Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge ameongoza jopo la wataalamu wa moyo kutoka Tanzania, kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwa cha Anjouan nchini Comoro.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo leo kisiwani Anjouan, Dk Kisenge amesema dhamira ya JKCI ni kuhakikisha wananchi wa Anjouan wanapata huduma bora za moyo kwa gharama nafuu na kwa wakati bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu hayo.
Dk Kisenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba Taifa na daktari bingwa wa moyo, amesema kwa siku ya kwanza ambayo ni leo Oktoba 6,2025 wameanza kambi hiyo, huku mwitikio wa wananchi ukiwa ni mkubwa.
“Siku ya kwanza ya leo tumeona wagonjwa 99, watoto wakiwa 39 na watu wazima 60 wagonjwa waliopewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI ni 20. Asilimia 80 ya wagonjwa tuliowaona wana matatizo ya misuli ya moyo kutanuka.”

“Tumekuja na timu kamili ya madaktari bingwa na wataalamu wa vipimo vya moyo. Tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Comoro kuboresha huduma za moyo kwa wananchi, hasa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa,” amesema Dk Kisenge.
Ameongeza kuwa kambi hiyo ya madaktari bingwa kutoka Tanzania itafanyika kwa muda wa siku nane, huku ikihusisha uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwamo ya moyo, pamoja na utoaji wa elimu ya kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Dk Kisenge amesema taasisi hiyo inawapokea wagonjwa wengi kutoka Visiwa vya Comoro ambapo kwa mwezi wanawaona wagonjwa zaidi 40.
Kuwepo kwa wataalamu hao kisiwani Anjouan kutawasaidia wananchi wenye uwezo mdogo kiuchumi kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo bila gharama yoyote ile.
Akizungumza na wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo kupata huduma za matibabu ya moyo, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu, amewapongeza kwa hatua waliyoichukua ya kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu ya moyo.
“Wagonjwa ni wengi kuna madaktari wengine wako njiani wanakuja kutoka Tanzania, nyie nyote mliopo hapa mtapata huduma na tutahakikisha wagonjwa wote wanapata huduma ya matibabu na dawa bila malipo yoyote yale,” amesema Balozi Yakubu.

Baadhi ya wananchi waliopata huduma za matibabu ya moyo katika Hospitali ya Hombo walielezea kufurahia uwepo wa wataalamu wa JKCI, huku wakisema wamepata matibabu na ushauri wa kitaalamu waliokuwa wakiukosa kwa muda mrefu.
“Huduma zimekuwa bora sana. Tulipokelewa vizuri na madaktari wametupima kwa umakini. Tunashukuru Serikali ya Tanzania na madaktari wa JKCI kwa moyo wa huruma waliotuonyesha,” amesema Fatima Bounou mkazi wa Domoni.
“Siku zote tulikuwa tukitafuta huduma ya moyo ya kitaalamu karibu nasi, lakini ilikuwa ngumu kupata, kutokana na ushirikiano uliopo baina ya Comoro na Tanzania tumepata matibabu bora bila gharama yoyote. Tunashukuru sana madaktari kwa kujitolea kwa moyo wote,” amesema Ahmed Ali mkazi wa Mutsamudu.
“Huduma hizi ni za kipekee. Tulipokelewa kwa heshima na madaktari walitupa muda wao kuzungumza nasi moja kwa moja kuhusu afya yetu ya moyo. Ni faraja kubwa kuona Tanzania kupitia JKCI inatufikishia matibabu haya hapa nyumbani,” amesema Amina Said mkazi wa Ouani.
Kambi hiyo inatarajiwa kuwafikia maelfu ya wananchi wa Anjouan huku JKCI ikiahidi kuendelea kutoa mafunzo ya pamoja kwa wataalamu wa afya wa Comoro, ili kuimarisha huduma endelevu za moyo.