RAUNDI ya kwanza ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), imemalizika ikiacha majeraha kwa baadhi ya timu huku zingine zikipata mwelekeo mzuri wa mechi zijazo.
Uhamiaji ni miongoni mwa timu zilizoanza kwa kufungua msimu na ushindi ikiwa ugenini, na mchezaji wake Adam Issa kuonyeshwa kadi nyekundu huku Mohamed Mussa akifungua pazia la kufunga bao la kwanza la msimu katika mechi iliyochezwa Septemba 25, 2025 kwenye uwanja wa Mao A, Mjini Unguja.
Kati ya timu nne zilizopanda daraja kucheza ZPL msimu huu, Fufuni kutokea Pemba ndio pekee iliyoibuka na ushindi wa mabao 3-1 ikiichapa Kipanga, tatu zikianza kwa kufungwa katika mechi zake.

Timu hizo zilizopanda daraja ni Polisi na New King za Unguja, Fufuni na New Stone Town kutoka Pemba. Polisi ilianza kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka Uhamiaji katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa msimu 2025-2026 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mao A, Mjini Unguja, Mwembe Makumbi iliikaribisha New King kwa kuifunga mabao 3-1 mechi iliyochezwa Septemba 29, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A Unguja.
Pia, katika mechi iliyochezwa Oktoba Mosi 2025, kati ya JKU na KVZ, ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku timu ya JKU ikipata bao la tatu lililokataliwa na mwamuzi ikidaiwa mfungaji aliotea. Mbali na hilo, kadi nyekundu nne zilitolewa katika raundi hiyo ambapo adhabu hiyo walikumbana nayo Kassim Ali wa KVZ, Tarik Mohammed wa JKU, Adam Issa wa Uhamiaji na Yussuf Makame kipa wa New King.

Timu ya Mafunzo imekuwa ya kuwanza kufunga mabao mengi katika ligi hiyo ikiichapa New Stone mabao 4-0, huku New Stone ikiwa ndiyo iliyoruhusu mabao mengi. Junguni imeacha sintofahamu baada ya kufika uwanjani bila ya jezi katika mechi iliyopangwa kuchezwa Septemba 26, 2025 dhidi ya Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba. Mechi hiyo ilivunjwa na KVZ kupewa pointi tatu na mabao mawili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali amesema ligi hiyo imekuwa na ushindani mkubwa kwa raundi hiyo kwa sababu ya kila moja kuhitaji kuvuna alama tatu na kuipa muelekeo mzuri timu yake.
Amesema, raundi hiyo haikuwa rahisi kwao kutokana na ubora wa kila timu kwani zimejipanga kushinda na hilo limethibitishwa uwanjani.

Kocha Mkuu wa JKU, Seif Nassor amewataka waamuzi kuwa makini kwa lengo la kutenda haki kwa kila timu ili ligi hiyo kuipa ubora unaostahili.
Kocha Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh amesema timu hiyo kuonyeshwa kadi katika mechi ya mwanzo haijawa athari kwani wana kikosi kipana kinachoweza kuziba nafasi hiyo.
Amesema katika kipindi cha maandalizi timu zilitumia nafasi hiyo kuvijenga vikosi kimwili, kisaikolojia na kiufundi na matokeo yanayopatikana ni mavuno.