Yafahamu majukumu mazito ya Pantev Simba

SIMBA imemtambulisha Dimitar Pantev kuwa Meneja Mkuu wa klabu hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kuondoka kwa Kocha Mkuu, Fadlu Davids. Kumbuka tayari Pantev ameanza kazi rasmi kikosini hapo Oktoba 6, 2025 huku akiwa na majukumu mazito yanayomkabili.

Kuanza kwake kazi ndani ya Simba, kuna maswali mengi watu wanajiuliza imekuaje atambulishwe kama Meneja Mkuu badala ya Kocha Mkuu? Hiyo inatokana na aliyeondoka Fadlu kuwa kocha mkuu na mrithi wake alipaswa kuchukua nafasi hiyo na si vinginevyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Kumuita Pantev Meneja maana yake sisi tumebadilisha muundo wetu, kwa maana yeye ndiye atakayesimamia uendeshaji mzima wa kikosi hicho.

“Pantev atahusika na mapendekezo ya mchezaji gani asajiliwe, wa kuachwa, wa kutolewa kwa mkopo, kufuatilia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja na tathimini ya ujumla ya kikosi chetu, ndio maana tukampa cheo hicho ili isiwe ndani ya uwanja tu, bali shughuli zote ahusike mwenyewe.”

Hata hivyo, mtaani kuna mjadala unaomuhusu Pantev kuitwa Meneja Mkuu badala ya Kocha Mkuu. Mjadala huo unaingiliana na ukweli uliopo kwamba Pantev ana leseni ya UEFA A, tofauti na inayotakiwa ya UEFA Pro kwa ajili ya kusimama kama kocha mkuu kufundisha timu ya Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ya CAF.


Licha ya kuwepo kwa mjadala huo, rekodi zinaonyesha Pantev katika timu nyingi alizopita amekuwa akitambulika kama Meneja na sio kocha.

Ndani ya Simba baada ya Fadlu kuondoka sambamba na wasaidizi wake akiwemo  Darian Wilken (Kocha Msaidizi), Wayn Sandilands (Kocha wa Makipa), Durell Butler (Kocha wa Utimamu) na Mueez Kajee (Mchambuzi wa Video), Seleman Matola amebaki ambaye alikuwa Kocha Msaidizi.

Uwepo wa Matola mwenye vigezo vya kusimama kama kocha mkuu wa timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Bara na michuano ya CAF, kunaifanya Simba kuendelea kuwa na benchi la ufundi imara.

Pantev aliyepewa mkataba wa miaka miwili ndani ya Simba, amesema: “Ni mapema sana kuahidi chochote kwa sasa, ila ninachoweza kuwaambia mashabiki watarajie aina nzuri ya uchezaji kwa sababu ndio kitu muhimu kwetu na wenzangu.”

MAJUKUMU HALISI YA MENEJA MKUU

Kwa kutambulishwa kama Meneja Mkuu wa timu, moja kwa moja Pantev anakabiliwa na majukumu makuu manne ndani ya timu hiyo. Kwa kawaida Meneja Mkuu wa timu majukumu yake ni pamoja na kufafanua mkakati wa jumla wa klabu, kuajiri na kusimamia wachezaji, kupanga mbinu na vipindi vya mazoezi, kutoa motisha kwa timu, kusimamia fedha na bajeti, kushughulika na vyombo vya habari, na kuwakilisha klabu kwa wadau wa nje.

Meneja Mkuu anafanya majukumu yake kama kiongozi mkuu wa timu, akisimamia shughuli zote zinazohusiana na mpira wa miguu uwanjani na nje ya uwanja ili kufikia malengo ya klabu.

Majukumu ya Meneja Mkuu wa timu yamegawanyika kwenye makundi manne ambayo ni majukumu ya kimkakati, usimamizi wa wachezaji, uendeshaji wa klabu na biashara sambamba na mawasiliano na uwakilishi.

MAJUKUMU YA KIMKAKATI NA KIMBINU

Mbinu za timu: Kukuza na kutekeleza mikakati ya mchezo, miundo na mifumo ya uchezaji ya mechi.

Mafunzo: Kupanga na kutoa vipindi vya mafunzo vilivyopangwa, vinavyohusika, na vinavyolenga maendeleo kwa wachezaji.

Maono na malengo: Kuweka malengo ya timu na maono na mwelekeo wa muda mrefu wa klabu.


Kuajiri wachezaji: Kutafuta, kusaini na kufanya biashara ya wachezaji kwenye soko la uhamisho.

Ukuzaji wa timu: Kukuza ukuaji na maendeleo ya wachezaji, pamoja na wale walio katika timu za vijana.

Uteuzi wa kikosi: Kuchagua kikosi cha kwanza.

UENDESHAJI WA KLABU NA BIASHARA

Usimamizi wa bajeti: Kusimamia bajeti za timu, malipo ya wachezaji, na kuhakikisha kuwa fedha ziko ndani ya mgao.

Ukuaji wa kifedha: Kuchangia faida ya klabu kwa kusimamia fedha, ufadhili na uuzaji.

Usimamizi wa Vifaa: Kuhakikisha vifaa muhimu, ikiwa ni pamoja na mipira ya mechi, vinapatikana na katika utaratibu mzuri wa kufanya kazi.

MAWASILIANO NA UWAKILISHI

Mahusiano ya vyombo vya habari: Kufanya kazi kama uso wa umma wa timu, kutoa mahojiano kabla na baada ya mechi kwa vyombo vya habari.

Mawasiliano ya ndani: Kuwasiliana na wachezaji, makocha, uongozi wa klabu na wajumbe wa kamati.

