Dar es Salaam. Benki ya NCBA Tanzania Kaulimbiu ya huduma kwa wateja mwaka huu, (Mission Possible), inaweka msisitizo wa dhamira yao kuhakikisha huduma bora hazibaki kuwa ndoto bali zinakuwa matokeo halisi yanayoonekana kwa wateja wake.
Uzinduzi wa wiki hiyo umefanywa leo Oktoba 06, 2025 katika tawi lake la Kijitonyama jijini Dar es Salaam, ikiashiria mwanzo wa wiki maalumu ya kuthibitisha dhamira ya benki hiyo katika kutoa huduma bora, bunifu na zenye kipimo halisi cha mafanikio kupitia falsafa yake ya “Maisha ni Hesabu”.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Mission Possible,” inaweka msisitizo kwa dhamira ya NCBA ya kuhakikisha huduma bora hazibaki kuwa ndoto bali zinakuwa matokeo halisi yanayoonekana kwa wateja wake.
Ikiwa imejikita katika falsafa ya Maisha ni Hesabu, benki inaendelea kuhesabu kila matokeo muda unaookolewa, urahisi wa huduma, uwazi wa mawasiliano na kiwango cha kuridhika kwa wateja.
“Mission Possible” inatukumbusha kuwa ubora wa huduma haupaswi kuwa ahadi pekee bali ni matokeo yanayopimika,” alisema Alex Mziray, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Tanzania na kuongeza kuwa kupitia falsafa ya Maisha ni Hesabu, wanahesabu kila hatua wanayoipiga na ila mteja ni namba muhimu katika mafanikio yao.
Mziray amesema mfumo huu mpya wa Internet Banking ni sehemu ya mageuzi makubwa ya kidijitali yanayoendelea ndani ya NCBA, ukitoa fursa kwa wateja kusimamia akaunti zao, kufanya miamala, kulipa bili, na kupata huduma za kifedha kwa haraka na usalama zaidi.
“Kupitia mfumo huu wa Internet Banking, Mission Possible inapata maana halisi kwa sababu tunawapa wateja uwezo wa kufanya kila kitu kwa urahisi, popote walipo na muda wowote. Huduma bora sasa ni halisi na inayoonekana,” aliongeza Mziray.
“Kupitia Internet Banking, Maisha ni Hesabu inakuwa dhahiri tunahesabu urahisi, kasi, usalama na ufanisi katika kila huduma.”
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa (Corporate Banking), Gilbert Kamugisha, alisisitiza mchango wa Asset Finance katika kukuza biashara nchini.
“Wateja wetu wakubwa ndio nguvu ya uchumi wa Taifa. Wanahitaji benki inayoweza kutoa maamuzi ya kifedha kwa kasi na uwazi. Kupitia Asset Finance, tumewezesha kampuni kupanua shughuli zao, kuongeza ajira, na kuimarisha uchumi. Hizi ndizo namba tunazozihesabu kila siku matokeo halisi yanayobadilisha biashara.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wateja Binafsi (Retail Banking), Ninael Mndeme, alizungumza kwa namna huduma za NCBA zinavyogusa maisha ya watu wa kawaida akisema kila akaunti ina ndoto nyuma yake ya kununua gari, kulinda familia, au kulipia elimu ya watoto.
“Kazi yetu ni kuhakikisha ndoto hizo zinatimia kwa kutumia huduma bora, salama na rahisi kufikiwa. Hiyo ndiyo maana halisi ya Mission Possible na Maisha ni Hesabu ni ahadi tunayoitekeleza kwa matendo.”
Katika maadhimisho haya, NCBA pia imezindua kampeni ya kitaifa inayohamasisha wateja kutoa maoni yao kupitia vituo vya sauti za wateja (customer voice booths) vilivyowekwa katika matawi yote, ili kuboresha zaidi huduma zinazotolewa.
Wateja wanaweza pia kushiriki kupitia majukwaa ya kidijitali, ikiwemo mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya benki.