Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikiingia siku ya 39 kesho, Jumanne Oktoba 7, 2025, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameweka wazi mtazamo wake kuhusu mwenendo wa kampeni na wagombea 16 wa nafasi ya urais.
Sumaye, aliyehudumu nafasi ya Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, ametoa tathmini yake hiyo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Jumapili, Oktoba 5, 2025.
Akizungumzia mazingira ya uchaguzi huo, Sumaye amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeweka masharti yanayowawezesha wagombea wote kufanya kampeni kwa usawa, lakini bado kuna vyama vya upinzani vinasuasua kufanya kampeni zake.
“Safari hii wagombea wote wa urais wamepatiwa usafiri, mafuta na posho. Ingawa sisi hatuna uhakika wa kiwango, lakini kimsingi wote wamewezeshwa. Kwa hiyo huwezi kusema kuna chama ambacho mgombea wake hana uwezo wa kuzunguka kuomba kura. Wote wanafanya hivyo na wamepewa ratiba maalumu,” amesema Sumaye.
Hata hivyo, itakumbukwa, Agosti 28, 2025, akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, alisema walichofanya ni kukuza demokrasia.
“Sisi tulichofanya ni kukuza demokrasia. Tunataka uwanja uwe sawasawa kwa sababu kumekuwa na malalamiko kwamba wagombea hawapo kwenye usawa. Wengine wanasema Rais aliyepo madarakani ana faida ya kuwa na magari, sasa magari haya tumeyatoa kuweka uwanja kuwa sawa,” alisema.
Kulingana na ratiba ya INEC, wagombea waliokidhi vigezo waliteuliwa, na kila mgombea alikabidhiwa gari jipya lenye mafuta yaliyojaa tanki (kwa mujibu wa madereva).
Wagombea hao wamepewa madereva wa Serikali na ulinzi katika kipindi chote cha kampeni hadi siku ya kutangazwa matokeo.
“Gari hili unapewa kwa ajili ya kampeni. Kumbuka ni mali ya Serikali, ila unaruhusiwa kubadilisha stika kwa gharama zako, na utazitoa kwa gharama zako,” alisema kwa kurudia Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, wakati akiwakabidhi magari hayo kwa nyakati tofauti.
Kwa mujibu wa INEC, vyama 16 vya siasa vinaendelea na kampeni kuelekea uchaguzi huo utakaofanyika kote nchini Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Akifafanua zaidi, Sumaye amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeonekana kufanya kampeni kubwa zaidi ukilinganisha na vyama vingine.
Sumaye amesema wagombea wa upinzani hawajazuiwa kufanya kampeni, bali changamoto kubwa inayoonekana ni kwamba vyama vyao havijajijenga vya kutosha kwa wananchi. Hali hiyo, amesema, inasababisha kampeni zao kutopewa uzito na wananchi ambao huona baadhi ya ahadi zao haziwezi kutekelezeka.
Mbali na mwenendo wa kampeni, Waziri Mkuu huyo mstaafu amesema kwa ujumla kampeni za mwaka huu zinaendelea vizuri na zimekuwa na utulivu tofauti na ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.
“Kwa kawaida, kampeni za uchaguzi mkuu huwa na vurugu na maneno mengi, lakini mwaka huu nimeona zinafanyika kwa utulivu. Vyama vinafanya kampeni zao, sijasikia vurugu kubwa isipokuwa labda visa vidogo vidogo ambavyo havijasababisha mapambano,” amesema Sumaye alipoulizwa anaonaje mwenendo wa kampeni tangu zilipozinduliwa rasmi Agosti 28, 2025.
Amesema utulivu unaoonekana pia huenda umetokana na utekelezaji wa ajenda za 4R, ikiwamo ya maridhiano, ambazo Samia aliwahi kuahidi.
“Hata wale wasiohusika moja kwa moja kwenye majadiliano ya maridhiano walipewa nafasi ya kuwasilisha mapendekezo yao. Kwa hiyo utaona Rais aliweka mazingira ya majadiliano kabla ya uchaguzi, jambo ambalo limechangia kuwepo hali ya amani na utulivu katika kampeni,” amesema.
Hata hivyo, amekiri kwamba bado wapo watu na makundi yanayopinga baadhi ya masuala yanayojitokeza katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Lakini Sumaye amesema mijadala na upinzani unaoendelea hasa kupitia mitandao ya kijamii si jambo jipya, kwa sababu imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kila inapokaribia kufanyika uchaguzi mkuu.
Siasa za uanaharakati hazijengi
Waziri Mkuu huyo mstaafu amesema si dhambi kukosoa mambo ya kisiasa, lakini amesisitiza umuhimu wa namna ya kukosoa kunavyofanyika, akionya dhidi ya matusi na vitendo vya uchochezi vinavyofanywa hasa kupitia mitandao ya kijamii.
