Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Kibamba kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki ameainisha vipaumbele 10 atakavyotekeleza kwa wakazi wa kata za Saranga na Goba endapo atachaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akihutubia wakazi wa maeneo hayo kwa nyakati tofauti, leo Oktoba 6, 2025, Kairuki amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya Serikali ya CCM, bado zipo changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka.
“Nikipewa nafasi ya kuwa mbunge wenu, nitaanza kwa kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari katika kata hizi mbili zinajengewa uzio ili kulinda usalama wa watoto,” amesema Kairuki.
Kuhusu usafiri, amesema atahakikisha njia mpya za daladala zinaanzishwa katika Kata ya Goba na maeneo mengine, kutokana na changamoto kubwa ya usafiri inayowakabili wananchi.
Kipaumbele kingine, amesema ni kuhakikisha eneo la makaburi linapatikana kwa ajili ya matumizi ya jamii.
“Kama itahitajika kulipa fidia tutafanya hivyo ili tuwe na eneo rasmi la kuzikia, maana suala la makaburi ni muhimu sana kwa jamii yetu,” amesema.
Kuhusu sekta ya afya, Kairuki amesema Serikali ya CCM tayari imewekeza zaidi ya Sh400 milioni katika ujenzi wa jengo la ghorofa mbili katika Kituo cha Afya cha Kimara huku Sh100 milioni zikiwa zimepangwa kununua vifaatiba.

Ameongeza kuwa Kituo cha Afya cha Saranga kimetengewa Sh100 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na kazi hiyo itaharakishwa ili huduma zianze mapema mwezi ujao.
Katika sekta ya elimu, Kairuki amesema zaidi ya Sh35.8 milioni zimeelekezwa kwenye ujenzi wa madarasa mapya, majiko ya shule na huduma ya chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa maeneo ya shule na kusema kutakuwa na utaratibu wa kulipa fidia ili kupata ardhi mpya, jambo litakalosaidia wanafunzi kuepuka kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Kuhusu miundombinu ya barabara, amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh1.8 bilioni katika miradi mbalimbali ya barabara ndani ya kata hizo.
Ameahidi kuwa akichaguliwa, ataweka kipaumbele katika utekelezaji wa awamu ya pili ya ujenzi wa barabara zikiwemo Kimungu–Suka–Ukombozi, Peponi–KKT Temboni, na Suka–Foleni–Karanga–Upendo ili kuboresha barabara za changarawe na kuimarisha mtandao wa usafiri ndani ya jamii.
Vilevile, Kairuki ameahidi kusimamia miradi ya maji katika maeneo ya Goba, Saranga na Ukombozi ambako wananchi hupata maji kwa muda wa saa tano pekee kwa siku. Amesema atafuatilia utekelezaji wa miradi mingine muhimu katika maeneo ya Bangu, Pasaka na Ruvu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii.
Kuhusu vijana na wanawake, ameahidi kuviwezesha vikundi vya ujasiriamali, ikiwemo vikundi vya watu wenye ulemavu, kwa kuwapatia mafunzo ya biashara na kuwaunga mkono katika miradi midogo ya kiuchumi.
Aidha, ameahidi kufuatilia ujenzi wa madaraja na vivuko ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayokumbwa na mafuriko, hatua itakayowasaidia kufanya shughuli zao kwa usalama na ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mary Chatanda, alimsifu Kairuki akisema ni kiongozi makini na mwenye uwezo wa kusimamia maendeleo ya wananchi.
“CCM imewaletea Angellah Kairuki Kibamba kwa sababu ni mchapakazi, ana uwezo wa kujenga hoja na kufuatilia masuala ya wananchi. Ni mtu sahihi kwa maendeleo ya jimbo hili,” amesema Chatanda.
Ametoa wito kwa wananchi wa Kibamba kumchagua Dk Samia Suluhu Hassan kuwa Rais kwa mara nyingine, akisisitiza kuwa Serikali yake imeleta maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Saranga, Jeremiah Sanga amesema vipaumbele vyake vimejikita katika utekelezaji wa ilani ya CCM.
“Tukipewa ridhaa, nitashirikiana na mbunge kutatua changamoto za maji, miundombinu na ujenzi wa uzio katika shule zetu,” amesema Sanga.