Geita. Dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter, lililogongana na basi la abiria katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, amefariki dunia, huku abiria wawili walikuwamo kwenye basi wakijeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea saa mbili usiku katika Kitongoji cha Kitongo, Kata ya Butengorumasa, Wilaya ya Chato.
Tukio hilo limehusisha gari aina ya Mitsubishi Canter, lililokuwa likiendeshwa na Said Ramadhan (23), mkazi wa Kibondo mkoani Kigoma, ambaye amefariki dunia katika ajali hiyo.

Pia, watu wawili wamejeruhiwa ambao walikuwa abiria katika basi la Kampuni ya Mallessa’s, lililogongana na Cante, ambalo lilikuwa likiendeshwa na Charles Mathayo (43), mkazi wa Geita.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa kwenye mtandao wa Jeshi la Polisi nchini leo, Oktoba 7, 2025, imebainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter, ambaye alihama upande wa barabara bila kuchukua tahadhari dhidi ya watumiaji wengine wa barabara.

‘’Uzembe wa dereva wa Mitsubishi Canter ambaye alihama kutoka upande wake na kwenda upande wa kulia pasipo kuchukua tahadhari au kuzingatia watumiaji wengine wa barabara, kisha kuligonga basi hilo na kusababisha kifo, majeruhi na uharibifu wa vyombo vya usafiri,’’ imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mbali na kifo cha dereva wa gari la Mitsubishi Canter, Said Ramadhan (23), taarifa hiyo ya polisi imetaja majeruhi wawili walionusurika katika ajali hiyo ambao ni abiria wa basi, Annastazia Yohana (25) na Ismail Omar (34), wote wakazi wa Dar es Salaam. Wamepata majeraha na kwa sasa wanaendelea kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Katoro.