Pemba. Nyota ya Maalim Seif Sharif Hamad, imeendelea kuwa turufu ya kisiasa kwa Chama cha ACT Wazalendo visiwani Pemba, baada ya chama hicho kueleza kupata uungwaji mkono kutoka kwa wananchi katika mikutano ya kampeni za mgombea wake wa urais, Othman Masoud Othman.
Ni nyota ya Maalim Seif (marehemu), kwa sababu ndiye mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa na ushawishi zaidi visiwani humo, hasa kutokana na harakati zake, uzalendo na misimamo yake ya kuweka mbele masilahi ya Wazanzibari badala yake binafsi.
Maalim Seif aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, kadhalika Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, kabla ya kufariki Februari 17, 2021, ni kama aliitengenezea njia ACT Wazalendo, baada ya kutoka CUF, kiasi kwamba wananchi wanakiona kivuli chake.
Hilo limethibitishwa hata na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa aliyesema uungwaji mkono wote unaoshuhudiwa kwa chama hicho visiwani Pemba, ni matokeo ya juhudi za Maalim Seif enzi za uhai wake.

Jussa ameeleza hayo leo Jumatatu Oktoba 6, 2025 wakati uzinduzi timu ya ushindi ya chama hicho, kwa upande wa Pemba uliohudhuriwa na mgombea urais wa Zanzibar (ACT Wazalendo), Othman Masoud Othman. Miongoni mwa majukumu ya timu hiyo ni kupita nyumba kwa nyumba kusaka kura za ushindi wa chama hicho.
Katika maelezo yake, Jussa amesema siku sita za mikutano ya hadhara ya Othman katika majimbo mbalimbali ya Pemba, wananchi wa kisiwa hicho wameonyesha mwitikio mkubwa kwa chama hicho, amefanisha hali na uwepo wa kivuli cha Maalim Seif.
“Katika hili tujisifu, nilikuwa namwambia ndugu yangu Mansour (Yusuph Himid-Mjumbe wa Kamati Kuu), si kazi ya Othman Masoud, wala si kazi ya Jussa, sote ni kama vile tumekaa kwenye baiskeli tupo kilimani halafu tunateremka zamani tulikuwa tunasema ‘free’.”
“Tunasafiria free ya kazi ya Maalim Seif au nasema uongo jamani? Akajibiwa kweli… Maalim Seif alipita kijiji kwa kijiji, kujenga mtandao Mungu amlaze mahali pema peponi. Huwezi kupambana na mbegu iliyopandwa na Maalim Seif, Pemba haihitaji kufundishwa siasa, bali ni chuo cha siasa,” amesema Jussa.
Katika hatua nyingine, Jussa ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Ushindi wa ACT Wazalendo Zanzibar, amesema timu za ushindi kwa upande wa Pemba zimeanza kazi za kuhakikisha ushindi wa chama hicho, tangu miezi mitatu iliyopita.
Jussa ameitaka timu hiyo kuhakikisha wote wanakuwa na lugha moja ya ushindi wa chama hicho, ifikapo Oktoba 29,2025.
Akizindua timu hizo, Othman amewashukuru viongozi wa ACT Wazalendo Pemba kwa maandalizi mbalimbali ya ziara ya mikutano yake ya kampeni ya kusaka kura iliyofanyika kwa siku sita akisema imekuwa na mafanikio.
“Huu mzunguko wa awamu hii, umekuwa muhimu sana Pemba, kwa sababu umekuwa na tija, umeongeza, ari hamasa na mafuta ya safari yetu. Mmefanya kazi nzuri viongozi mmetuheshimisha, tunajisikia faraja kwamba tuna taasisi imara,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo (Zanzibar), Omar Ali Shehe amesema msingi wa ushindi wa chama hicho unaanzia na ushindi wa chama katika ngazi ya kijiji.

“Tukishinda katika ngazi ya kijiji na mitaa yote, maana yake majimbo yote tumeyachukua, pia kura za urais zitakuwa zipo juu katika ngazi ya mkoa hadi Taifa,” amesema Shehe.
Shehe amesema kila kijiji na mitaa yote ya Pemba, ACT Wazalendo kina muundo mzuri wa kiuongozi, hatua itakayorahisisha chama hicho kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwisho mwa mwezi huu.