Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imemjibu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kuhusu madai yake aliyoyaibua kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi yake ya uhaini ikisema kuwa mambo aliyoyalalamikia yapo kwa mujibu wa sheria.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akituhumiwa kutamka maneno kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kesi hiyo ya inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndungiru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, imeanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri leo.
Hata hivyo kabla ya kuanza usikilizwaji huo Lissu ameibua madai ya baadhi ya watu wake aliotakiwa kuwaorodhesha kwa ajili ya kuingia mahakamani kusikiliza kesi hiyo, wamezuiliwa na kuna watu wengine wamepigwa.
Pia amehoji na kutaka mahakama impe ufafanuzi kuwa nani aliyeagiza kuwasilisha orodha ya watu wake 100 watakaopata nafasi kuhudhuria kesi hiyo, na mwenye mamlaka ya kuzuia watu mahakamani hapo kama ni Polisi au mahakama.
Vilevile amedai kuwa alipokea taarifa ya maandishi kutoka kwa Naibu Msajili wa mahakama hiyo ikimtaka kuhudhuria kikao cha awali kabla ya vikao vya usikilizwaji wa kesi hiyo (pre session meeting) saa mbili kabla, kwa njia ya mtandao, ambacho amedai kuwa hakuhudhuria kwa sababu hakupewa taarifa sahihi.
Hata hivyo amehoji kuwa utaratibu huo katika kesi za jinai umetoka wapi akidai kuwa haupo kwenye sheria za Tanzania.
Lissu pia amedai kuwa hati ya wito aliyopelekewa inaonesha kuwa kesi hiyo itasikilizwa kuanzia leo Oktoba 6 mpaka 24, 2025 na kwamba hati hiyo ya wito iliambatanishwa na ratiba ya vikao ya usikilizwaji wa kesi hiyo (cause list).
Amefafanua kuwa ratiba hiyo inayoonesha kuwa baada ya Oktoba 24 kutakuwa na mapumziko ya siku 10 kisha itaendelea kuanzia Novemba 3 mpaka 12, 2025 na kwamba Novemba 12 itakuwa siku ya hukumu.
Hivyo amehoji kuwa inawezekanaje kesi ambayo ina mashahidi 30 wa Jamhuri na 15 wa upande wake imeshapangiwa tarehe ya hukumu kabla hata haijaanza kusikilizwa.
Kutokana na sababu hiyo amehoji iwapo tayari mahakama imeshaandika hukumu yake kabla ya kusikiliza kesi na akaomba kama hivyo basi asomewe tu hukumu hiyo, badala ya kupoteza muda.
Akitoa ufafanuzi wa madai hayo, Jaji Ndunguru amesema kuwa usikilizwaji wa kesi za jinai huongozwa na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (Criminal Procedure Act – CPA).
Kuhusu tarehe ya hukumu kupangwa kabla kesi haijaanza kusikilizwa Jaji Ndunguru amesema hilo limefanyika chini ya kifungu cha 185(1) na (2) cha CPA.
Amefafanua kuwa kifungu hicho ambacho kinaeleza utaratibu kwa mashauri ya jinai ambayo Mahakama Kuu ina mamlaka ya asili ya kusikiliza shauri kwa mara ya kwanza lisilo rufaa au mapitio.
Amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu hicho Jaji Mkuu ana mamlaka ya kutoa mwongozo utakaoratibu uendesheaji wa mashauri hayo na kwa mujibu wa miongozo iliyotolewa na Jaji Mkuu, mashauri yanaendeshwa kwa muda wa siku 30, ambazo zinajumuisha na hukumu.
Hata hivyo amesema kuwa kuna mwongozo mwingine wa Jaji Mkuu ambao unahusu kuongeza muda baada ya siku hizo 30, lakini akasema kuna mashauri mengine yanaendeshwa chini ya muda huo wa siku 30.
“Hiyo ratiba iliandikwa kwa kufuata utaratibu huo”, amesema Jaji Ndunguru.
Kuhusu kikao cha awali kabla ya kuanza kesi hiyo, Jaji Ndunguru amesema ni utaratibu wa kawaida ambao unalenga kukutanisha pande zote ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.
Jaji Ndunguru amesema kuwa hata hivyo kuwepo au kutokuwepo kwa kikao hicho hakuwezi kuathiri upande wowote katika kesi husika.
Kuhusu watu kuzuiwa amesema kuwa mahakama ilishatoa utaratibu wa uhudhuriaji wa kesi hiyo, watu hawazuiwi lakini wanapaswa kufuata utaratibu uliowekwa.
Hata hivyo kutokana na madai hayo ya Lissu, Jaji Ndunguru amesema
kuwa wamemwelekeza Msajili kufuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuhakiki majina ya watu walioorodheshwa kwenye orodha hiyo, waliotajwa na mshtakiwa Lissu, wanaopaswa kuruhusiwa kuingia mahakamani kufuatilia kesi hiyo.
Baada ya ufafanuzi huo, sasa mahakama hiyo inaendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo ambapo shahidi wa kwanza wa Jamhuri amesimama kutoa ushahidi wake.
Katika kesi hiyo Lissu anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha maneno yafuatayo:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alikofikishwa kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, kwa ajili ya usikilizwaji kamili.
Baada ya upelelezi kukamilika kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu Agosti 18, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji kamili.