Pantev aanza kazi rasmi Simba, afunguka kumaliza utawala wa Yanga

MENEJA mpya wa Simba, Dimitar Pantev, Oktoba 6, 2025 ameanza kazi ya kukinoa kikosi hicho, huku akiweka bayana kuridhishwa na ubora wa wachezaji aliowakuta baada ya kufanya tathmini ya awali akisema asimilia 80 wanaweza kufikia malengo msimu huu ikiwamo ubingwa ambao umechukuliwa na Yanga misimu minne mfululizo.

Moja ya malengo ya Simba msimu huu ni kuhakikisha inarejesha mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) ambayo inayasotea kwa misimu minne mfululizo pamoja na kufika mbali katika michuabno ya CAF ikiwa ipo raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Dimitar aliyewasili wikiendi iliyopita akitokea Gaborone United ya Botswana akiwa na msaidizi wake, Boyko Simeonev kwa sasa ana siku 11 za kuandaa kikosi hicho kwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini itakayopigwa Oktoba 18, 2025 ugenini kabla ya kurudiana Oktoba 26, 2205 jijini Dar es Salaam.

Kocha huyo raia wa Bulgaria amesema katika uchambuzi wake wa awali ameridhishwa kwa zaidi ya asilimia 80 na hali ya kikosi, akieleza wachezaji wengi wanaonekana kuwa na sifa za kuendana na falsafa alizonazo na kwamba anaona kuna dalili za mafanikio akiwa na kikosi hicho.

PANT 01


“Nilichokiona kwa wachezaji mmoja mmoja katika tathimini yangu kimenipa matumaini. Hii ni timu yenye vipaji vikubwa, kila mmoja ana kitu cha tofauti. Kazi yangu ni kuhakikisha tunatengeneza mfumo wa pamoja unaojumuisha uwezo wa kila mmoja,” amesema Dimitar aliyewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Cameroon na Botswana akiwa na timu za Victory United na Gaborone United mtawalia.

Tofauti na Fadlu Davids ambaye mara nyingi alipendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao umekuwa ukilenga uwepo wa uwiano katika kulinda na kushambulia kutokana na kuwa na viungo wawili wenye uwezo mkubwa zaidi wa kulinda, Dimitar ni muumini mkubwa wa mfumo wa 4-3-3.  “Tutaona namna bora zaidi ambayo inaweza kutufanya kuwa bora kama timu uwanjani, tutaenda hatua kwa hatua, naamini inawezekana na ndio maana nipo hapa,” amesema kocha huyo.   

Mfumo wa Dimitar unajikita zaidi katika mashambulizi ya moja kwa moja kupitia winga na mshambuliaji wa kati mmoja, huku viungo watatu nyuma wenye sifa tofauti wakiwa na jukumu la kusukuma timu mbele. 

PANT 02


Uwepo wa wachezaji kama vile, Ellie Mpanzu, Charles Jean Ahoua, Kibu Denis, Morice Abraham, Joshua Mutale, Ladack Chasambi na Mohammed Bajaber ambaye yupo njiani kurejea ni silaha muhimu kwa timu hiyo katika kuwafungua wapinzani wao.

Uwezo wa kukaa na mpira mguuni, unaweza kutoa nafasi ya kutengeneza nafasi za kutosha kwa washambuliaji wa mwisho, Jonathan Sowah, Seleman Mwalimu ‘Gomes’  na hata Steven Mukwala. Katika mechi tano ambazo Simba imecheza msimu huu mashindano yote mbili chini ya Fadlu na tatu Seleman Matola na Hemed Suleiman ‘Morocco’, imeshinda tatu ikiwemo mbili za Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate na Namungo na sare ya 1-1 dhidi ya Gaborone ziliporudiana baada ya kushinda ya kwanza Botswana (1-0) na kupoteza 1-0 katika Ngao ya Jamii mbele ya Yanga. 

Timu hiyo imefungwa jumla ya mabao manane, ina wastani wa kufunga mabao mawili kwenye kila mechi, imeruhusu mabao mawili tu. 

PANT 03


Akiwa na Gaborone msimu uliopita, Dimitar aliiongoza kushinda mechi 20, sare sita na kupoteza mechi nne, alikifanya kikosi hicho kuwa na wastani wa kufunga karibu mabao mawili katika kila mechi sawa na wastani wa 1.8. 

SAFARI ESWATINI
Kwa mujibu wa ratiba ilivyo Simba itaondoka nchini Oktoba 16 na Shirika la Ndege la Air Tanzania hadi Afrika Kusini kisha kupanda ndege nyingine kwa ajili ya kuingia Eswatini.

PANT 04


Kabla ya kuwafuata Nsingizini Hotspurs, Simba itakuwa na mechi mbili za kirafiki ili kujiweka sawa, moja ya mechi hizo inaelezwa itachezwa keshokutwa Alhamisi dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambayo nayo imefuzu raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitarajiwa kuvaana na Polisi Kenya.

Al Hilal inaitumia mechi hiyo dhidi ya Simba kujiweka fiti kabla ya kuvaana na Polisi iliyowatoa Mogadishu City ya Somalia, wakati wapinzani wao hao wakiing’oa majirani zao za Jamus ya Sudan Kusini kwa faida ya bao la ugenini kutokana na mattokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 3-3.