Hatima ya Mpina kugombea urais kujulikana Oktoba 10

Dodoma. Hukumu ya mwanachama wa chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina ya kutaka arudishwe kuwa mgombea kiti cha urais, sasa itasomwa Ijumaa ya Oktoba 10, 2025 saa 8 mchana.

Katika shauri hilo ambalo linasikilizwa na jopo la majaji watatu, Fredrick Manyanda (kiongozi wa jopo),  Abdallah Gonzi na Sylvester Kainda, lilipangwa kuendelea leo Jumatatu Oktoba 6,2025 kwa ajili ya hoja za ufafanuzi kutoka kwa mawakili wa pande zote, lakini walipofika mahakamani kila mmoja alisema hana hoja na kuomba mahakama isonge mbele kutoa uamuzi.

Mpina kupitia mawakili wake, alifungua shauri la kikatiba akipinga kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, uliopangwa kufanyika Oktoba 29.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba  24027 limefunguliwa na Mpina na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo (mwombaji wa kwanza na wa pili mtawalia) dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wajibu maombi wa kwanza na wa pili mtawalia.

Leo, katika Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma, Jaji Manyanda amesema pande zote katika wapeleka maombi na wajibu maombi, zimepeleka nyaraka toshelezi kama zilivyoagiza na mahakama na hivyo akaomba muda ili waandae hukumu.

Jaji amesema watatumia muda wa siku tatu kusoma hoja kutoka pande zote wakati wanaandaa hukumu yao na kwamba kama litahitajika jambo la ufafanuzi watafanya hivyo kwa kuwaita mawakili, ili kulipata lakini wasipoitwa inabidi wasubiri hadi siku ya hukumu.

“Shauri hili lina uhimu wake na uharakati kwa sababu linagusa masilahi ya wengine, sasa nimesema kwa kuwa baadhi ya maombi tumepokea leo hasa kutoka kwa waleta maombi, tupeni muda tusome hoja zote ili tuje na hukumu mapema Ijumaa ya Oktoba 10, 2025 saa 8 mchana,” amesema Jaji Manyanda.

Kiongozi huyo wa jopo la majaji watatu, amesisitiza kuwa lazima hukumu itolewe mapema kwani kuna watu wanaguswa na hasa kipindi hiki cha uchaguzi ambao unaendelea nchi nzima.

Jaji amewaita wananchi ambao wangependa kusikiliza kesi hiyo waruhusiwe kuingia mahakamani ili kusudi wakasikilize wenyewe, na akasisitiza watu wasizuiwe kwenda mahakamani siku hiyo, mchana.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Mpina amesema katika mchakato huo anapeleka pongezi kwa waandishi wa habari ambao wamemsaidia kufikisha ujumbe kwa dunia kwani bila ya hao kesi ingekuwa gizani.

Wengine aliowapongeza ni viongozi wa ACT-Wazalendo, akisema wamemtia moyo na kuwapa nguvu mawakili wake ambao wameendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha sheria haipindishwi.

Hata hivyo, mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Kisesa, amesema angetamani hukumu ya mahakama itoke hata kesho ili kusudi afunguliwe na akawaambie Watanzania kwa nini anataka kuwa rais wa nchi.

“Wenzetu wanaendelea na kampeni, sisi tunaendelea na Mahakama, kusema kweli natamani sana kama ingependeza huku hii itoke hata kesho na waseme kuwa ninakwenda kugombea ili kusudi nikawaambie kwa nini nataka nafasi hiyo, uchache wa siku siyo hoja,” amesema Mpina.

Kwa upande wake, kiongozi wa chama hicho, Doroth Semu amesema bado wana imani kubwa na Mahakama kwamba itatenda haki na kuwarudisha wagombea wao ili wananchi wakatoe uamuzi wenyewe.

Semu amesema muda siyo kigezo kwao kwa kuwa hata sasa kuna watu wanaendelea kuomba kura za chama kupitia kwa wagombea wa ubunge na udiwani, hivyo anaamini kuwa endapo akirudishwa Mpina bado wanakwenda kufanya.

Mpina na ACT Wazalendo wanawakilishwa na mawakili watatu ambao ni John Seka, Edson Kilatu na Jasper Sabuni wakati upande wa Serikali unawakilishwa na mawakili wanne ambao ni Marck Murwambo, Vivian Method, Stanley Kalokola na Erick Rumisha.