Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko la joto litokanalo na mabadiliko ya tabianchi, watafiti wamebaini uwepo wa miti katika mashamba ya mazao (kilimo mseto) ni ulinzi thabiti dhidi ya hatari za kiafya zinazotokana na joto kali.
Hayo yamebainishwa na watafiti ambao walikusanya ushahidi wa awali miongoni mwa wakulima mkoani Dodoma.
Mradi huu unatoa takwimu dhahiri kuhusu jinsi kilimo mseto (agroforestry) kinavyoweza kuboresha afya na mazingira ya kazi moja kwa moja kwa mamilioni ya wakulima ambao shughuli zao ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.
“Lengo letu ni kujua kama kulima mazao pamoja na miti, yaani kilimo mseto, kunaweza kuleta tofauti katika afya za wakulima kwa kubadilisha mazingira yao ya karibu kazini,” amesema Dk Faraja Chiwanga, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani na kiongozi wa mradi kutoka shirika la LEAD Foundation.
Matokeo ya utafiti huu yaliwasilishwa leo Ijumaa, Oktoba 3, 2025 wakati wa Jukwaa la KISHADE (KISHADE FORUM) lililofanyika wakati Mkutano wa 12 wa Afya wa Tanzania (Tanzania Health Summit) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkulima kutoka Kongwa, mkoani Dodoma Henry Mubi aliunga mkono matokeo ya utafiti huo akisema joto kali limekuwa likiwapunguzia muda wa kufanya kazi, na wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.
Kichwa kinauma mwili unachoka, kusikia kizunguzungu ni mazingira magumu sana ambayo tunakabiliana nayo.
“Kutokana na kufanya kazi kwa muda mfupi kipato nacho lazima kipungue, vilevile joto linapokua kali mazao yananyauka yanayostahimili kwa muda mrefu ni yale yaliyo kwenye kivuli,” amesema Muba.
Wakati zaidi ya asilimia 70 ya nguvukazi ya Taifa ikiwa imewekezwa katika mashamba ya kilimo, utafiti huu unajibu moja kwa moja swali muhimu: Je, miti inaweza kulinda afya ya wakulima vijijini?
Kwa miaka mingi, kumekuwepo na ushahidi wa kimazingira kutoka kwa wakulima wanaoshiriki katika programu ya Kisiki Hai ambayo imesaidia kurejesha zaidi ya miti milioni 30 katika kaya 260,000.
Ushahidi umeonesha kuwa miti hutoa faida kama kupunguza joto kali. Utafiti huu sasa unafanya majaribio kupima nadharia hiyo kwa kutumia njia za kisayansi.
“Wakulima nchini mwetu wanakabiliwa na tishio linaloongezeka la magonjwa yanayohusiana na joto, ikiwa ni pamoja na hali ya upungufu wa maji mwilini, ugonjwa sugu wa figo, shinikizo la juu moyo na mishipa,” amesema Dk Chiwanga.
“Hatari hizi zimeongezeka kutokana na ukosefu wa kivuli na miundombinu yakupunguza joto kali katika mazingira kilimo, na kufanya joto kali kuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa binadamu na uzalishaji wa kiuchumi,” ameongeza.
Utafiti huu wa KISHADE unasaidia kutambua athari chanya ya miti katika kupunguza hatari za kiafya na kuweka mikakati ya kivitendo, inayozingatia ushahidi ya kudhibiti joto kali katika jamii za wakulima.
Ili kujua jinsi miti inavyosaidia, wanasayansi katika utafiti huu walizungumza na wakulima na kuwatazama wakifanya kazi ili kuelewa changamoto zao za kila siku.
Wakati huohuo, walitumia vitambuzi vinavyovaliwa (wearable sensors) kupima joto la mwili na mapigo ya moyo ya wakulima kwa wakati halisi.
Watafiti pia walichukua sampuli za mkojo na damu ili kuangalia matatizo yoyote ya kiafya yanayosababishwa na joto.
Kwa kulinganisha data kutoka kwa wakulima wanaofanya kazi karibu na miti na wale ambao hawafanyi hivyo, na kwa kutumia vitambuzi vya hali ya juu kupima hali ya hewa ya eneo husika, utafiti umeweza kuthibitisha hasa jinsi miti inavyolinda afya ya wakulima.
Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Anthropolojia kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mratibu wa mradi wa KISHADE, Dk Richard Sambaiga amesisitiza umuhimu wa kuhusisha jamii katika utafiti huu ili waonyeshe mwitikio.
Amesema kuwa mradi wa KISHADE tayari unaonyesha matokeo ya chanya, huku timu ya utafiti ikipokea uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa jamii za mitaa na bodi ya ushauri, jambo ambalo limefanya iwe rahisi kuwahusisha wakulima katika kupatikana kwa data za uhakika.
“Wakulima pia wameitikia vyema kwa kutumia teknolojia inayovaliwa ambayo inafuatilia viwango vyao vya joto, ikionyesha kuwa wanashiriki kikamilifu na wako tayari kushiriki. Ruhusa zote za kimaadili zinazohitajika zilipatikana vizuri, kuruhusu mradi kuendelea bila kuchelewa,” amesema Dk Sambaiga.
Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa, kupanuka zaidi ya mipaka ya Tanzania. Wanufaika si tu jamii ya wakulima na wakulima wa ndani, bali pia watunga sera, mamlaka za Serikali, na watoa huduma za afya ambao watapewa miongozo inayozingatia ushahidi katika utendaji wao wakati wakisaidia walioathiriwa na joto kali.
Dkt. Ivan Ivanov, mtaalamu wa Afya ya Kazini na Mahali pa Kazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Ivan Ivanov amebainisha umuhimu wa kimataifa wa utafiti huo.
Amesema kitaalamu inashauriwa kuacha miti mashambani, ukifanya kazi katika shamba lisilo na miti ni hatari zaidi kuliko shamba lenye miti, “Kwenye shamba lenye miti wanatumia muda mrefu zaidi na wanapata kipato kingi zaidi kuliko lile lisilo na miti.”
Utafiti huu, unaojulikana kama KISHADE, umefanywa na shirika la LEAD Foundation na washirika wengine kama London School of Hygiene and Tropical Medicine, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), na Meta Meta.