Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeomba Rais atakayechaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kuwapa nafasi za kutosha wanawake katika uteuzi.
“Tunatamani kuona wanawake wengi zaidi kwenye nafasi za maamuzi, ni wajibu wetu kama wanasheria kuendelea kuishauri Serikali na vyama vya siasa kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi sawa,” amesema makamu wa rais wa chama hicho, Leticia Ntagazwa.
Akizungumza katika jukwaa la wanasheria wanawake lililofanyika Oktoba 4, 2025 makao makuu ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), jijini hapa, Ntagazwa amesema historia ya Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa kwa wanawake walioteuliwa kushika nyadhifa nyeti serikalini.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani aliwaamini wanawake, akitolea mfano wizara nyeti ya ulinzi na wizara ya mambo ya nje ambako aliwateua wanawake kuongoza.
“Katika Mahakama ya Rufani mwaka 2000 haikuwa na jaji mwanamke, mwaka huu kati ya majaji 40, 13 ni wanawake, vilevile kwenye Mahakama Kuu, kati ya majaji 105, 40 ni wanawake.
“Haya ni mafanikio makubwa yanayoonyesha kuwa wanawake wamekuwa wakiaminika zaidi kushika nyadhifa za juu katika mihimili ya dola.
“Ombi letu mawakili wanawake, Rais atakayechaguliwa katika vyama 16 vinavyogombea kuhakikisha anawapa nafasi wanawake kwenye nafasi za uteuzi, hususan nafasi za ujaji, ukatibu mkuu, wakurugenzi, makatibu na nafasi nyingine za uteuzi,” amesema.
Jukwaa hilo pia lilijadili nafasi ya mwanamke katika uongozi, uchaguzi na utawala wa kisheria kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Ntagazwa amesema kwa mujibu wa Sheria ya Tanganyika kifungu cha nne mawakili wana jukumu la kulinda haki za wananchi, kutetea masuala ya kijamii na kuhakikisha misingi ya utawala wa kisheria inalindwa.
Amesema ni wajibu wa wanasheria wanawake kuangazia nafasi ya mwanamke katika uongozi, uchaguzi na utawala wa kisheria kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu na masuala mengine yanayowahusu wanawake nchini.
“Tunapojadili nafasi ya mwanamke, tunapaswa kuangalia zaidi kile tunachoweza kufanya kama wanasheria wanawake ili kusaidia jamii kuelekea uchaguzi mkuu.
“Wajibu wetu ni kulinda haki za Watanzania na kuwakumbusha wajibu wao kwa mujibu wa Katiba na sheria,” amesema akigusia
Sheria ya Tanganyika kifungu cha nne, kinachosema mawakili wana jukumu la kulinda haki za wananchi, kutetea masuala ya kijamii na kuhakikisha misingi ya utawala wa kisheria inalindwa.
Jukwaa hilo pia lilijadili mwamko wa wanawake kugombea nafasi za juu za uongozi, hususan urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambao wanawake watatu wameaminiwa na vyao vya kuwa wagombea wa nafasi ya urais, ikiwa ni idadi kubwa kutokea nchini kulinganisha na chaguzi zilizopita.
Amesema katika uchaguzi wa 2005 kwa mara ya kwanza, alijitokeza mgombea mwanamke (Anna Senkoro) aliyewania nafasi hiyo.
“Miaka 10 baadae kwenye uchaguzi wa 2015 akajitokeza Anna Mghwira (sasa ni marehemu), mwaka 2020 wanawake wawili waligombea nafasi hiyo na mwaka huu tumeshuhudia wanawake watatu wakipambana kusaka kura baada ya kupitishwa na vyama vyao na Tume Huru ya Uchaguzi,” amesema kiongozi huyo.
Ntagazwa amesema hiyo ni hatua kubwa kwa wanawake na ni dalili kwamba wanaaminiwa na wanaendelea kupata nafasi kwenye siasa za kitaifa.
Akimwakilisha mgeni rasmi Rais, Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliwakumbusha washiriki wa jukwaa hilo umuhimu wa kuendelea kufasili dhana ya mafanikio na demokrasia na kuangalia namna wanawake wanavyoweza kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi na katika utawala wa sheria.
Amesema tangu kuanzishwa kwa TLS mwaka 1954, ni mawakili wawili pekee wanawake wamewahi kuwa marais wa chama hicho, akibainisha ni wajibu wa sasa kuhakikisha wanawake wanasheria wanakuwa sehemu ya uongozi wa juu kuanzia ndani ya TLS yenyewe.
“Wanawake hawapaswi kuwa waoga kushiriki katika mapinduzi ya kijamii na kisiasa. Ni jukumu letu kuondoa vikwazo vyote vinavyowanyima nafasi,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Jukwaa hilo limeandaliwa si kwa ajili ya wanasheria wanawake pekee, lilihusisha pia wanawake kutoka kada mbalimbali likilenga kujadili kwa pamoja masuala yanayomhusu mwanamke, ikiwamo mafanikio katika uongozi, ustawi wa kijamii na changamoto zinazowakabili.