MSANII wa vichekesho nchini, Aman Nzala maarufu kama ‘Anko Nzala’ amesema japo ni shabiki wa Simba lialia, anafurahi kuonA video zake zinafuatiliwa hadi na watu wa upande wa pili akiwamo kipa Diarra Djigui na Rais wa Yanga, Hersi Said.
Nzala ameliambia Mwanaspoti kuwa, rais wa Heshima wa Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji na yule wa Yanga, Hersi sambamba na wachezaji wakubwa wa klabu hizo za Kariakoo akiwamo Jonathan Sowah na Diarra ni watu wanaoongoza kufuatilia video zake mtandaoni.
Alisema kila anapokutana na Hersi na Diarra wanamwambia wanafurahishwa na vichekesho vyake na vingine wanamuonyesha katika simu zao ambavyo wamevichukua mitandaoni.
“Hersi na Diarra wakiniona huwa wanacheka muda wote pia wananipa moyo kwamba kazi yangu ni nzuri na ya kibunifu napaswa kusonga mbele zaidi ili siku moja niwe mchekeshaji wa kimataifa,” alisema.

Alisema ingawa bilionea wa Klabu ya Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji hawakutani mara nyingi, lakini ana sapoti kubwa katika kazi zake.
“Nakumbuka tajiri Mo Dewji alivyoniposti katika mtandao wa kijamii (Instagram) iliniongezea thamani sana, kwani ana watu wengi wanaomfuatilia na kwa ratiba zake hadi akaona nilichokifanya hilo lilinipa nguvu na moyo wa kuendelea kusonga mbele,” alisema Anko Nzala na kuongeza:
“Ukiachilia mbali wachezaji wa Simba ambao asilimia kubwa ni washikaji zangu nakutana nao mara kwa mara pia Fei Toto, Kibwana Shomari na Denis Nkane wanapenda ninachokifanya.”

Alisema kabla ya mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah kujiunga na klabu hiyo alimuahidi kwamba ni lazima atajiunga na wana Msimbazi kwa ajili yake na hilo alilitimiza.
“Video ipo mtandaoni ambayo Sowah ananiambia atakuja Simba kwa ajili yangu, hilo limetimia na mimi namtakia kila heri aanze kucheka na nyavu, kwani ni mchezaji mzuri hilo lilionekana akiwa na Singida Black Stars ambako alifunga mabao 13,” alisema msanii huyo na kuongeza:
“Japokuwa siwezi kuzungumza sana Kingereza na Sowah hawezi Lugha ya Kiswahili, ila tunaelewana mara nyingi anachukua video zangu anakwenda kuzitafsiri kwa Kiingereza kisha ananipigia simu na kuanza kucheka.”