Polisi Watoa Onyo Kuhusu Matumizi Mabaya ya Mitandao ya Kijamii – Global Publishers

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa on warning kali dhidi ya kile lilichokiita matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa kusambaza maudhui yenye viashiria vya uhalifu na uchochezi, kufuatia kuenea kwa video inayomuonesha mtu anayejitambulisha kwa jina la “Kapteni Tesha”, anayesema kuwa ni afisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime, video hiyo ina maneno yanayoweza kuathiri usalama wa Taifa na amani ya nchi, na uchunguzi umeanza mara moja kubaini watu wote waliohusika katika utayarishaji na usambazaji wake.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayejihusisha na utengenezaji au usambazaji wa taarifa zenye mwelekeo wa uchochezi, upotoshaji au uvunjifu wa amani kupitia mitandao ya kijamii. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa bila upendeleo,” alisema SACP Misime.

Ameongeza kuwa Tanzania ni nchi yenye utawala wa sheria, hivyo yeyote mwenye malalamiko au maoni kuhusu masuala ya kijamii au kisiasa anatakiwa kuyawasilisha kwa njia halali badala ya kutumia mitandao kuhamasisha chuki au vurugu.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya mitandaoni. Tunawahimiza wananchi kutumia mitandao kwa ajili ya maendeleo, si kwa kuvuruga amani,” alisisitiza Misime.

Video hiyo, ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye majukwaa kadhaa ya mitandao ya kijamii tangu Oktoba 4, 2025, inadaiwa kuwa na kauli za kuhamasisha jeshi kuingilia masuala ya kisiasa, jambo lililokanushwa vikali na JWTZ siku iliyofuata, likisisitiza kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa uaminifu, utii na uhodari.