Dar es Salaam. Wakati Serikali ikilenga kutafuta uwekezaji wa Sh36.862 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026 maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bagamoyo, Kwala, Benjamin Mkapa yamepigiwa chapuo huku bidhaa za kipaumbele zikitajwa.
Uwekezaji huo unatafutwa wakati ambao robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha (Julai hadi Septemba 2025) tayari imerekodi miradi 201 yenye thamani ya Sh6.18 trilioni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri amesema wameendelea kushuhudia ongezeko la uwekezaji mpya katika mwaka 2025 licha ya kuwa ni kipindi cha uchaguzi.
Hiyo ikiwa na maana kuwa imani ya wawekezaji imeendelea kukua jambo ambalo ni kiashiria kikuu cha kuimarika kwa uchumi.
“Katika robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba tumerekodi miradi 201 yenye thamani ya Sh6.18 trilioni ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 20,808. Katika miradi hiyo viwanda iliongoza kwa kuwa na miradi 85, ujenzi wa majengo ya biashara 30, uchukuzi 29, utalii 24 na kilimo 13,” amesema.
Akiitaja mikoa iliyoongoza kwa kurekodi miradi mingi amesema Dar es Salaam iliongoza kwa kuwa na miradi 79 yenye thamani ya Sh2.03, Pwani ikiwa na miradi 29 yenye thamani Sh417.99 bilioni.
“Mikoa mingine ni Mwanza yenye Miradi 12 ikiwa na mtaji wa Sh482.97 bilioni, Dodoma ikiwa na miradi 13 ikiwa na mtaji Sh455.32 bilioni na Arusha ikipata miradi16 yenye mtaji wa Sh261.02 bilioni,” amesema Teri.
Amesema matokeo hayo yanaonyesha mwendelezo chanya wa kukua uwekezaji katika miradi mbalimbali nchi huku akiwaita Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo.
Amesema nchi za Jumuiya ya Umoja wa Falme za Kiarabu, China na India zikiwa kinara kwa kusaka fursa hizo za uwekezaji.
Ili kukuza uwekezaji zaidi na kufikia malengo yaliyowekwa katika mwaka huu wa fedha, Tiseza imekuja na kampeni ya kutangaza maeneo maalumu matano ya uwekezaji yaliyopewa kipaumbele.
Maeneo yaliyowekwa sokoni kwa kuanzia ni Bagamoyo, Kwala, eneo la Benjamin Mkapa, Buzwagi lililopo Kahama.
“Maeneo hayo yapo mengi mengine Ruvuma, Mirerani, Tanga nayo tumeyapa kipaumbele, akitokea mwekezaji ndani ya miezi 12 anaweza kuanzisha kiwanda na mamlaka utampa eneo bure,” amesema.
Katika maeneo hayo bidhaa 10 zimepewa kipaumbele ambazo wawekezaji wanaweza kuzalisha ikiwemo zile za matumizi ya haraka, bidhaa uzalishaji wa nguo, viwanda vya uzalishaji dawa, uunganishaji wa magari, utengenezaji magari na vipuri, karatasi na vifungashio, bidhaa za mpira na raba ikiwemo matairi.
Bidhaa nyingine zilizopewa kipaumbele ni uundaji injini za boti, pikipiki, utengenezaji sola, za umeme jua, betri, teknolojia nyingine vifaa vya umeme na samani za ujenzi.
“Sisi kama Tiseza tutaendelea kutoa taarifa kwa umma na kuendeleza maeneo ya kiuchumi mikoani kote. Pia niwaombe watu watumie takwimu sahihi kuhusu masuala ya uwekezaji kutoka Tiseza na si kutumia zinatolewa na taasisi zisizo rasmi,” amesema.
Akizungumzia suala hilo, Rashid Mzamili alitaka miradi hiyo ya uwekezaji kufanyiwa kazi ndani ya wakati, ili Watanzania wanufaike nayo ikiwemo upataji wa ajira au ongezeko la bidhaa sokoni.
“Hiyo itasaidia wao kuona umuhimu wa takwimu za ongezeko la uwekezaji zinazotolewa kila wakati kwani Watanzania wataona ni kitu kinachowagusa moja kwa moja.”
“Miradi hii ikitekelezwa kwa wakati wananchi watapata ajira, hii tatizo la ajira kelele zake zitapungua mitaani na kufanya wananchi wafurahie kile kinachofanyika,” amesema.