Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema kuwa hakuna lisilowezekana na kauli mbiu ya wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu kwao ni mkakati unaowezekana.
CRDB ilizindua wiki hiyo jana katika tawi la Dar Village jijini Dar es Salaam, ikiambatana na kaulimbiu ya kimataifa ya “Mission Possible” uzinduzi huo uliohudhuriwa na wateja, wafanyakazi, wadau wa sekta ya fedha, na waandishi wa habari.
Akiongoza uzinduzi huo Raballa
alisisitiza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inaakisi safari ya mafanikio ya miaka 30 ya benki hiyo, iliyojengwa juu ya uthubutu, ubunifu, na uhusiano wa karibu na wateja akiongeza kuwa hakuna lisilowezekana pale kunapokuwa na mkakati sahihi na dhamira ya pamoja.
“Tulipoanza safari yetu mwaka 1996, wengi walidhani hatutaweza kushindana na benki kubwa za kimataifa. Lakini leo, baada ya miaka 30, Benki ya CRDB ni benki kubwa zaidi nchini Tanzania na kinara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema Raballa.
Alitaja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyotokana na uthubutu wa Benki hiyo kuwa ni pamoja na upanuzi wa kimataifa kupitia kampuni tanzu za Burundi na Congo (DRC), uanzishwaji wa taasisi mpya kama CRDB Insurance na CRDB Bank Foundation, pamoja na ujumuishi wa huduma za kifedha unaowezesha Watanzania kupata huduma za kibenki kidijitali na kupitia mawakala.

Raballa alifafanua kuwa mageuzi ya kiteknolojia yamekuwa sehemu ya msingi wa mafanikio hayo. Hivi karibuni Benki hiyo imekamilisha mageuzi makubwa ya kihistoria kwa kuingiza mfumo mkuu mpya wenye viwango vya kimataifa wa Temenos Transact (T24), unaoiweka Benki ya CRDB katika kiwango sawa na benki kubwa duniani.
“Mfumo huu umeongeza kasi, usalama na ubunifu wa huduma zetu, ukiwezesha matumizi ya akili unde (AI) na kujihudumia kwa wateja Pia, umefungua fursa ya kupanua huduma zetu katika masoko mapya kama Dubai,” alisema.
Aliitumia fursa hiyo pia kuwaomba radhi wateja waliopata changamoto wakati wa kipindi cha mpito, akisisitiza kuwa huduma sasa zimerejea katika ubora wake na Benki inaendelea kuboresha mifumo kwa ustahimilivu na kujituma.
“Maboresho makubwa kama haya hayakosi changamoto. Tunawashukuru wateja wetu kwa uvumilivu wao na tunawaahidi huduma bora zaidi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo, alisema CRDB Bank inaamini kuwa huduma bora kwa wateja si jambo la msimu bali ni dhamira ya kila siku.
“Wiki hii ni fursa ya kuwasherehekea wateja wetu ambao wametupa imani na maoni yanayotuongoza kuboresha huduma kila siku. Pia ni wakati wa kuwapongeza wafanyakazi wetu wanaoishi falsafa ya huduma bora kwa weledi na ubunifu,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wateja, Hashim Lema aliyekuwa mgeni maalumu katika hafla hiyo alitoa pongezi kwa Benki ya CRDB kwa huduma zenye ubunifu, mageuzi ya kidijitali, na ushirikiano wa karibu na wateja wake.
“Benki ya CRDB ni alama ya mafanikio ya kizalendo. Huduma zake zimetusaidia wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima, wanafunzi na wastaafu kutimiza ndoto zetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya Mission Possible,” alisema mteja huyo.