Dar es Salaam, Oktoba 2025.
AIRTEL Tanzania imeungana na mataifa katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2025, chini ya kaulimbiu “Mission Possible” (Dhamira Inawezekana).
Kaulimbiu hii inaendana kwa karibu na falsafa ya Airtel ya “Mteja Kwanza”, ambayo imeendelea kuwa mwongozo katika kila hatua na uamuzi wa kampuni hiyo, ikilenga kuboresha huduma na kuongeza thamani kwa wateja wake kote nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Bw. Charles Kamoto, amesema kuwa maadhimisho ya wiki hii yanalenga kutambua, kushukuru na kuthibitisha tena dhamira ya kampuni katika kuhakikisha huduma bora, zenye ubunifu na zinazoweka mteja katika kiini cha shughuli zake zote.
“Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu ‘Mission Possible’. Kwa upande wa Airtel, hii inamaanisha ‘Mteja Kwanza’. Tunaitazama wiki hii kwa mtazamo mpana, siyo kama maadhimisho ya muda mfupi pekee, bali kama fursa ya kuimarisha utamaduni wetu wa kufanya kazi kwa kuzingatia kwamba mteja ndiye kipaumbele chetu cha kwanza. Wiki hii tutadhihirisha hilo kupitia vituo vyetu vyote vya huduma, idara za huduma kwa wateja na hata timu nzima ya uongozi,” amesema Bw. Kamoto.
Katika kipindi cha mwaka uliopita, Airtel Tanzania imeendelea kuwekeza katika ubunifu na huduma zinazomrahisishia mteja maisha ya kila siku. Huduma kama LUKU Token Retrieval zimewawezesha maelfu ya wateja kupata namba zao za LUKU kwa urahisi, na hivyo kuepuka kukatika kwa umeme. Vilevile, huduma za kujihudumia (self-care tools) zimewapa wateja uwezo wa kusimamia akaunti zao kwa uhuru na urahisi zaidi.
Aidha, Airtel Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na wateja wake ili kuelewa mahitaji yao yanayobadilika. Kupitia mrejesho wa moja kwa moja, kampuni imeboresha huduma zake na kuimarisha uhusiano wake na jamii. Jitihada hizi zimeenda sambamba na upanuzi wa mtandao wa vituo vya huduma nchini, hatua inayolenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi, mijini na vijijini, kwa huduma zenye ubora na ukaribu.
“Katika kipindi cha maadhimisho haya, tumeandaa shughuli mbalimbali za kuwashukuru wateja wetu kupitia maduka na majukwaa ya kidijitali, ikiwa ni ishara ya kutambua imani na uaminifu wao kwetu,” amekngeza Bw. Kamoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Bi. Adriana Lyamba, amebainisha kuwa kampuni imeboresha zaidi huduma zake za kujihudumia ili kuongeza urahisi, usalama na ufanisi kwa wateja.
“Miongoni mwa huduma hizo ni huduma ya self-reversal, inayomwezesha mteja kurejesha muamala uliofanyika kimakosa bila kulazimika kwenda kwa wakala au ofisini. Huduma hii inamwezesha mteja kurekebisha makosa mara moja na kupata udhibiti kamili wa akaunti yake ya Airtel Money,” amesema Bi. Lyamba.