Dar es Salaam. Huduma mpya ya tiba ya urejeshaji (Regenerative Medicine) inayohusisha matumizi ya seli shina za mwili wa binadamu, huenda ikawa mbadala kwa wanaohitaji upasuaji wa kurekebisha maumbile maarufu ‘plastic surgery.’
Tiba hiyo yenye umuhimu katika sekta ya afya na urembo, inayopatikana kuanzia Dola 200 (Sh 490,654) hadi 300 za Marekani (Sh735,981) kwa kila kikao, huku matibabu kamili yafikia Dola 10,000 za Marekani (24,532,719)kutegemea na hali ya mgonjwa, husaidia mwili kujitibu kwa kutumia seli zake asilia bila upasuaji.
Kupitia tiba hiyo, wagonjwa wanaweza kurejesha ngozi iliyochoka, kuota nywele upya, kupunguza mikunjo, uzito, kasi ya kuzeeka (anti-aging), kujenga misuli, kuponya vidonda na hata kupunguza maumivu katika viungo vilivyoathirika ikiwamo ogani za mwili.
Daktari wa masuala ya urembo, Arshni Malde anasema tiba hiyo imeanza kuvutia watu wengi kutokana na matokeo yake ya haraka na gharama nafuu ikilinganishwa na upasuaji wa plastiki.
Katika mahojiano na Mwananchi, Dk Arshni ameeleza namna tiba hiyo inavyofanyika na matokeo kwa mgonjwa ikilinganishwa na tiba za awali za upasuaji.
Anasema tofauti na upasuaji wa plastiki ambao huhitaji muda mrefu kupona wakati mwingine madhara, tiba ya urejeshaji haina majeraha na inahusisha muda mfupi wa kupona, hutoa matokeo ya kudumu kwa sababu inachochea mwili kuunda upya ‘collagen’, mishipa na tishu zilizoharibika.

Dk Arshni anayefanya kazi jijini Nairobi Kenya, anasema kwa sasa wanapanua ujuzi zaidi katika tiba za urejeshaji na tiba za utendaji.
Anasema tiba za urejeshaji duniani zimeendelea sana kiasi kwamba watu sasa wanaweza kurejesha viungo kama ini, figo hata kukuza meno mapya.
“Kwa mfano, katika urejeshaji wa meno, madaktari hutumia fizi (gums) kukuza meno mapya, ingawa teknolojia hiyo bado haijaendelea sana nchini Kenya, lakini huduma za urejeshaji na seli shina (stem cells) zinapatikana katika mataifa mengine duniani,” anasema Dk Arshni ambaye pia ni Mkurugenzi wa kliniki za TIA na Regenera Pharma.
Anasema kwa sasa wamekuwa wakifanya urejeshaji wa ngozi na nywele kwa wanaume na wanawake.
“Kwa mtu anayetatizwa na upungufu wa nywele, tunatumia seli shina kutoka kwenye mwili wake. Seli hizo hutolewa kwenye damu ya mgonjwa kama vile kuchukua sampuli ya damu, kisha huzichakata na kuzirudisha kwa njia ya sindano kwenye ngozi ya kichwa, jambo linalochochea ukuaji wa nywele mpya.
“Hata hivyo, ikiwa mtu hana kabisa nywele kwa maana amepoteza zote kichwani, tiba ya seli shina haiwezi kufanya kazi vizuri, na hapo hupendekezwa upandikizaji wa nywele. Kwa jumla, urejeshaji unahusiana moja kwa moja na matumizi ya seli shina,” anafafanua.
Vivyo hivyo, Dk Arshni anasema kwa uso na ngozi, tiba hiyo hutumika kupunguza mikunjo, kufanya ngozi iwe na mwonekano mzuri na kung’aa na kusaidia mwili kuzalisha upya ‘collagen.’
Pia, anasema tiba hiyo hutumika kurejesha ngozi iliyoharibika au yenye makovu ya moto. Mbali na hayo, hutumika pia katika kupunguza na kudhibiti maumivu ya mwili.
Anasema pale mtu anapokuwa na maumivu katika sehemu fulani ya mwili, seli shina hupandikizwa katika eneo husika ili kusaidia kurejesha mishipa, ligament au cartilage (nyama laini zinazounganisha mifupa).
“Ingawa mifupa haiwezi kurejeshwa kikamilifu, viungo vingine vinaweza kurejeshwa kwa asilimia 90 hadi 100 kwa wanaume na wanawake,” anafafanua.
Anaeleza kuwa tiba urejeshaji ni pana, ingawa yeye huihusisha zaidi kwa malengo ya urembo.
Hata hivyo, amekuwa akihudumia watu wanaougua maumivu ya mwili wanaume na wanawake.
Anawashauri madaktari wengine kutumia vifaa vya seli shina kwa ajili ya tiba za urejeshaji kwenye taaluma zao mbalimbali.
Dk Arshni anasema hapa Tanzania, wapo madaktari wachache walioanza kutumia tiba hii hasa katika uwanja wa urembo na maono yake ni kuona tiba za urejeshaji zinapanuka katika mataifa yote ya Afrika.
