Dk Dau: Hii ndiyo Udart tuitakayo

Ilikuwa siku ya Alhamisi Oktoba 2, 2025 wakati natoka kuswali swala ya Alasiri katika msikiti wa Mjimwema, Kigamboni, nilipigiwa simu na mmoja kati ya watu wangu wa karibu kuniarifu kuwa nimeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (Udart). Mara tu baada ya simu hiyo, nilianza kupokea salaam za pongezi na za pole kwa simu na ujumbe was WhatsApp kutoka kwa watu mbalimbali mmoja mmoja na kutoka makundi sogozi mbalimbali. 

Kwa hakika malalamiko yalikuwa mengi. Si nia yangu kuyaorodhesha hapa kwani kwa kufanya hivyo itakuwa sawa na kukosha nguo zako chafu hadharani. Lakini kwa ujumla wake, mengi yalikuwa kwenye maeneo ya huduma mbaya kwa wateja, hujuma kama vile mabasi kwenda matupu na kuwaacha abiria vituoni kwa kisingizio kuwa muda wa kazi wa dereva umemalizika, abiria kutorudishiwa “chenji” zao wakati wa kulipa nauli, ubadhirifu wa mali na mengine mengi. 

Baada ya utangulizi huo, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa tunijaalia afya njema. Pili, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteuwa Mwenyekiti wa kampni ya Udart haswa ikizingatiwa changamoto zilizojitokeza hivi karibuni. Hii ni dhamana kubwa kutokana na unyeti wa Mkoa wa Dar es Salaam.  Mimi na wenzangu kwenye Bodi na Menejimenti tutafanya kila liwezekanalo ambalo lipo ndani ya uwezo wa kibinadamu kutimiza wajibu wetu kwani Kanuni ya Fiqh inatuelekeza kuwa “lisilowekezakana lote, lisiachwe lote”.

Nikiri kuwa hii si mara ya kwanza kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tofauti na teuzi zote nilizopita, kwenye uteuzi huu nimepata salaam nyingi sana. Pamoja na pongezi, wengi wao wamenipa pole. Yupo ndugu yangu mmoja ambaye ni sahib wangu wa miaka mingi aliniambia kuwa hatonipa pongezi mpaka aone mabadiliko makubwa kwenye usafiri Dar es Salaam. Alikuwa sahihi kabisa. Nawashukuru wote kwa salaam zenu.

Kufuatia changamoto zilizopo kwenye Udart, niliamua nifanye ziara ya kimya kimya kwa kupanda basi kama abiria wa kawaida ili niweze kusoma na kuielewa vyema Udart. Nafahamu kuwa ziara ya siku moja haitoshi kuielewa vyema Taasisi yoyote lakini nilidhani ziara hiyo itanipa utambulisho (introduction) mzuri wa Udart. Sharti ambalo mimi mwenyewe nilijiwekea ni kuwa katika ziara hiyo, nisingependa watu wanitambue kwani nilitaka niyashuhudie mambo katika uhalisia wake.    

Kabla kufanya ziara hiyo, nilitaka ushauri kutoka kwa watu mbalimbali huku nikiwaeleza sharti langu. Katika kuficha kujulikana (identity) kwangu, nilifikiria nivae mavazi ya kawaida lakini nivae kofia ambayo maarufu inajulikana kama kapelo.  Baada ya kuwaeleza dhamira yangu, mmoja kati ya dada zangu (jina ninalihifadhi) ambaye ana wadhifa mkubwa Serikalini alinishauri kuwa kama kweli nataka nisijulikane ni vyema nikavaa buibui na ikiwezekana nifunike uso wote isipokuwa macho tu. Uvaaji huu maarufu unajulikana kama “ninja”. Dada yangu alinishauri kuwa kinyume cha hivyo watu watanifahamu na dhamira yangu haitotimia.

Baada ya kupokea ushauri huo, nikajadiliana na mke wangu kwa sababu mbili. Kwanza, mimi sina buibui. Hivyo basi, itabidi niombe la kwake na haswa kwa vile vimo vyetu havipishani sana. Pili, ni vyema jambo kubwa kama hilo la kubadili mavazi ningepata ushauri na ridhaa yake. Wazo hilo likaonekana si zuri kwa sababu kwanza hairuhusiwi kuvaa “ninja” kwenye mwendokasi lakini pili endapo atatokea mtu akanitambua, itakuwa fedheha kubwa kwangu. Kwa maana hiyo, niliamua kuvaa nguo za kawaida na kofia ya kapelo. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana wakati naondoka nyumbani nilisahau kofia yangu.

Nilianza ziara Jumapili Oktoba 5, 2025, saa 5:50 asubuhi katika kituo cha Posta ya zamani kwenda Kimara ambapo tulifika saa 6 dakika 20. Nilikaa Kimara kiasi cha dakika 15 na kuondoka saa 6:35 na kufika Posta ya zamani saa 7:10. Wakati wa kwenda sikubahatika kupata kiti. Nilisimama kutoka Posta ya zamani hadi Kimara. Kwa bahati wakati wa kurudi nilipata kiti kutoka Kimara hadi mwisho wa safari yangu.

Kwenye safari yangu yote (kwenda na kurudi) nilipata bahati mbaya ya kupanda mabasi mapya yenye rangi ya kijani iliyokolea. Nasema ilikuwa bahati mbaya si kwa sababu ya rangi ya mabasi au sababu nyingine yoyote isipokuwa nilitamani kupanda mabasi ya zamani ya rangi ya buluu ili niweze kufanya tathmini ya hali ya mabasi hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kuwa ni mabovu. Natumai Balozi Hamza atanielewa.

Katika ziara hii nimejifunza mengi sana. Mengi ya malalamiko niliyoambiwa nimeyashuhudia. Hata hivyo, hapa si mahala pake. Ni mambo ambayo tutajadiliana kwenye vikao vya Bodi na Menejimenti ili tuweze kupata ufumbuzi wa matatizo hayo. Tutajitahidi kuwajuza wananchi jitihada ambazo zinafanywa kuondoa kero hizo.

Kwa bahati nzuri, ile dhamira yangu ya kutotambuliwa ilitimia isipokuwa wakati wa kurudi. Tulipofika Manzese, kuna kijana mmoja alinikaribia na kunitazama kwa muda mrefu kidogo. Baada ya macho yetu kukutana aliniamkia, nami nikaitikia. Kwa sababu nilikuwa nimekaa, haraka nikatoa simu yangu na kuanza ku-“chat” ili kukwepa asianze kunisemesha na kuwafanya watu wengine wanitambue.

Kwa kumalizia, naomba niwakumbushe Wakurugenzi wenzangu na Menejimenti kuwa dhamana tuliyopewa ni kubwa na matarajio ya wananchi ni makubwa. Nina imani tukifanyakazi kwa juhudi, maarifa ikiwemo ubunifu na kuweka uzalendo mbele, tutatoa mchango mkubwa kwa nchi yetu.

Kwa wafanyakazi wa Udart, naomba mkae mguu sawa. Kazi ya kujenga Udart mpya imeanza!

Mwandishi ni Balozi na Mwenyekiti wa Bodi ya Udart.