Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema bado kuna kazi ya kuendelea kujenga barabara kuu na za ndani kufungua zaidi uchumi wa Pemba.
Dk Mwinyi amesema licha ya Pemba kufunguliwa, lakini inahitaji kuendelea kufunguliwa zaidi wananchi.
Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 6, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa kuomba kura kwa makundi mbalimbali katika uwanja wa Msuka Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Kwa sasa Pemba tumeshaifungua, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya, tutaendelea kujenga barabara kuu na za ndani ili ifunguke zaidi maana tunataka tukitoka madarakani tuache alama kubwa,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amewaeleza wananchi hao kwamba iwapo wakiendelea kuwaamini watafanya makubwa zaidi: “tumejenga hospitali za wilaya lakini tunatambua bado kuna uhitaji wa vituo vya afya vidogovidogo.”
Katika upande wa miundombinu, amesema tayari wameanza kujenga bandari na viwanja vya ndege hayo yote ni katika kuleta mageuzi makubwa katika kisiwa hicho.
“Tutaendelea kuwawezesha makundi ya kijamii, tulifanikiwa kupandisha pensheni ya jamii kutoka Sh20,000 hadi Sh50,000 kwa hiyo tukipewa fursa tena hatutashindwa kupandisha zaidi ya hapo,” amesema.
Amewaahidi wanawake wakulima wa mwani kwamba wataangalia ombi lao la kusamehewa mikopo ya boti walizopewa ili kukuza uchumi wao.
Amerejea kauli yake ya mpango mkakati alionao wa kushusha bei za vyakula ikiwa ni pamoja na kujenga bandari ambapo meli zitakuwa zinashusha bidhaa zake katika kisiwa hicho, badala ya Pemba na kujenga maghala ya kuhifadhia chakula kwa mwaka mzima.
Awali, akimkaribisha Dk Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Dk Mohamed Said Dimwa amesema wanakwenda kifua mbele kwa wananchi kuomba ridhaa tena kutokana na mambo makubwa ya maendeleo yaliyofanywa chini ya uongozi wa Dk Mwinyi kwa kipindi cha miaka mitano.
“Kuna mafanikio mengi yamefanyika, sasa hayo iwe sababu tosha ya kukichagua Chama cha Mapinduzi tofauti na wengine wanakuja kwenu kuwaeleza maneno matupu,” amesema Dk Dimwa.
Mgombea wa ubunge wa Msuka kwa tiketi ya NCCR Mageuzi, alikuwa miongoni mwa watu waliopata fursa kuzungumza katika mkutano huo, amesema licha ya uanamageuzi wake lakini anatambua kazi iliyofanywa na CCM.
Amesema kupitia uanaharakati wa maendeleo amepigia kelele bandari ya Msuka ilipopatwa na dhoruba lakini Serikali ilitekeleza.
“Nitaendelea kuwa mwanamageuzi, ila sio kwamba niwe kipofu nisione kilichofanyika, binafsi sio mpinzani wa maendeleo,” amesema.
Mkazi wa Msuka, Omar Ali Mwinyi amesema licha ya kujengwa barabara kutoka Konde hadi bandari ya Msuka lakini bandari hiyo ina hali mbaya, hivyo wanaomba kujengewa ya kisasa kama maeneo mengine.
“Hii ndio bandari yetu ambayo kwa muda wote tunategemea, lakini ina hali mbaya, tunahitaji tujengewe soko la kisasa katika bandari hii ambayo inawafanya biashara zaidi ya 1,500,” amesema Omar.
Katibu msaidizi wa umoja wa waendesha bodaboda Mkoa wa Kaskazini Pemba, Kassim Issa Juma amesema kupitia sekta hiyo vijana wengi wamejiajiri baada ya kurasimishwa, ambapo hatua hiyo imefanyika katika utawala wa Dk Mwinyi.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Msuka, Abdallah Ali Rashid ameomba kujengewa barabara katika maeneo yao ili kuondoa changamoto ya usafiri.
Pia, amesema wakati wa mvua wanafunzi wanapata changamoto kuvuka kwenda eneo lingine, hivyo wanaomba kujengewa shule na kukarabati kituo cha afya.
“Tunaomba utujengee sekondari, na kutuwekea madawati kwenye shule ya msingi,” amesema.
Kwa niaba ya wajane, Moza Juma Said amesema kuna changamoto ya vijana wazururaji na kusababisha wizi, hivyo kuomba wajengewe chuo cha amali kuokoa vijana hao wasiendelee kuharibikiwa.
Pia, amesema akina mama walipewa boti ndogo za mwani lakini wanaomba wasamehewe mikopo hiyo ili waweze kujiendeleza na kumudu uendeshaji, ombi ambalo Dk Mwinyi amesema ataangalia.