“Si dhambi kukosoa, lakini unakosoa kwa namna gani? Kwenye mitandao ya kijamii kuna watu wanatukana. Mimi nasema katika binadamu wako wa aina nyingi, na si mara ya kwanza kutokea watu wa aina hii nyakati za uchaguzi. Wapo pia wanaotamani kuona nchi yetu inachafuka, lakini hao hawafiki hata 10. Hata hivyo tunaamini nchi yetu ipo mikononi mwa Mungu na haitafika huko,” amesema Sumaye.
Ameongeza kuwa katika historia ya kisiasa ya Afrika, vyama vingi vilivyopigania uhuru au kuwa na misimamo isiyopendwa na wakoloni wa zamani, mara nyingi vimekuwa vikichukiwa, jambo ambalo Tanzania pia haikuachwa nyuma.
Akikumbuka alipokuwa Waziri Mkuu, Sumaye amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa ilikuwa ikikosolewa vikali na vyama vya upinzani vilivyokuwa na nguvu, lakini nguvu hiyo ilichanganyika na uanaharakati uliokwamisha ustawi wa siasa za ushindani.
“Kuna siku nilimwambia Rais wangu wakati huo, (marehemu Mkapa), naamini kama isingekuwa upinzani ule uliokuwa unanikwamisha, ningefanya kazi nyingi zaidi. Wakati ule vyama vya upinzani vilikuwa na nguvu, lakini badala ya kushindana kwa kukaza mwendo ili viifikie CCM, vilikuwa vikifanya kazi ya kukuvuta nyuma,” amesema.
Sumaye amesema anahisi huenda baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, ziliingia kwenye mfumo wa demokrasia si kwa hiari kamili, bali kwa shinikizo lililotokana na nguvu za kifedha kutoka mataifa ya nje.
“Kuna nyakati nafikiri tulirukia mfumo wa vyama vingi mapema au tuliingizwa kwa nguvu ambazo sisi wenyewe hatukuwa tumezifikia. Nchi ikiwa tayari imepata uhuru, haipaswi tena kuendeleza uanaharakati. Tatizo la vyama vingi vya Afrika ni kuendelea kutumia uanaharakati hata baada ya uhuru, jambo linalosababisha fujo zisizo na tija kwa wananchi,” amesema.
Amefafanua kuwa kujenga chama cha siasa si kazi ngumu endapo kitajengwa kwa misingi sahihi ya siasa safi na kujitenga na uanaharakati.
“Tatizo ni kwamba vyama vingi havijajitofautisha na uanaharakati, ndiyo maana mara nyingine wanakamatwa na polisi, kwa sababu hakuna kiongozi atakayekubali nchi iingie kwenye vurugu,” amesema.
Akigusia mifano ya vurugu zinazofanywa na kizazi kipya katika baadhi ya nchi, Sumaye amesema hatua hizo hazileti maendeleo bali huacha hasara kubwa kwa wananchi.
“Unapoharibu miundombinu, matengenezo yake yanahitaji pesa, na mwisho wa siku wananchi ndiyo watalipa gharama hizo kupitia kodi zao. Gen Z anaweza kufikiria hayamhusu kwa wakati huo, lakini baada ya miaka mitano au kumi, atakapokuwa analipa kodi, ataona gharama hizo zimemrudia,” amesema.
Kwa mtazamo wake, mabadiliko ya kisiasa hayapaswi kutafutwa mitandaoni wala kwa fujo, bali kupitia sanduku la kura.
“Nashauri watu wasiangaike na maneno ya mitandaoni kuhusu uchaguzi. Wasiache kupiga kura, kwa sababu kama Watanzania tukiamini kuna nafuu upande wa pili, mabadiliko yapatikane kupitia kura, tusije tukaiga wengine,” amesema.
Amesema wale wanaosema hawaridhishwi na CCM wana haki ya kuunda chama kipya cha siasa kitakachowapa matumaini badala ya kususia uchaguzi.
Kuhusu nafasi ya CCM kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Sumaye amesema matarajio hayo yako wazi kutokana na mwitikio anaouona miongoni mwa wananchi.
“Mimi naratibu Kanda ya Kaskazini katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Ukiwa mratibu unaona mbele kukoje. CCM itashinda kwa sababu ya muitikio wa watu.
“Vyama vingine havijafanya kazi ya siasa kwenye ngazi za chini. Mfano, unakuta mgombea wa udiwani wa upinzani hana hata wanachama kwenye kata anayogombea, sasa atawezaje kushinda?” amehoji