Dar es Salaam. Wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kikijipanga kuanza kutoa elimu kwa njia ya mtandao, kimewapika wakufunzi wake ili waendane na mabadiliko hayo.
Mafunzo hayo yamezinduliwa Oktoba 6, 2025 jijini Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uwezo wakufunzi hao juu ya namna gani ya kutumia mfumo huo kama sehemu ya kuboresha mbinu za ufundishaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Naibu Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Liberato Haule amesema chuo hicho kinatarajia kuongeza mbinu ya ufundishaji kwa njia ya mtandao kuanzia mwaka wa masomo unaoanza Novemba 2025.

Dk Haule amesema kwa kuanza mbinu hiyo ya ufundishaji kwa njia ya mtandao itaanza kutumika kwa kozi takribani 98 zilizojikita katika fani za Uhandisi, Sayansi, Teknolojia, Biashara, Elimu, Sanaa na Lugha.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwapa fursa watu wengi zaidi kupata elimu ya juu pamoja na kuongeza ufanisi wa kitaaluma.
“Mbinu hiyo itakapoanza kutumika itawapa fursa wengi waliokuwa na ndoto ya kusoma Udsm kupata fursa hiyo, wataweza kuwa na machaguo kujifunza kwa njia ya mtandao au ana kwa ana,” amesema.
Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Mtandaoni (Centre for Virtual Learning) cha Udsm, Dk Fatuma Simba amesema kupitia mfumo huo wataweza kuwafikia wanafunzi katika mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi bila ya wao kulazimika kufika chuoni.
“Changamoto tunayoipata ni kuwafikia wote wenye vigezo vya kusoma elimu ya juu maana kuwaleta wote miundombinu inakuwa haitoshelezi ila kupitia teknolojia ya tehama tutawafikia wengi zaidi popote walipo,” amesema.
Pia, amesema hatua hiyo itasaidia chuo kuendelea na shughuli zake za utoaji wa elimu hata inapotokea majanga.
“Kama mnakumbuka kipindi cha Uviko-19, vyuo vilifungwa lakini tukitumia Tehama hata inapotokea changamoto za aina hiyo, bado tutaendelea kutoa elimu,” amesema.
Dk Simba amefafanua kuwa mfumo huo utakaokuwa unatumika kufundishia una uwezo wa kubaini iwapo mwananfunzi atafanya udanganyifu wa kitaaluma ‘Plagiarism’.
“Mfumo wetu tumeuunganisha na programu ambayo inaangalia udanganyifu wa kitaaluma, inaangalia kazi iliyowasilishwa na mwanafunzi ni kwa kiwango gani imehusisha matumizi ya akili mnemba (AI) au amechukuwa kazi ya watu wengine,” amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema hatua hiyo ni sehemu ya mradi wa HEET unaolenga kufanya wahitimu watakaozalishwa waweze kuendana na soko la ajira katika karne ya 21.

Pia, amesema inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 huku ukilenga kuifanya Udsm kuwa kinara wa mageuzi ya elimu ya juu ya kidijitali barani Afrika.
“Tunataka elimu ya juu Tanzania iwe ya kufikika, yenye kubadilika kulingana na mahitaji ya maendeleo ya taifa letu,” amesema.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Profesa Boniface Rutinwa, amesema Udsm inawekeza katika mafunzo kwa wahadhiri ili waendelee kutumia mbinu shirikishi na bunifu za kufundisha mtandaoni bila kupoteza ubora wa elimu.
Kwa upande wake, Profesa Benadeta Killian, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayehusika na Mipango, Fedha na Utawala, ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa HEET Udsm, amesema mageuzi hayo ya kidijitali ni sehemu ya juhudi za kuoanisha elimu ya juu na vipaumbele vya kiuchumi vya taifa.