Dar es Salaam. Wakati kukiwepo na taarifa za madai ya kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema limeanza kufuatilia taarifa za madai hayo, huku likisisitiza kuwa bado linaendelea kumsubiri kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Awali, Jeshi la Polisi lilimtaka Polepole kufika ofisini kwa DCI ili kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, kumekuwepo taarifa kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa anayedaiwa ndugu wa Polepole akidai kuwa ametekwa.
Jeshi la Polisi katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumatatu, Oktoba 6, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, limesema kuwa Polepole alitumiwa wito wa kisheria kutakiwa kuripoti ofisini kwa DCI kwa ajili ya mahojiano, lakini hadi sasa hajatekeleza agizo hilo.
“Humphrey Polepole alitumiwa barua ya wito kwa mujibu wa sheria za nchi aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili atoe maelezo kuhusiana na tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii, lakini hadi leo hajatekeleza maelekezo hayo,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo imeeleza kuwa jeshi hilo linachunguza taarifa zinazosambaa mitandaoni kutoka kwa baadhi ya ndugu wa Polepole wanaodai ametekwa huku likisema kuwa, hatua za uchunguzi wa awali zinaendelea ili kubaini ukweli wa madai hayo. “Tumeanza kufanyia kazi taarifa hizo ili kupata ukweli wake,” limeeleza Jeshi la Polisi.