Hersi, Arafat waachiwa msala hatima ya Folz Yanga

PRESHA iliyopo ndani ya Yanga hivi sasa, inamfanya kocha mkuu wa kikosi hicho, Romain Folz kusikilizia hatima yake ndani ya timu hiyo. Hali hiyo imekuja kufuatia kundi kubwa la mashabiki hawajaridhika na kiwango cha timu hiyo licha ya kwamba haijapoteza mechi yoyote hadi sasa.

Inaripotiwa kwamba uongozi wa Yanga umeanza mchakato wa kimyakimya wa kumsaka Kocha Mkuu mpya jambo ambalo haliwezi kuwa habari nzuri upande wa Folz ambaye ana umri wa miaka 35.

Wakati Wanayanga na Kocha Folz mwenyewe wakikaa mkao wa kula kusubiria nini kitatokea juu ya Mfaransa huyo, kuna vichwa nane ambavyo ndio vimeshikilia uamuzi wa kuendelea au kutoendelea na kocha huyo ambaye alishawahi kuinoa Mamelodi Sundowns akiwa msaidizi.


Vichwa hivyo nane ndio vinaunda Kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo ambayo ndio chombo chenye mamlaka ya kuajiri au kuachana na makocha wa timu hiyo.

Vigogo hao nane wanaongozwa na Rais wa klabu hiyo, Mhandisi Hersi Said ambaye katika miaka ya hivi karibuni ameonyesha nguvu kubwa ya ushawishi katika masuala ya usajili wa wachezaji na ajira za makocha na maofisa wa benchi la ufundi.

Kichwa kingine ni Arafat Haji ambaye ni Makamu wa Rais wa Yanga aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

Ukiondoa vigogo hao wawili, kuna wengine sita ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, watano wakiwa wa kuteuliwa na mmoja akiwa wa kuteuliwa.


Wajumbe hao ni Gerald Kihinga, Seif Gulamali, Munir Seleman, Alex Ngai, Yanga Makaga na Rodgers Gumbo.

Folz ameiwezesha Yanga kutetea ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, Septemba 16, 2025.

Pia ameiongoza Yanga kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitupa nje Wiliete ya Angola kwa ushindi wa mabao 5-0 katika mechi mbili baina yao.