Vodacom yajivunia huduma bunifu, jumuishi kwa wateja

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Vodacom Tanzania PLC inajivunia miaka 25 ya huduma ya mabadiliko, ikithibitisha tena dhamira yake ya kutoa huduma jumuishi, zenye uwezo na ubunifu kwa kila mteja hapa nchini.

Siku ya kwanza ya maadhimisho ya wiki hiyo, Vodacom imezindua duka jipya (Vodashop) la huduma jumuishi kwa wateja katika kituo kipya cha East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Duka hilo lina dawati  la huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu, likionyesha dhamira ya Vodacom ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma, heshima na ubunifu unaomlenga mteja.

“Wiki ya Huduma kwa Wateja ni muda wa kuungana na wateja wetu na kusherehekea mahusiano tuliyojenga kwa miaka yote. Tunapoadhimisha miaka 25 ya kuwaunganisha na kuwawezesha wateja wetu, tunajivunia kuimarisha ajenda yetu ya ujumuishi kupitia upanuzi wa huduma zetu na uzinduzi wa dawati lingine la huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC, Philip Besiimire,

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara na Masoko, Brigita Shirima, alisisitiza kuwa safari ya ujumuishi ya Vodacom inaonekana kupitia mipango inayolenga wateja wenye mahitaji maalumu pamoja na wale wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

“Kuanzia wakalimani wa lugha ya alama na msaada wa video kupitia WhatsApp kwa wateja viziwi, huduma za haraka kwa wateja wasioona ambao wamesajiliwa kwetu, hadi njia za kuingilia madukani kwa kutumia viti mwendo (wheelchair) na sasa madawati ya huduma yanayofikika kwa urahisi kwa wateja wenye mahitaji maalumu,” alisema Brigita.

Akifafanua shughuli zilizopangwa kwa wiki hii, Mkuu wa idara ya Huduma kwa Wateja na Huduma za Kidijitali Belinda Wera, alieleza kuwa “wiki hii tutawatambua na kuwasherehekea si tu wateja wetu bali pia washirika wetu katika mfumo wa M-Pesa pamoja na timu zinazofanya kazi usiku na mchana kuwahudumia wateja.

Tukitambua kuwa hatupo peke yetu, tutakuwa na shughuli za kurudisha kwa jamii kama njia ya kuwashukuru kwa msaada wao wa kudumu kila wakati.”

Alisema kwa Vodacom, huduma kwa wateja si jukumu la idara moja tu, bali ni utamaduni uliojengwa kwa miaka 25 ya ubunifu unaomlenga mteja. Kila mwingiliano, iwe kupitia huduma za kidijitali, washauri wanaotoa msaada au majukwaa kama VodaTube, unaangazia dhamira ya kampuni ya kuwawezesha wateja.