Vodacom Tanzania Yaadhimisha Miaka 25 ya Huduma Katika Wiki ya Huduma kwa Wateja: Urithi wa Ujumuishi na Ubunifu Unaomlenga Mteja

Wakati dunia ikiadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Vodacom Tanzania PLC inajivunia kusherehekea miaka 25 ya huduma ya mabadiliko, ikithibitisha tena dhamira yake ya kutoa huduma jumuishi, zenye uwezo na ubunifu kwa kila mteja hapa nchini.

Ili kuanza wiki hii, Vodacom imezindua duka jipya (Vodashop) la huduma jumuishi kwa wateja katika kituo kipya cha East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam. 

Duka hilo lina dawati maalum la huduma kwa watu wenye mahitaji maalum, likionyesha dhamira ya Vodacom ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma, heshima na ubunifu unaomlenga mteja.

“Wiki ya Huduma kwa Wateja ni muda wa kuungana na wateja wetu na kusherehekea mahusiano tuliyojenga kwa miaka yote. 

Tunapoadhimisha miaka 25 ya kuwaunganisha na kuwawezesha wateja wetu, tunajivunia kuimarisha ajenda yetu ya ujumuishi kupitia upanuzi wa huduma zetu na uzinduzi wa dawati lingine la huduma kwa watu wenye mahitaji maalum,” alisema Philip Besiimire, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara na Masoko, Brigita Shirima, alisisitiza kuwa safari ya ujumuishi ya Vodacom inaonekana kupitia mipango inayolenga wateja wenye mahitaji maalum Pamoja na wale wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

“Kuanzia wakalimani wa lugha ya alama na msaada wa video kupitia WhatsApp kwa wateja viziwi, huduma za haraka kwa wateja wasioona ambao wamesajiliwa kwetu, hadi njia za kuingilia madukani kwa kutumia viti mwendo (wheelchair) na sasa madawati ya huduma yanayofikika kwa urahisi kwa wateja wenye mahitaji maalum, juhudi hizi zinaonyesha dhamira yetu ya kuhakikisha kila mteja anahudumiwa kwa heshima, uangalifu na urahisi,” alisema Brigita.

Akifafanua shughuli zilizopangwa kwa wiki hii, Belinda Wera, Mkuu wa idara ya Huduma kwa Wateja na Huduma za Kidijitali, alieleza, “wiki hii tutawatambua na kuwasherehekea si tu wateja wetu bali pia washirika wetu katika mfumo wa M-Pesa pamoja na timu zinazofanya kazi usiku na mchana kuwahudumia wateja. 

Tukitambua kuwa hatupo peke yetu, tutakuwa na shughuli za kurudisha kwa jamii kama njia ya kuwashukuru kwa msaada wao wa kudumu kila wakati.”

Kwa Vodacom, huduma kwa wateja si jukumu la idara moja tu, bali ni utamaduni uliojengwa kwa miaka 25 ya ubunifu unaomlenga mteja. 

Kila mwingiliano, iwe kupitia huduma za kidijitali, washauri wanaotoa msaada au majukwaa kama VodaTube, unaangazia dhamira ya kampuni ya kuwawezesha wateja.

 Kwa kurahisisha uelewa wa kidijitali na elimu ya kifedha, Vodacom inawezesha maamuzi sahihi na kufungua uwezo kamili wa teknolojia ya simu.

Kampuni inapoingia katika sura yake inayofuata, Vodacom inabaki na dhamira ya kuendeleza ubunifu wenye lengo la kuunda Tanzania iliyounganishwa, jumuishi na yenye kutoa huduma kwa wote.