Viongozi wa dini wataka vijana, wanawake kulinda amani

Mwanza. Viongozi wa dini mkoani Mwanza wamewataka vijana na wanawake kuhakikisha wanalinda amani kabla wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 wakisisitiza bila amani hakuna maendeleo yatakayopatikana.

Wakizungumza wakati wa mdahalo wa viongozi hao ulioratibiwa na Shirika la Ladies Joint Forum kuhusu umuhimu wa amani kabla na baada ya uchaguzi kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wanawake na vijana leo Jumatatu Oktoba 6, 2025 jijini Mwanza, viongozi hao wametahadharisha kuwa amani ndio msingi wa kila jambo kwenye nchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata)  Mkoa wa Mwanza, Ustadhi Twaha Bakari amesema amani ni msingi wa maisha na maendeleo ya taifa lolote, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha inalindwa kwa vitendo.

“Sisi tunawahusia kila siku na kuwaambia hakuna jambo muhimu kama amani. Sehemu ikikosekana amani hakuna kitu kitakachoendelea…amani ni sahani ya mambo yote mazuri,” amesema Ustadhi Bakari.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuhakikisha jamii inamjua Mungu na kutambua thamani ya amani, kwani wao husikilizwa na kuheshimika na watu wengi.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Ladies Joint Forum, Fransisca Mboya akizungumza wakati wa mdahalo wa viongozi wa dini kuhusu amani kabla na baada ya uchaguzi.



Mchungaji Jacob Mutashi, amesema kipindi cha kuelekea uchaguzi mara nyingi kimekuwa na changamoto nyingi, hivyo ni muhimu vijana wakawa na utulivu na kuepuka kushawishiwa kuvunja amani.

Ameongeza kuwa vijana ni kundi muhimu katika jamii na pia ndilo linalolengwa zaidi na watu wenye nia ya kuchochea vurugu.

“Hata Shetani anahitaji vijana kwa sababu wazee hawana nguvu ya kufanya mambo mbalimbali, ndiyo maana sisi tunasisitiza vijana wamjue Mungu zaidi na wawe walinzi wa amani,” amesema Dk Mutashi.

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Ilemela, James Wembe, aliyemuwakilisha Ofisa Uchaguzi wa Wilaya hiyo amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatambua umuhimu wa wadau katika kusambaza elimu kwa jamii, hususan wanawake na vijana.

“Tume inahitaji wadau ili kufikisha elimu kwa jamii. Kundi kubwa linalohusishwa mara nyingi ni wanawake na vijana. Wakipata elimu na taarifa sahihi, jamii nzima itakuwa salama,” amesema Wembe.

Amesema wanawake na vijana wamekuwa wahanga wakubwa wa vurugu za kisiasa, hivyo kuwapatia elimu sahihi kuhusu kulinda amani ni hatua muhimu katika kujenga taifa lenye utulivu.

“Takwimu zinaonyesha wanawake na vijana ndiyo wengi katika jamii na hata kwenye nyumba za ibada, wakielimishwa vizuri, maana yake jamii kubwa itapata taarifa sahihi na amani itaimarika.

“Amani tunaitamani kabla, tunaitamani ionekane siku ya uchaguzi na tunaitamani ionekane baada ya uchaguzi. Hatuna nchi nyingine…kwetu ni hapa hapa, tunapaswa kuilinda amani yetu,”amesisitiza.


Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Ladies Joint Forum, Fransisca Mboya amesema lengo la mdahalo huo ni kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamasisha amani hususani kipindi hiki kuelekea uchaguzi lakini pia kuunga mkono ajenda ya ushirikishwaji wa wanawake kwenye ulinzi, amani na usalama.

Katika hatua nyingine, zaidi ya vijana 100 wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamepewa elimu ya mpigakura na shirika hilo ili kushiriki uchaguzi mkuu kwa kuchagua diwani, mbunge na rais.