::::::::::
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025 leo, Oktoba 6, jijini Dar es Salaam, likiongozwa na kaulimbiu “Mission: Possible”.
Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha ubunifu, mshikamano na utayari wa kutatua changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wote nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, alisema kuwa maadhimisho haya ni fursa muhimu ya kutathmini namna shirika linavyotoa huduma kwa wateja, pamoja na kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya TTCL na wananchi. Alibainisha kuwa TTCL itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia za kisasa, kuboresha mifumo yake na kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania wote – mijini na vijijini.
Bi. Moshi alieleza kuwa ujenzi wa zaidi ya minara 1,400 ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini unaendelea kwa kasi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bila kikwazo. Aidha, alisisitiza kuwa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi wilaya zote ni msingi wa kukuza mawasiliano ya intaneti na sauti hadi ngazi ya jamii.
Katika hotuba yake, alieleza pia kuhusu huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako”, inayolenga kuwapatia wananchi huduma ya intaneti ya kasi na uhakika, kwa viwango vya kimataifa. Alisema huduma hiyo inaleta fursa zaidi katika uchumi wa kidijitali, elimu mtandaoni na huduma za kijamii, hivyo kuchochea maendeleo kwa wote.
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCHMEDIA