Hatua kuu kesi ya uhaini ya Lissu, kuanza kusikilizwa leo

Dar es Salaam. Ile siku ambayo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alikuwa akiisubiri ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri katika kesi yake ya uhaini inayomkabili, imefika.

Siku hiyo ni leo, Jumatatu, Oktoba 6, 2025, ambapo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam itaanza usikilizwaji kamili wa kesi hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani iliyopelekwa kwa pande zote, kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia leo, Oktoba 6, 2025, hadi Oktoba 24, 2025.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha maneno yafuatayo:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025, na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, alikofikishwa kwa ajili ya maandalizi ya awali, ikiwemo kukamilisha upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji kamili.

Kabla ya upelelezi kukamilika, kila kesi hiyo ilipokuwa ikiitwa kwa tarehe zilizopangwa, Lissu alikuwa akiulalamikia upande wa mashtaka kwa ucheleweshaji wa upelelezi huo, akitaka upande wa mashtaka ukamilishe haraka upelelezi wake ili kesi hiyo ipelekwe Mahakama Kuu haraka ianze kusikilizwa.

Baada ya taratibu zote kukamilika, sasa kesi hiyo itaanza kusikilizwa leo mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Hii ni sehemu ya kwanza ya usikilizwaji wa kesi hiyo, ambayo pia ndio mwanzo wa kuelekea mwisho wa kesi hiyo.

Katika sehemu hii ya kwanza ya usikilizwaji wa kesi, mahakama itapokea ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri ambao watatoa ushahidi wakiongozwa na waendesha mashtaka. Watakuwa wakiwauliza maswali ya kuwaongoza kueleza wanachokijua kuhusiana na kesi hiyo.

Kisha, mshtakiwa Lissu ambaye anajiwakilisha mwenyewe, atakuwa na nafasi ya kuwauliza mashahidi hao maswali ya dodoso yanayolenga kutikisa uimara wa ushahidi wao na kuonesha matobo yanayoibua mashaka ambayo yanaweza kumnufaisha.

Katika kesi hiyo, Jamhuri imebainisha kuwa itakuwa na mashahidi 30 na vielelezo tisa. Mashahidi hao ni maofisa wa polisi na raia ambao mahakama hiyo ilitoa amri ya kuwalinda kutokana na maombi ya Jamhuri.

Ulinzi huo unahusu kutotajwa majina yao wala taarifa zozote zinazoweza kuwafanya watambulike wao, familia zao au watu wa karibu yao, kutokuonekana wakati wakitoa ushahidi wao na kutumia majina bandia.

Kisheria, hakuna idadi maalumu inayohitajika ili kuthibitisha kesi. Hivyo, licha ya kutajwa idadi hiyo, hailazimiki kuwaita mashahidi wote, bali inaweza kuwaita baadhi yao tu na pale itakaporidhika na ushahidi wao kuwa umeweza kuthibitisha shtaka, itafunga kesi kwa upande wake.

Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake, mawakili wanaweza kuomba kuwasilisha hoja za kuishawishi mahakama kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Hata hivyo, hilo ni utashi wa mahakama ambayo ina uhuru wa kutoa nafasi hiyo au la.

Kama itatoa nafasi hiyo au haitatoa, hatimaye mahakama itatoa uamuzi iwapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, uamuzi ambao ndio utakaoamua kama kesi hiyo itaendelea katika sehemu ya pili au itaishia hapo.

Kama itamuona mshtakiwa kuwa hana kesi ya kujibu, itaamuru aachiliwe huru na kesi hiyo itaishia hapo.

Iwapo mahakama itaridhika kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu, kesi hiyo itaingia katika sehemu ya pili ya usikilizwaji, ambayo ni utetezi wa mshtakiwa, ambapo atawasilisha utetezi wake na kuita mashahidi wake pamoja na kuwasilisha vielelezo kama atakuwa navyo.

Kisha atasubiri tarehe ya hukumu ambapo mahakama itaamua kama ana hatia au la.

Katika kesi nyingine za jinai, Jamhuri huwa na wajibu wa kuthibitisha kama mshtakiwa ndiye aliyetenda kosa analoshtakiwa nalo, lakini katika kesi hiyo ya Lissu mambo ni tofauti.

Septemba 22, 2025, wakati wa usikilizwaji wa awali, Lissu aliposomewa shtaka, kwanza alikiri kutamka maneno hayo yaliyonukuliwa kwenye hati ya mashtaka yanayodaiwa kuwa yanaunda kosa la uhaini, lakini akasema kuwa maneno hayo hayaoneshi kosa lolote la uhaini.

Kisha alisomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo na kubainisha mambo anayokubaliana nayo na asiyokubaliana nayo.

Katika maelezo hayo, alikubali majina yake kamili, makazi yake, wadhifa wake ndani ya Chadema kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, huku akiongeza kuwa ni wakili wa Mahakama Kuu na pia mwanasheria.

Mengine ni shtaka linalomkabili kuwa anashtakiwa kwa kosa la uhaini, kuwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumiliki hati ya kusafiria (passport) iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji.

Vilevile, alikubali kuwa alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 841KJ Mafinga mwaka 1989 na kumalizia kikosi cha 844KJ Itende, kilichopo Mbeya.

Hata hivyo, aling’aka kuwa kuhudhuria mafunzo hayo kusichukuliwe kama yeye ni mwanajeshi, huku akidai kuwa anajua ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusiana na hoja hiyo.

Maelezo mengine aliyokubaliana nayo ni kukamatwa Aprili 9, 2025, wilayani Mbinga, na kurejeshwa Dar es Salaam, kisha kupelekwa mahakamani siku iliyofuata, ambako alifunguliwa shtaka la uhaini.

Hivyo, ushahidi wa upande wa mashtaka utajikita zaidi katika hoja zinazobishaniwa.

Hatua ya Lissu kukiri kutamka maneno yanayodaiwa kutengeneza kosa la uhaini ni kama vile ameirahisishia Jamhuri kazi, kwani inaweza isilazimike kutumia nguvu kuleta mashahidi wengi kuthibitisha kuwa ndiye aliyetamka maneno hayo.

Badala yake, nguvu kubwa itakuwa ni kuthibitisha kuwa maneno hayo yanatengeneza kosa la uhaini, jambo ambalo ni hoja za kisheria zaidi kuliko kiushahidi, na kwa kiasi kikubwa ni jukumu la waendesha mashtaka kuishawishi mahakama kuwa kisheria maneno hayo yametengeneza kosa la uhaini.