Wawili wafariki ajalini, gari la mizigo na basi zikigongana Geita

Geita. Watu wawili wamefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo ikihusisha basi la Kampuni ya Mallesa’s  na gari la mizigo aina ya Canter kugongana uso kwa uso.


Ajali hiyo imetokea saba usiku wa kuamkia leo Oktoba 7, 2025, katika Kijiji cha Lumasa, Kata ya Butengorumasa, wilayani Chato mkoani Geita. 

Aidha, gari la mizigo lililogongana na basi hilo inaelezwa kuwa lilikuwa likitokea Jijini Mwanza kuelekea wilayani Kibondo mkoani Kigoma likiwa limebeba vifaa vya ujenzi, ambapo basi   lilikuwa likitokea jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Geita.


Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema watu wawili wamefariki dunia ambao walikuwa katika gari dogo la mizigo.


“Ni kweli ajali imetokea na watu wawili waliokuwa ndani ya gari la mizigo wamepoteza maisha,” alisema Kamanda Jongo, na kuongeza kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea ambapo ameahidi kutoa taarifa kamili baada ya taratibu za   kiuchunguzi kukamilika.