Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kuwa alimfungulia Lissu jalada la uchunguzi wa kosa la uhaini kwa kuwa aliitisha Serikali.
Shahidi huyo, Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu Dar es Salaam (DZCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Bagyemu, ametoa sababu hiyo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, leo Jumatatu, Oktoba 6, 2025.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi hiyo ya inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, imeanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri leo.
Katika ushahidi wake, akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, Bagyemu kwanza ameieleza mahakama kuwa katika shughuli zake kama ofisa wa Polisi amepitia mafunzo na kozi mbalimbali.
Amezitaja kozi na mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kuhusiana na Sheria mbalimbali zikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) na Sheria ya Ushahidi (TEA).
Kwa mujibu wa ushahidi wake,
Aprili 4, 2025 asubuhi, akiwa ofisini kwake, aliingia Mkaguzi John Kaaya anayefanya kazi katika dawati la Doria Polisi mtandao, akamwambia kuwa katika kazi zake aliona picha mjongeo (video ) kwenye mtandao wa Youtube ya Jambo TV.
Mkaguzi Kaaya alimweleza kuwa video hiyo ilikuwa na kichwa cha habari ” Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia, No reforms no Election na kwamba maudhui yake yalikuwa na ujinai.
Mkaguzi Kaaya alimuonesha video hiyo kupitia simu yake janja( Smartphone) ambapp alimsikia Lissu akitamka maneno mbalimbali yaliwemo yaliyoko kwenye hati ya mashtaka.
Maneno hayo yaliyoko kwenye hati ya mashtaka ambayo yanadaiwa kutengeneza kosa la uhaini yanasomeka kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Baada ya kuisikiliza video hiyo alimpendekeza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Michael, kufungua jalada la uchunguzi DCMZ/ CID/ PP.101/2025.
Lengo la uchunguzi huo lilikuwa kwanza kujua kama picha mjongeo hiyo ni halisi au zimetengenezwa na pili
kuwapata Jambo TV kuwathibitishia kama hiyo picha mjongeo walirekodi wao au wanaitambua.
Baada ya kufungua jalada hilo, aliteua timu ya wapelelezi na alimtaarifu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuhusiana na picha hiyo mjongeo.
DCI alimwambia aendelee na upelelezi, lakini niwe na wasiliana na Ramadhani Ng’anzi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai, Mtandaoni, Maadili kwa Umma, Utengamano na Ulinzi wa Taifa.
Aprili 6, 2025 aliwasilia na kiongozi wa jambo TV ambaye alimwambia kuwa hiyo video anaitambua lakini aliyerekodi na kurusha live ni kijana wake, ambaye kwa muda ule alikuwa Dodoma na vifaa vyote alivyorekodia alikuwa navyo huko.
Hivyo alimpa namba yake ya simu na yeye ACP Bagyemu alimjulisha Ng’anzi aliyekuwa Dodoma kuwa aliyekuwa kwenye tukio aliyerekodi picha mjongeo na kifaa kilichotumika kurekodi, yupo Dodoma kikazi na akamtajia namba yake ya simu na jina la kijana huyo.
Aprili 7, 2025 mchana alimpa maelekezo Kaaya kupakua picha mjongeo Disk kutoka kwenye mtandao wa Kijamii wa You Tube wa Jambo TV na kuiweka kwenye flash disk ili kuifanyia uchunguzi wa Sayansi Jinai, naye akafanya hivyo.
Pia siku hiyohiyo usiku Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Churo alifika ofisi akiwa na kadi ya kutunzia data (memorial card), maelezo ya shahidi huyo aliyerekodi picha hiyo, (anayetambiliwa kwa jina la P) na hati ya kukabidhia na kielelezo cha hicho.
“Baada ya kupata memory Card niligundua kuwa hiyo picha mjongeo ilikuwa ni picha halisi iliyopo kwenye kielelezo” amedai ACP Bagyemu.
Aprili 8, 2025, asubuhi alimuelekeza, Michael yafunguliwe majalada mawili tofauti, moja la uhaini na lingine la kuchapisha taarifa mtandaoni naye akafanya hivyo.
ACP Bagyemu amedai kuwa katika video hiyo Lissu alisema atahamasisha uasi na atazuia uchaguzi, atakinukisha sana sana na atakivuruga sana na kwamba kwa maneno hayo aliitisha Serikali kwa yale anayotaka kuyafanya.
Amedai kuwa uchaguzi mkuu upo kwa mujibu wa Katiba na sheria na msimamizi wa sheria hizo ni Serikali, na kwamba kuitishia Serikali ni kwenda kinyume na sheria hizo na hivyo kwenda kinyume na matakwa ya Serikali.
Amedai kuwa aliamua kufungua kesi hiyo chini ya kifungu 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kwa kuwa Lissu aliitishia Serikali ifanye yale aliyoyataka.
” Lissu alienda mbele zaidi kudhihirisha nia yake ya kuzivunja sheria zinazosimamiwa na Serikali kwa kutoa na kuchapisha mtandaoni taarifa ambazo ni kuhamasisha uasi. Kutoa taarifa mtandaoni za kukinukisha na ndivyo vilivyonisukuma kufungua kesi”, amedai ACP Bagyemu.

Hata hivyo, Lissu amepinga ushahidi wa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni akidai kuwa ushahidi huo hauhusiani na kesi hiyo bali nyingine iliyoko Mahakama ya Kisutu na hivyo haupaswi kupokea na mahakama imekubaliana na pingamizi lake hilo.
Shahidi huyo amedai kuwa Lissu katika kutimiza nia yake alichapisha taarifa hizo kwa kuwaita waandishi wa habari ambapo zilisambazwa kupitia na mitandao ya kijamii, ili kiwafikia watu wengi, ndani na nje ya Tanzania.
Baada ya shahidi huyo kumaliza ushahidi wake huo wa msingi kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Jumanne, Oktoba 7, 2025 kwa ajili ya shahidi huyo kuhojiwa na Lissu maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake huo, kabla ya kuendelea na mashahidi wengine.
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, alikofikishwa kwa ajili ya maandalizi ya awali na baada ya upelelezi kukamilika, Agosti 18, 2025 kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu, kwa ajili ya usikilizwaji kamili.