Chuo Kikuu Mzumbe kimezindua kampeni ya utoaji chanjo ya homa ya ini (Hepatitis B) kwa watumishi wake ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulinda afya na ustawi wa rasilimali watu ndani ya taasisi hiyo ya elimu ya juu nchini.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kampasi Kuu ya Morogoro, na umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo, wataalamu wa afya na watumishi huku takribani watumishi 900 katika kampasi zote za chuo hicho nchini watapatiwa chanjo hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha amesema kampeni hiyo inalenga kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini ambao ni miongoni mwa magonjwa hatarishi yanayosababisha vifo vingi duniani.
“Chuo chetu kinatambua thamani ya rasilimali watu, ndiyo maana tumeamua kuanzisha mpango huu wa chanjo. Homa ya ini ni ugonjwa hatari unaoweza kuathiri maisha na uzalishaji kazini. Nasisitiza watumishi wote wachukue hatua hii muhimu bila visingizio vyovyote,” amesema Prof. Mwigoha.
Kwa upande wake, Dkt. Mhamedi Ayub, amesema kuwa ugonjwa wa homa ya ini huambukizwa kwa njia ya majimaji ya mwili kama damu, mate na pia kwa njia ya kujamiana hivyo watu wanaobadilisha wapenzi mara kwa mara wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi hayo.
“Ugonjwa huu unaweza kuishi mwilini kwa muda mrefu bila dalili, lakini madhara yake ni makubwa. Chanjo ni kinga bora zaidi, na tunawahimiza watumishi wote kutumia fursa hii,” alisema Dkt. Mhamedi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni 254 duniani wanaishi na maambukizi sugu ya homa ya ini aina ya B, huku zaidi ya milioni 1.2 wakipata maambukizi mapya kila mwaka. Aidha, mwaka 2022 vifo vinavyohusiana na homa ya ini B na C vilifikia takribani milioni 1.3 duniani.
Nchini Tanzania, tafiti za kiafya zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kiko kati ya 3.8% hadi 8.0% kulingana na makundi ya watu, huku wastani wa kitaifa ukiwa takribani 6.9% ya watu wazima. Wataalamu wa afya wanasema takwimu hizi zinaonyesha umuhimu mkubwa wa kampeni za chanjo na elimu ya kinga katika jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Afya na Huduma za Kitabibu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Nyangara Rajabu Mtilly, alisisitiza umuhimu wa chanjo kwa watumishi, akibainisha kuwa inalinda dhidi ya homa ya ini aina ya Hepatitis B, ambayo huambukizwa kupitia damu, majimaji ya mwili, na kutoka mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua.
Aidha, alibainisha kuwa zoezi la kupata chanjo linafuata utaratibu wa kupima afya kwanza kabla ya mtu kupata chanjo. Chanjo ya Hepatitis B hutolewa kwa watu wazima kwa awamu tatu ili kuhakikisha kinga kamili, huku watoto wachanga wakipatiwa chanjo mara tu baada ya kuzaliwa. Katika Kampasi Kuu ya Morogoro, zoezi hilo litaendelea tarehe 10 Oktoba 2025, ikifuatiwa na Ndaki ya Mbeya kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba 2025, na Ndaki ya Dar es Salaam kuanzia tarehe 20 hadi 24 Oktoba 2025.
Baadhi ya watumishi waliopata chanjo wameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuanzisha mpango huo, wakisema utasaidia kulinda afya zao na kuongeza ufanisi kazini.
“Tunampongeza uongozi wa chuo kwa kutuleta huduma hii hapa kazini. Wengi tulikuwa hatujui madhara ya ugonjwa huu, lakini sasa tumeelimishwa na tumepewa kinga,” alisema mmoja wa watumishi waliochanjwa. Amesema Mariam Rajabu