anaongeza kwamba, utaratibu wa kupiga kura utawekwa na uchaguzi utakuwa huru na haki.
OMO anasema kipaumbele chake cha kwanza kwa Wazanzibari ni Katiba mpya, itakayowezesha Zanzibar kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Anasema, kila kitu, kuanzia Katiba mpya hadi Tume Huru ya Uchaguzi, waamuzi watakuwa Wazanzibari wenyewe.
Ndani ya miaka minne akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, amekuwa sauti ya kupiga vita rushwa na ufisadi Zanzibar.
Ahadi yake kwa miaka mitano ijayo kama atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni kukuza uchumi wa nchi na kudhibiti matumizi holela ili kuijenga Zanzibar bora itakayompendeza kila Mzanzibari.