WATOTO WAPEWE ELIMU YA MAZINGIRA MAPEMA KUWA MABALOZI WA UHAIFADHI

Kisarawe, Pwani

MIONGONI mwa mikakati muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kuwekeza katika elimu ya mazingira kwa watoto, ili wawe mabalozi wa kulinda na kuhifadhi mazingira wanapokua.

Wito huo umetolewa na Rahim Mselem, mdau wa elimu, wakati wa mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Madugike wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, ambapo amesisitiza kuwa elimu ya mazingira inapaswa kuanza tangu hatua za awali za malezi.

 “Elimu kuhusu mazingira ni silaha muhimu ya kulinda afya za binadamu na uoto wa asili. Kila mzazi na mwanafunzi anapaswa kuwa mfano wa vitendo katika kutunza mazingira kwa kupanda miti, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuepuka uharibifu wa mazingira,” alisema Mselem.

Ameongeza kuwa elimu bora haiwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa mazingira safi na salama ya kujifunzia, huku akiwataka wazazi na jamii kushiriki kikamilifu katika juhudi hizo.

Katika kuboresha miundombinu ya elimu, Mselem alibainisha kuwa serikali imetoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Madugike, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Aidha, aliahidi kuwalipia wanafunzi 20 ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuchangia chakula shuleni, akisisitiza kuwa lishe bora ni sehemu muhimu ya mafanikio ya kielimu.

Mselem pia aliahidi kushughulikia changamoto za shule hiyo zikiwemo ukosefu wa vifaa vya TEHAMA, samani za ofisi, nyumba za walimu, kisima cha maji na uzio wa shule, ili kuboresha mazingira ya kufundishia na usalama wa wanafunzi.

Akitambua nafasi ya michezo katika mtaala mpya wa elimu, Mselem alisema:

 “Michezo ni sehemu ya kujifunza na inaweza kuwa kitega uchumi kwa vijana. Watoto wenye vipaji wasikatishwe tamaa.”

Alikabidhi jezi na mipira kama mchango wake wa kuendeleza michezo shuleni hapo.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Madugike, Ramadhan Juma Kihiyo, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka sita wanaandikishwa katika darasa la awali, akisema hatua hiyo ni msingi muhimu wa mafanikio ya kielimu.