Unguja. Uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025 kwa nafasi ya urais, wabunge, wawakilishi na madiwani nchini, kampeni zake zinaendelea kushika kasi.
Kwa upande wa Zanzibar, watapiga kura kwa siku mbili, ikimaanisha kutakuwa na kura ya mapema itakayopigwa Oktoba 28.
Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 2018 inayoitaja kura ya mapema na kuwataja wanaotakiwa kushiriki katika kura hiyo.
Kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya Uchaguzi ya Mwaka 2018, Zanzibar kutakuwapo na kura ya mapema na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itaandaa kanuni inayoeleza kura ya mapema itapigwa kabla ya uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa sheria, kura hiyo inawatambua watendaji wote wanaoshughulika na uchaguzi, walinzi wote wanaoshughulika na usimamizi siku ya uchaguzi, wamepewa haki yao ili kutimiza majukumu yao bila changamoto zozote.
Hata hivyo, kuwapo kwa kura ya mapema kunagonganishwa vichwa vya wanasiasa visiwani hapa na kwa nyakati tofauti, huku baadhi ya wagombea wameonesha kutofautiana na wengine wakikubalina nayo na wengine wakiipinga.
Chama cha ACT – Wazalendo kimekuwa mstari wa mbele kupinga kura ya mapema kwa madai hiyo ni mbinu itakayosababisha waibiwe kura.
Kabla ya mchakato wa kampeni, chama hicho kupitia kwa viongozi wake, walikuwa wakisema hawapo tayari kusikia jambo la kura ya mapema na wakawa wanaishinikiza tume kufanya marekebisho kabla uchaguzi na kutoruhusu jambo hilo lifanyike.
Hata hivyo, kadri muda ulivyokuwa ukipita na ZEC kuonesha msimamo kwa mujibu wa sheria, chama hicho kilianza kusema hawatasususia uchaguzi lakini hawatakuwa tayari kuona kura ya mapema ikpigwa.
Kauli hizo mara kadhaa zilikuwa zikitamkwa na mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman ambaye kwa sasa ndiye mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.
Hata hivyo, baada ya kuanza mchakato wa uchaguzi na kuanza rasmi kampeni, Othman katika baadhi ya mikutano yake amenukuliwa akisema Serikali imekubali kwenda kwenye kura ya mapema, siku hiyo wanachama wa ACT – Wazalendo watatoka kuwasindikiza.
“Kura ya mapema haina maana katika kisiwa kidogo kama cha kwetu, lakini siku hiyo wakitoka kwenda kupiga kura na sisi tutawasindikiza,” alisema Othman akisema hivyo mara kadhaa kwenye mikutano yake ya kampeni.
Kutokana na msimamo wa ACT – Wazalendo, umekiibua Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeeleza msimamo wake katika hilo na kauli zinazotolewa na upande mwingine.
CCM inasema kura ya mapema ipo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi na wahusika wa kura hiyo wanatambulika kisheria.
Hivyo, inasema kitendo cha wengine kutaka kujitokeza siku ya kura Oktoba 28 ambao sio wahusika, ni dalili za kutaka kuleta chokochoko ya kuvunja amani.
Msimamo huo umepigiliwa msumari hivi karibuni na mgombea urais wa chama hicho Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika mkutano wa kampeni uwanja wa Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja
Wakati akihutubia wananchi na wafuasi wa chama hicho kwenye mkutano katika viwanja vya Kidimni Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk Mwinyi aliwaeleza wasidanganyike na mtu akajitokeza siku hiyo kwenda kupiga kura kwa sababu wahusika wanatambuliwa na sheria.
Alisema kitendo cha kuhamasishwa kujitokeza siku hiyo ni dalili za kutaka kuleta chokochoko ya kuvunja amani kwa sababu wahusika wanajulikana.
“Nimeanza kusikia kuna watu wanataka kusindikiza wapigakura siku hiyo, ndugu zangu hiyo ni dalili ya kutaka kuvunja amani, mkisikia mtu anakwambieni kutoka majumbani mwenu siku hiyo, kama wao ni hodari waache watoke wenyewe,” alisema Dk Mwinyi.
Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina anasema sheria bado ni ile ile haijabadilishwa na ndio itakayotumika katika uchaguzi mwaka huu akirejea akifafanua wanaotakiwa kupiga kura siku husika.
“Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaeleza wazi kwamba,kutakuwepo na upigaji wa kura ya mapema na ZEC imetoa kanuni inayooeleza kuwa, kura ya mapema itapigwa siku moja kabla ya uchaguzi,” anasema
Hoja ya kura ya mapema kipindi cha nyuma iliwahi kushupaliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AAFP), Said Soud Said kiasi cha kuipeleka mahakamani akipinga kuwapo kwa kura ya siku mbili.

Hata hivyo, kwa siku za hivi karibuni Soud amebadili mawazo na kuanza kuonesha kukubalina nayo.
Alisema tume haina kosa, inatekeleza sheria lakini sheria hiyo inatakiwa kutolewa tafasiri na Mahakama kwa kuzingatia misingi ya Katiba.
“Kwa sasa nilishaondoa msimamo huo baada ya kuona hakuna sababu na jambo hilo lipo ksheria na tunapaswa kuheshimu sheria, sisi tunaona sawa na waaotaka kuhamasisha kusiwepo kura ya mapema basi wajue wanafanya kosa,” anasema Soud.
Kwa nyakati tofauti katika mchakato wa kuchukua fomu, kurejesha na kuanza kampeni, Soud alisikika akisema kura ya mapema ipo kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo hakuna budi kukubaliana nayo na iwapo wakitaka hilo lisiwepo, ni vyema wakapitia mchakato wa kupeleka hoja barazani ili ikafutwe.
Wengine wanaokubalina na kura hiyo, ni pamoja na mgombea wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA),, Khamis Faki Mgau anasema siku hiyo ipo kisheria, kwa hiyo wanaopinga watakuwa na masilahi binafsi.
Pia, Mgombea wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib anakubalina na hoja hiyo kwamba, kura ya mapema ipo kwa mujibu wa sheria kwa hiyo hawana kipingamizi nayo na wanaoipinga huenda wana ajenda ya siri.

Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Ada Tadea, Georges Gabriel Bussungu akinadi sera zake kisiwani Pemba.