:::::::::::
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Licha ya Tanzania kuwa katika kipindi cha uchaguzi, hamasa ya wawekezaji kuwekeza nchini imeendelea kuimarika, hatua inayoonesha imani kubwa waliyonayo kwa uongozi wa serikali ya awamu ya sita.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TIC), Gilead Teri, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa uwekezaji katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Teri alisema kuwa hali hiyo inaashiria mazingira mazuri ya kisiasa na kiuchumi nchini, na kwamba wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wanaendelea kuonesha nia ya dhati ya kuwekeza, jambo ambalo si la kawaida katika mataifa mengi yanayokabiliwa na uchaguzi.
“Pamoja na kwamba nchi yetu ipo kwenye uchaguzi, kasi ya uwekezaji haijapungua hata kidogo. Hii inaonyesha imani kubwa ya wawekezaji kwa Mheshimiwa Rais na serikali kwa ujumla kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu,” alisema Teri.
Alibainisha kuwa Tanzania imejijengea sifa ya kuwa nchi salama kwa uwekezaji, hata katika vipindi ambavyo kwa kawaida huwa na changamoto kwa baadhi ya mataifa mengine.
Aidha, aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu badala ya kuwaachia wageni pekee kunufaika nazo.
“Watanzania tusiwe watazamaji, tuchangamkie fursa hizi. Uwekezaji si kwa wageni tu, ni kwa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Teri, TIC inaendelea kufungua milango ya uwekezaji na kutoa huduma rafiki kwa wawekezaji ili kuhakikisha mazingira bora ya kufanya biashara yanaendelea kuimarika nchini kote.