Afrika yatikisa Kombe la Dunia U20

Timu tatu kati ya nne za Afrika zimefanikiwa kutinga hatua ya 16 ya Fainali za Kombe la Dunia la Vijana Chini ya Umri wa miaka 20 zinazoendelea nchini Chile.

Wakati Misri ikiwa ndio mwakilishi pekee wa Afrika ambaye ameaga mashindano hayo, Afrika Kusini, Morocco na Nigeria zimefanikiwa kutinga hatua hiyo ya mtoano.

Morocco imetinga hatua ya 16 bora kibabe kwa kuongoza kundi lake C licha ya kupoteza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mexico kwa bao 1-0.


Ushindi katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Brazil na Hispania uliifanya Morocco kuwa mwakilishi wa kwanza wa Afrika kusonga mbele.

Morocco sasa itakutana na Korea, Alhamisi Oktoba 9, 2025 kusaka tiketi ya robo fainali ambayo itakutana na mshindi baina ya Italia na Marekani.

Nigeria licha ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi F, imeingia hatua ya 16 bora kwa kubebwa na kigezo cha kuwa miongoni mwa timu zenye matokeo bora ambazo zimemaliza katika nafasi ya tatu.

Sare ya bao 1-1 dhidi ya Colombia katika mchezo wa mwisho imeipeleka mikononi mwa Argentina katika mechi ya mtoano itakayochezwa Jumatano, Oktoba 8, 2025 jijini Santiago.


Kocha wa Nigeria, Aliyu Zubairu amesema kuwa wapo tayari kucheza na Argentina.

“Kikubwa tulichohitaji ni kufika katika hatua inayofuata na sasa tupo tayari kukabiliana na yoyote,” amesema Zubairu.

Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Marekani usiku wa kuamkia leo umeifanya Afrika Kusini kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E.


Kwa kumaliza katika nafasi hiyo, Afrika Kusini itakutana Colombia, Jumatano, Oktoba 8, 2025 jijini Talca.

Kocha wa Afrika Kusini, Raymond Mdaka amesema kuwa wanataka kuhakikisha wanafika mbali zaidi katika mashindano hayo.