MAMBO yanazidi kupamba moto ndani ya kikosi cha TRA United baada ya mabosi wapya wa timu hiyo kupokea maombi ya makocha 500, walioomba kazi huku mchujo ukitarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii.
TRA United ambayo hapo awali ilikuwa ikiitwa Tabora United, tangu msimu uanze imekuwa haina kocha mkuu ikiongozwa na kocha msaidizi, Mkenya, Kassim Ottieno.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa TRA United, Christina Mwagala amesema ni kweli muda wa kusaka kocha mkuu wa timu hiyo umefika na wameshapokea maombi.
Amesema mchujo unaendelea na Ijumaa kamati itapitisha majina ya makocha waliopita, hivyo mpaka wiki ijayo nafasi hiyo itakuwa imekwishapata mrithi.
“Wametuma maombi makocha 500, ila kama tunavyojua haiwezekani kwa wote kupitishwa lazima apatikane mmoja, kwani msaidizi tayari yupo na wachezaji.

“Ijumaa majina yaliopitishwa yatatoka, ila niseme tu makocha walituma maombi ni wengi na wakubwa, hivyo siwezi kuwataja wote, ila wiki ijayo atapatikana mmoja,” amesema. Miongoni mwa timu zilizomaliza vyema msimu uliopita TRA ni miongoni mwao, ikishika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi, licha ya kuwa na rekodi ya kubadili makocha.
Msimu huu wa 2025-2026 TRA imecheza mechi mbili za ligi, huku ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji na 0-0 dhidi ya Pamba Jiji.