Uwakilishi wa klabu: Kuwakilisha klabu katika masuala rasmi na kukuza maadili yake.

Huyu ni raia wa Bulgaria aliyezaliwa Juni 26, 1976, jijini Varna, kwa sasa ana umri wa miaka 49. Ana leseni UEFA A inayotolewa na Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA).

Simba ni timu ya tano kwa Kocha Pantev barani Afrika, kabla ya hapo amezinoa Victoria United ya Cameroon, FC Johansen ya Sierra Leone, Orapa na Gaborone United za Botswana.

Kabla ya kuwa kocha, amecheza soka hadi ngazi ya Ligi Kuu ambapo alikuwa akicheza kwenye nafasi ya kiungo.


Akiwa mchezaji amezitumikia timu za Cherno More, FC Suvolovo, Chernomorets Byala, Kaliakra Kavarna, Chernomorets Balchik, Volov Shumen, Dobrudzha, Vladislav, Shabla na Spartak Varba.

Katika miaka ya mwisho ya uchezaji wake kabla ya kustaafu, Pantev alikuwa akicheza na kufundisha kuanzia mwaka 2006 hadi 2016 alipostaafu rasmi kucheza.

Maisha yake ya ukocha yalianzia katika kikosi cha vijana cha Varna City kisha akawa Kocha Msaidizi wa Al Ahli Hebron kisha akawa Kocha Mkuu katika timu za Flamengo, Victoria United, Johansen, Orapa na baadaye Gaborone United.

Katika miaka hiyo mitano aliyofundisha Afrika, ametwaa mataji mawili ya ligi Kuu katika timu mbili kutoka mataifa mawili tofauti ambayo ni ya Ligi Kuu Cameroon na Ligi Kuu Botswana.

Muda mwingi ameutumia kufundisha mchezo wa Futsal na ametwaa mataji matano ya Ligi Kuu Bulgaria ya mchezo wa Futsal.

Ameondoka Gaborone United akiwa ameitumikia kwa muda wa miezi nane (siku 254) tangu alipojiunga nayo Januari 23 mwaka huu.

MUDA ALIOKAA KATIKA TIMU ALIZOPITA

Dobrudzha Dobrich ya Bulgaria (Alikuwa meneja msaidizi kuanzia Julai 1, 2008 hadi Juni 30, 2009 alikaa kwa takribani siku 364 sawa na miezi 11 na siku 30.

FC Vladislav  ya Bulgaria (Alikuwa kocha mchezaji kuanzia Julai 1, 2009 hadi Juni 30, 2010, alikaa kwa takribani siku 364 sawa na miezi 11 na siku 30).

FC Shabla ya Bulgaria (Alikuwa kocha mchezaji katika timu hii ya nchini Bulgaria kuanzia Julai 1, 2010 hadi Machi 1, 2011, alikaa kwa takribani siku 243, sawa na miezi nane.

FC Grand Pro ya Bulgaria (Kuanzia Machi 1, 2011 hadi Juni 30, 2015, alikuwa meneja wa timu hii ambapo alikaa kwa takribani siku 1,573 sawa na miaka minne, miezi mitatu na siku 20).

Spartak Varna ya Bulgaria (Alikuwa kocha kwa takribani siku 334 sawa na miezi kumi na siku 30. Hiyo ilikuwa kuanzia Agosti 1, 2015 hadi Juni 30, 2016).

FC Grand Pro ya Bulgaria (Kuanzia Agosti 1, 2016 hadi Januari 30, 2017, alikuwa meneja wa timu hii, ni kipindi cha takribani siku 182 sawa na miezi 6).

Ahli Al-Khaleel ya Palestina (Alikuwa meneja msaidizi kuanzia Desemba 1, 2018 hadi Mei 30, 2019, hizo ni takribani siku 180 sawa na miezi mitano na siku 29).

FC Alshoban ya Palestina (Alikuwa meneja kuanzia Juni 15, 2019 hadi Desemba 31, 2019, ni takribani siku 199 sawa na miezi 6 na siku 17 alizokaa hapo).

H16 Sports Club ya Dubai (Alikuwa meneja kuanzia Januari 10, 2020 hadi 30/07/2021 ni siku 567 sawa na mwaka mmoja, miezi sita na siku 20).

Svetkavitsa ya Bulgaria (Alikuwa meneja kuanzia Agosti 12, 2021 hadi Oktoba 8, 2021, ni siku 57 sawa na mwezi mmoja na siku 26). Flamengo KSA ya Saudi Arabia (Alikuwa meneja kuanzia Januari 10, 2022 hadi Juni 30, 2022, hizi ni siku 171 sawa na miezi mitano na siku 20).

Victoria United ya Cameroon (Alikuwa meneja kuanzia Julai 13, 2022 hadi Septemba 30, 2022, ni siku 79 sawa na miezi miwili na siku 18).

FC Johansen ya Sierra Leone (Alikuwa meneja kuanzia Februari 1, 2023 hadi Juni 30, 2023, ni siku 149, sawa na miezi minne na siku 29).

Victoria United ya Cameroon (Alikuwa meneja kuanzia Machi 21, 2024 hadi Mei 31, 2024, ni siku 71 sawa na miezi miwili na siku 10).

Orapa United ya Botswana (Alikuwa meneja kuanzia Julai 1, 2024 hadi Desemba 1, 2024, ni siku 153 sawa na miezi mitano na siku mbili).

Gaborone United ya Botswana (Alikuwa meneja kuanzia Januari 20, 2025 hadi Oktoba 03, 2025, ni siku 256 sawa na miezi minane na siku 13).