“Tulianza Kenya, na sasa madaktari wengi wa fani tofauti wameanza kutoa huduma za urejeshaji kwa wagonjwa. Unaweza kuona jinsi madaktari wanavyowekeza kwenye tiba hizi. Ni muhimu madaktari kote Afrika kuanza kuzitumia, na bila shaka zitakua zaidi. Hata Tanzania zitapatikana kwa wingi kwa kuwa wapo wachache tayari wanaofanya hivyo,” anasema.
Pia, anasema amekuwa akifanya tiba za kutumia peptides kwa ajili ya kupunguza kasi ya kuzeeka (anti-aging), kupunguza uzito, kujenga misuli, kuponya vidonda kwani tiba hiyo ina matumizi mengi.
Anasema tiba hiyo ni mpya hata katika mataifa ya magharibi, bado ni taaluma changa.
Akifafanua tofauti kati ya upasuaji wa plastiki na tiba ya urejeshaji, anasema: “Tiba ya urejeshaji haina upasuaji (non-surgical), wakati upasuaji wa plastiki ni wa kufanyiwa upasuaji. Siyo kila mtu anafaa kufanyiwa upasuaji, na tafiti zinaonesha ni takribani asilimia 40 pekee ya watu wanaokidhi vigezo hivyo. Hapo ndipo tiba za urembo huingia kusaidia.”
Anasema si kila mtu anayetaka upasuaji anaweza kumudu gharama zake, hivyo watu wengi hupendelea tiba za urejeshaji badala ya upasuaji.
Kwa upande wa gharama, anasema tiba za urejeshaji ni nafuu zaidi zikianzia Dola 200 hadi 300 za Marekani kwa kila kikao, huku matibabu kamili yanaweza kufikia hadi Dola 10,000 za Marekani kutegemea na hali ya mgonjwa.
Hata hivyo, anasema wanajitahidi kuhakikisha huduma hizi zinabaki kuwa nafuu.
“Kipande kizuri cha tiba hizi ni kwamba tunashauri wagonjwa jinsi ya kupanga matumizi kulingana na kipato chao. Ikiwa mtu hawezi kumudu tiba kamili, kuna bidhaa zetu za dawa zinazosaidia urejeshaji, ingawa matokeo yake huchukua muda mrefu,” anasema.
Anasema kuna bidhaa za kifamasia maalumu kwa ajili ya watu wanaotaka kufanyiwa tiba ya urejeshaji lakini hawawezi kumudu gharama kamili.
Tiba za anti-aging zimekuwa gumzo kubwa kwa sababu kila mtu anataka kuonekana kijana, Dk Arshni anabainisha kuwa, watu wengi hufika na picha wakitaka kuonekana kama watu fulani, lakini yeye hufuata maadili ya kitaaluma na hukataa matakwa yasiyo ya kitaalamu licha ya kuwa kuna mahitaji makubwa.
“Ni jambo la kushangaza kuona kizazi cha sasa kinapendelea kuonekana kizuri, hata kama hakina uwezo wa kusaidia familia au kuweka chakula mezani,” anasema.
Anafafanua kuwa, peptides ni tiba za kinga (kinga ya kuzeeka), si tiba kamili. “Watu ambao bado hawajapata mikunjo hutumia dawa hizi kama kinga ili kuzuia mikunjo kujitokeza,” anasema.
Tanzania bado ipo katika hatua za awali, lakini baadhi ya wataalamu wa tiba za urejeshaji bado wanajifunza kutumia mbinu hizo katika matibabu ya ngozi, nywele na afya ya mwili kwa jumla.
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, Aidan Njau anasema kuna umuhimu wa huduma hiyo nchini kutokana na kuongezeka kwa uhitaji.
“Ni wengi wanahitaji hii huduma lakini katika upasuaji ni gharama, tiba urejeshaji ingawa ni teknolojia mpya ambayo hapa nchini haijaingia uwekezaji wake ni gharama.
“Katika uandaaji wa huduma na vifaa, lazima uwe na maabara nzuri inayoeleweka na kila kitu kinachohitajika,” anasema Dk Njau.
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Erick Muhumba anasema matibabu hayo ni teknolojia mpya na yana utofauti mkubwa na upasuaji wa kurekebisha maumbile.
“Kuna tofauti kubwa na tiba hii ambao kwa Tanzania tumeshaanza kuitoa, lakini ni tiba muhimu kuwepo nchini, maana watu wanaangalia matokeo iwapo haina madhara mengi na gharama zake zikoje,” anasema Dk Muhumba.
Baadhi ya wanawake wanasema huduma hiyo ni muhimu kwani wanawake wengi wanatamani kufanya urejeshaji wa miili lakini wanaishia kwenye huduma za kupaka pekee.
“Ukitumia losheni za collagen ni ngumu kupata matokeo ya haraka na haidumu ukiacha tu kuipata unarudi palepale, naamini ukipata tiba urejeshaji seli zako zitaendelea kujiendesha kama ulivyokuwa kijana,” anasema Naomi Barton mkazi wa jijini Dar es Salaam.